Adverts

Feb 6, 2011

HOTUBA YA MWENYEKITI CCM TAIFA TAREHE 5 FEB

"
HOTUBA YA MWENYEKITI WA CCM TAIFA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KATIKA SHEREHE ZA
KUTIMIZA MIAKA 34 YA KUZALIWA KWA CCM
UWANJA WA JAMHURI, DODOMA
TAREHE 05 FEBRUARI, 2011
CCM Oyee!
Kidumu Chama Cha Mapinduzi!
Ndugu William Kusila; Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Dodoma;
Ndugu Lt. Mst. Yusuf Makamba, Katibu Mkuu wa CCM;
Waheshimiwa Wabunge;
NduguViongozi mbalimbali mlioko hapa;
Ndugu Wana-CCM na
Ndugu Wananchi;
Utangulizi:
Naomba nianze kwa kuwashukuru wenyeji wetu, viongozi, wana-CCM na wananchi wa Dodoma kwa mapokezi mazuri na kwa maandalizi mazuri ya sherehe hii. Sherehe zimefana sana. Sisi sote ni mashahidi. Vile vile matembezi ya mshikamano yalikuwa mazuri ingawaje umbali ulikuwa mfupi kidogo. Safari ijayo tufikirie kuongeza umbali.
Kwa vile ni mara ya kwanza kukutana nanyi tangu uchaguzi mkuu umalizike, napenda kutumia nafasi hii kuwashukuru wananchi wote wa mkoa wa Dodoma kwa kuchagua CCM. Mkoa huu mmekipa CCM ushindi mnono, mmekuwa ngome kubwa ya CCM. Imani huzaa imani. Napenda kuwaahidi kuwatumikia kwa moyo na uwezo wangu wote. Tutakamilisha kazi tuliyoianza na kutekeleza ahadi zetu zilizomo katika Ilani na zile za papo kwa papo kwa pamoja. Naomba kila mkoa na wilaya watuletee orodha ya yale tuliyoaahidi ili tuyatengenezee mipango ya utekelezaji.
Ndugu zangu;
Leo ni siku muhimu katika historia ya Chama cha Mapinduzi. Ni siku ambayo tunapiga ndege wawili kwa jiwe moja. Tunasherehekea miaka 34 ya kuzaliwa kwa CCM na tunasherehekea ushindi mnono tulioupata katika uchaguzi mkuu uliopita.
Ndugu Wana-CCM na Ndugu Viongozi;
Siku ya leo, kama nilivyokuwa nasema wakati wote, ni siku ya kufanya tathmini ya mafanikio ambayo Chama chetu kimepata na changamoto zinazotukabili na namna ya kuzitafutia ufumbuzi. Aidha, ni wakati wa kuweka malengo na mwelekeo wetu kwa siku za usoni.
Ni ukweli ulio wazi, tena wa kujivunia, kwamba katika miaka 34 ya uhai wake, Chama chetu kimepata mafanikio makubwa. Kimeendela kukua na kimezidi kuimarika kwa kila hali. Wanachama wameongezeka sana na kufikia takriban milioni 5.7. Wanachama wake ni watu wenye umoja, mshikamano na ushirikiano wa hali ya juu pamoja na kuwepo kwa changamoto za hapa na pale kwa nyakati fulani fulani.
Kwa sababu hiyo, Chama cha Mapinduzi kimeweza kufanya mambo mengi mazuri na ya kujivunia katika nchi yetu. Tumejenga taifa lenye umoja, amani, utulivu na maendeleo yanazidi kupatikana mwaka hadi mwaka. Najua wapo wenzetu wanaopenda ukweli huo usionekane kwa kukuza changamoto za hapa na pale. Hata changamoto hizo tuna uwezo nazo, suala lililopo ni kuwa huwezi kufanya mambo yote wakati mmoja. Hata Mwenyezi Mungu asiyeshindwa na lolote aliumba dunia kwa siku sita na siyo siku moja. Hii inatufundisha kuwa na subira na kupanga vizuri mipango yetu.
