Adverts

Feb 2, 2011

EXIM BANK kujitanua zaidi mwaka huu

EXIM BANK kujitanua zaidi mwaka huu: "

Meneja Mkuu wa Exim Bank (Tanzania) Limited, bwana Dinesh Arora, alipokuwa akijibu hoja mbalimbali za wateja waliojumuika naye kwa hafla fupi ya chakula cha jioni mwishoni mwa wiki

Katika utekelezaji wa mpango mkakati wake wa kuzidi kuwa karibu zaidi na wananchi, Benki ya Exim (Tanania) Limited, inatarajiwa kujitanua zaidi mwaka huu kwa kufungua matawi matano zaidi katika sehemu mbalimbali nchini, ikiwa ni pamoja na kuongeza matawi zaidi katika jiji la Dar es salaam.

Hayo yamebainishwa na Meneja Mkuu wa benki hiyo, Bw. Dinesh Arora, mwishoni mwa wiki katika hafla ya chakula cha pamoja na wafanyibiashara mbalimbali jijini Mbeya, ambapo alitaja mikoa mingine itakayonufaika na mpango huo kwa mwaka huu kuwa ni ile ya Dodoma, Shinyanga na Kigoma. hafla hiyo ilifanyika katika ukumbi wa hoteli ya Beaco, jijini Mbeya na kuhudhuriwa na watu mbalimbali.

Mbali ya kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi wa Tanzania, meneja huyo amesema kuwa, benki yake itaendelea pia na mpango wake wa kujitanua zaidi hata nje ya mipaka ya Tanzania, kwa kufungua matawi kwenye nchi jirani ya Zambia, ambapo tayari taratibu za kukamilisha mpango huo zimekaribia mwishoni na kwamba ufunguzi wa matawi hayo ya nje ya nchi unatarajiwa kufanyika wakati wowote.

Bw. Arora, ambaye pia alitumia wasaa huo kuainisha mafanikio na vikwazo mbalimbali ambavyo wamekuwa wakikabiliana navyo, alisema kuwa, ufunguzi wa matawi ya Exim Bank, nchini Zambia, unafuatia mafanikio makubwa ambayo wameyapata kutoka katika matawi ya benki hiyo yaliyoko visiwa vya Comorro na kwamba wanatarajia kuwa mpango huu utazidi kuiweka benki yao katika nafasi ya mafanikio zaidi.

“Exim Bank, ndio benki pekee binafsi ya Kitanzania, ambayo imekuwa ikitanua wigo wa huduma zake hadi nje ya nchi yetu, na tunajivunia mpango huu ambao sisi ndio wa kwanza kuutimiza na tunatarajia kuwa utaendelea kuinufaisha benki kwa kiasi kikubwa na hivyo wateja wetu pia kuendelea kunufaika na huduma zetu zenye kiwango cha kimataifa” alisema Bw. Arora.

Naye mwakilishi wa mkuu wa mkoa katika hafla hiyo, bibi Bertha Swai, alimpongeza meneja huyo kwa huduma zao ambazo wamekuwa wakizitoa katika tawi lao lililoko jijini Mbeya, sanjari na ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za kijamii ikiwa ni pamoja na uchangiaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo.

Meneja Mkuu wa Exim Bank Bw. Arora (kulia), akiteta jambo na Meneja wa Exim tawi la Mbeya, Bw. Geoffrey Kitundu (katikati, huku wakisikilizwa na afisa masoko wa tawi hilo bi. Dorothy Rutatika

Alisema kuwa, mkoa wa Mbeya ni moja ya mikoa yenye fursa mbalimbali za kiuchumi na kimaendeleo hivyo anatarajia kuwa benki zenye kutoa huduma zake mkoani hapa, zitaleta hamasa zaidi kwa wananchi kujishughulisha na miradi hiyo ya kimaendeleo kwa kuwapatia miongozo muhimu ya kijasiriamali ikiwa ni pamoja na mikopo yenye masharti nafuu.

Nao wafanyibiashara mbalimbali waliokuwa wamejumuika na wafanyakazi wa benki hiyo pamoja na meneja wao mkuu, walitoa pongezi zao kwa uongozi wa tawi na benki hiyo kwa ujumla kutokana na huduma zao zilizobora, huku wakiahidi kuendelea kuipa ushirikiano wa dhati benki hiyo kwa lengo la kuendelea kuinua uchumi wa mkoa wa Mbeya kwa ujumla.

Hata hivyo, waliiomba benki hiyo kuangalia uwezekano wa kuongeza matawi zaidi mkoani hapa, ikiwa ni pamoja na sehemu za wilayani ili wananchi zaidi wanufaike na huduma zao, ombi ambalo meneja mkuu wa Exim, Bw. Arora, alisema amelichukua na ataliwasilisha katika mamlaka husika kabla ya kufikiwa maamuzi ambayo alisema anaamini yatakuwa yenye lengo la manufaa kwa pande zote mbili.

Benki ya Exim, ni benki ya kibiashara ambayo ilianza kutoa huduma zake nchini mwaka 1997, na tawi la Mbeya ilifungua mwaka 2009, ambapo kwa mujibu wa Meneja wa Tawi hilo, Bw. Geoffrey Kitundu, hadi sasa wana wateja wapatao 6000 huku idadi ya wateja wao ikitarajiwa kuzidi kuongezeka kutokana na mikakati ambayo tawi limejiwekea ili kuhakikisha kuwa linawapatia wananchi wa kawaida huduma zenye kiwango cha kimataifa kwa gharama zilizo nafuu sana.

"