Uchaguzi Mkuu 2010
Ndugu zangu, viongozi wenzangu, na Wanachama wenzangu;
Kwa sababu ya mema mengi tuliyoifanyia nchi hii na watu wake ambayo yanaonekana wazi na kujisemea yenyewe, Chama cha Mapinduzi kimeendelea kuaminiwa na wananchi wa Tanzania kama nguzo na kimbilio lao la kupata majawabu ya uhakika kwa matatizo yanayowakabili. Ndiyo maana tumeendelea kupewa ridhaa ya kuongoza nchi hata tangu mfumo wa vyama vingi uanze mwaka 1992 mpaka leo. Mimi sina wasiwasi kabisa kuwa kama tutaendelea kuwatendea mema Watanzania na kuboresha taswira ya Chama chetu tutaendeelea kushinda katika chaguzi nyingi zijazo.
Ndugu Viongozi, Wana-CCM Wenzangu na Wananchi Wenzangu;
Ukweli huu ndiyo uliotupatia ushindi mnono katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba, 2010 pamoja na vitimbi na mbinu chafu tulizofanyiwa na wapinzani wetu. Wakati mwingine haya yanayoendelea sasa ya vurugu zinazofanywa na wapinzani wetu ni hasira ya hasara waliyoipata, hasa wakikumbuka kiasi walichowekeza, pamoja na ubaya na hujuma mbalimbali walizotutendea bila ya mafanikio. Wanasahau Mola ndiye mtoaji. Akiandika kupata unapata.
Hivi sasa wanakula njama za kutaka wapate kile walichokosa kwenye kura za wananchi kwa njia ya maandamano, migomo na kuchochea ghasia. Nalo wanajidanganya, kamwe hawatafanikiwa. Napenda kuwahakikishia wana-CCM na wananchi wenzangu wote pamoja na hao wanaohangaika usiku na mchana kupanga njama ovu na hujuma dhidi yangu na Chama cha Mapinduzi kuwa hawatafanikiwa ng’o. Wananchi wengi wa Tanzania ni werevu na wanajua kupambanua ukweli na uongo na zuri na baya. Hawatawafuata watu hasidi na wasioiombea mema nchi yetu na watu wake. Nawasihi msiwasikilize na msiwafuate watu ambao hawajali mateso watakayopata watu wengine ili mradi tu maslahi yao binafsi yanaendelezwa.
Ndugu Zangu Wana-CCM Wenzangu na Ndugu Wananchi;
Tembeeni kifua mbele, acheni unyonge, tupo na tutakuwepo. Tutamaliza miaka yetu mitano kwa salama na heshima na tutashinda kwa kishindo mwaka 2015 kwa nafasi zote. Wakati mwingine ninapoona wana-CCM mnakuwa wanyonge kwa matokeo ya uchaguzi uliopita huwa nashangaa sana. Najiuliza kwa nini?
Tumemsikia Katibu Mkuu akitueleza kuwa katika uchaguzi wa Rais, mgombea wetu alipata kura 5,276,827 aliyemfuata alipata kura 2,271,942. Tofauti ya kura milioni 3 zisizokuwa na ubishi. Kwa upande wa Ubunge wa Majimbo kati ya viti 239, CCM ilipata viti 187 (78.2%), wenzetu wamegawana viti 52 (21.8%) kama ifuatavyo:- CUF viti 24 (10%), CHADEMA viti 22 (9%), NCCR –Mageuzi viti 4 (1.7%), TLP na UDP walipata kiti kimoja kimoja (0.4%) kila kimoja. Katika Viti Maalum 102, CCM imepata viti 67 wenzetu wamegawana viti 45. Katika jumla ya viti 341, CCM inavyo viti 254 na wenzetu wana 87. Nani mwenye nguvu kubwa?
Kwa nini tujisikie wanyonge baada ya kupata ushindi mnono kiasi hicho? Nadhani tunatishwa na kelele na propaganda za Chama fulani na Bwana fulani ambazo zinajenga hisia kama vile wako wengi sana na wamepata ushindi mkubwa sana hata kuliko CCM. Hilo si kweli, ingawaje safari hii wamepata viti vingi kuliko uchaguzi uliopita. Ukweli ni kwamba Chama hicho kimepata asilimia tisa tu ya viti vyote vya Majimbo.
Chama chetu, kwa maana ya Viongozi, wanachama na makada, lazima tujipange vizuri kukabiliana na propaganda hizi za wachache. Hali kadhalika, tujipange kimkakati ili uchaguzi ujao viti tulivyowaazima tuvichukue tena wenyewe. Lazima tuazimie sasa kufanya hivyo na kujiandaa kisawasawa kwa ajili hiyo. Wakati wote tusisahau kanuni muhimu ya siasa kwamba “mwisho wa uchaguzi mmoja ni mwanzo wa matayarisho ya uchaguzi mwingine”. Ndugu zangu huu ndiyo wakati wa kujipanga kwa ajili ya 2015.
Tathmini ya Uchaguzi Uliopita
Wana-CCM Wenzangu;
Jambo la kwanza muhimu sana kufanya katika kujipanga kwa uchaguzi ujao ni kufanya tathmini ya kina ya uchaguzi uliopita. Lengo letu kuu ni kutambua nguvu zetu na udhaifu wetu uko wapi na makosa gani tulifanya katika uchaguzi uliopita. Lengo letu ni kuimarisha nguvu zetu na kurekebisha kasoro zetu na kusahihisha makosa yetu. Katika tathmini hiyo pia tuangalie nguvu za wapinzani wetu zilikuwa kwenye maeneo gani na udhaifu wao ulikuwa wapi na kisha tutumie udhaifu huo kwa manufaa yetu.
Tumeagiza kila ngazi tangu shina hadi taifa ifanye tathmini yake. Taarifa ya ngazi ya chini ipelekwe ngazi ya juu. Mwezi ujao mwishoni tutafanya vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa kufanya tathmini kwa ngazi ya taifa. Nawasihi viongozi wenzangu mlichukulie zoezi hili kwa uzito unaostahili. Ushindi wa Chama chetu unategemea sana mafanikio tutakayofanya katika zoezi hili na tutakavyotekeleza yale tutakayokubaliana kufanya. Naomba muifanye kazi hii kwa utulivu, umakini na bila ya jazba. Tusigeuze vikao hivi kuwa ni vya kugombana na kukomoana pamoja na haja ya kuwa wakweli na wawazi. Wenye jazba na hasira hawatajenga bali watabomoa. Tunataka tutoke katika vikao hivyo tukiwa wamoja zaidi wenye ari zaidi na nguvu zaidi.
Ndugu Viongozi na Ndugu Wana-CCM Wenzangu;
Jambo la pili muhimu kufanya katika kujipanga vizuri kwa uchaguzi ujao ni kuimarisha Chama. Baada ya uchaguzi kumalizika kazi yetu ya kwanza ni kuziba nyufa na kutibu majeraha yaliyotokea kuanzia kura za maoni miongoni mwa wagombea na washabiki wao. Katika maeneo mengi tuliyoshindwa au hata kufanya vibaya katika uchaguzi, mgawanyiko wakati wa kura za maoni umechangia sana. Baadhi ya wana-CCM waliacha kupiga kura au hata kudiriki kupigia kura wagombea wa upinzani kwa sababu ya hasira. Hatuna budi kuyatambua maeneo hayo na hatua za haraka zichukuliwe kupatanisha pande zilizonuniana na kufanyiana vitendo vya uhasama.
Tujiimarishe Kiuchumi
Ndugu Wana-CCM;
Jambo jingine muhimu katika kuimarisha Chama ni kujenga uwezo wa kiuchumi wa Chama cha Mapinduzi. Hali ya kifedha ya Chama chetu siyo imara. Tunategemea mno ruzuku inayotokana na ushindi wetu kwa upande wa Wabunge na Madiwani. Kwa ajili hiyo vyanzo vya asili vya Chama kupata fedha za kuendesha Chama vimesahaulika. Miaka yote ada na michango ya wanachama vilikuwa ndizo nguzo na vyanzo vikuu vya mapato ya Chama. Siku hizi baada ya mfumo wa vyama vingi na utaratibu wa ruzuku kwa vyama kuwepo, vyanzo asilia vimeachwa kabisa. Hili ni kosa lazima tujirekebishe haraka. Hatuwezi kuacha jukumu la kugharamia uendeshaji wa Chama chetu mikononi mwa wafadhili matajiri. Tunahatarisha uhuru wa Chama chetu.
Bahati mbaya safari hii ruzuku hiyo imepungua kwa sababu ya nguvu ya vyama vya upinzani kuongezeka. Uchaguzi ujao nguvu ya upinzani ikiongezeka zaidi tutakuwa na hali mbaya. Lazima tuanze safari ya uhakika ya kuacha kutegemea ruzuku kuendesha Chama. Tutafute vyanzo vingine na hasa uwekezaji. Bahati nzuri fursa ziko nyingi kila mahali na Chama chetu kina rasilimali nyingi zinazoweza kutumika kwa ajili hiyo. Hatujazitumia ipasavyo. Sasa lazima tufanye, vinginevyo hatma yetu itakuwa mbaya. Tujipange vyema katika ngazi zote kuhakikisha kuwa rasilimali zilizopo zinatambuliwa na kutumika kukiwezesha Chama kiuchumi. Kisha tuwe wabunifu kutafuta fursa na maeneo mapya ya uwekezaji tuwekeze. Rasilimali isiyotumika ni mtaji mfu.
Mageuzi Ndani ya Chama
Ndugu Wana-CCM Wenzangu;
Jambo jingine muhimu sana kufanya ni kuanza mchakato wa mageuzi ya ndani ya Chama chetu ili kujiweka katika nafasi nzuri zaidi ya kushindana na kushinda katika uchaguzi ujao. Chama chetu ni cha siku nyingi jambo ambalo lina faida na hasara zake. Kwa sababu ya kujulikana sana na uzoefu wake kinaweza kuwa na fursa ya kupata ushindi hasa pale ambapo watu wameridhika na matendo yake au wana hofu na mabadiliko.
Lakini upande mwingine wa sarafu kuwepo muda mrefu inaweza kuwa ndiyo hatari yetu. Wakati mwingine watu wanaweza kutaka mabadiliko tu hata kama Chama kinafanya mazuri ila kwa sababu ya kukinahi au kutaka kuwajaribu wengine waone. Hatari inakuwa kubwa zaidi pale Chama kitaposhindwa kuwaridhisha watu au kuwaudhi kwa baadhi ya mambo pamoja na matendo ya viongozi. Kwa sababu hiyo, CCM lazima wakati wote ibaki kuwe Chama cha matumaini ya mambo mapya mazuri kwa wananchi. Kitoe matumaini ya kuwa Chama cha kuleta mabadiliko yenye tija na Chama kinachotenda mema.
Kwa maneno mengine, Chama cha Mapinduzi kiige tabia ya nyoka ya kila baada ya muda fulani hujivua gamba lake na kupata jipya. Hatuna budi kufanya hivyo na kufanya hivyo sasa. Wakati wa vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa vya tathmini tutalijadili pia suala zima la mageuzi katika Chama. Nitapenda tuelewane juu ya namna tutakavyotekeleza agenda hii muhimu kwa uhai na maendeleo ya Chama chetu. Hili ndugu zangu haliepukiki. Lazima tukihuishe ili kukiongezea mvuto mbele ya watu. Tuutazame muundo wetu kama unakidhi haja. Tuwatazame viongozi watendaji kama wanakidhi haja na kama siyo mzigo unaokipaka matope Chama chetu. Wale tunaoweza kuachana nao sasa tuachane nao kwa maslahi mapana ya Chama chetu.
Kutafuta Wanachama Wapya
Ndugu Wana-CCM na Ndugu Wananchi;
Uhai wa Chama unategemea zaidi wanachama. Hivi sasa Chama chetu kinao wanachama milioni 5.7. Tuendelee kuongeza wanachama katika Chama na kuhakikisha kuwa wanajiandikisha kupiga kura. Aliyejiandikisha ni bora zaidi kwani ni mtaji wa ushindi. Asiyejiandikisha hana manufaa hayo, labda uhamasishaji wa watu kuunga mkono CCM. Hiyo pekee haitoshi. Hivyo, tuwasisitize wanachama wetu wote kujiandikisha kupiga kura ili wachangie ushindi wa Chama chetu. Pia tuwasisitize watimize wajibu wao wa msingi wa uanachama wa kulipa ada na kushiriki katika shughuli mbalimbali za Chama katika ngazi zote.
Utekelezaji wa Ilani ya CCM
Ndugu Wana-CCM na Ndugu Wananchi;
Jukumu la msingi la Chama kufanya katika kujipanga kwa ushindi wa 2015 ni kusimamia utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015. Hii ndiyo ahadi kuu tuliyoitoa kwa wananchi na ndiyo mkataba wetu nao. Tukiitekeleza vizuri tutakuwa tumetimiza ahadi. Watu watatuona waungwana na kuendelea kutupenda na kutuchagua. Tusipotekeleza watatukasirikia na hatari yake tunaielewa sote. Wabunge, Madiwani na Mawaziri ndiyo watu wetu wa mstariwa mbele wa mapambano ya kuhakikisha tunatimiza ahadi.
Sisi katika Chama, kupitia vikao vyetu halali tuhakikishe kuwa viongozi wetu hao wanawajibika ipasavyo kuhusu utekelezaji wa Ilani. Tuwabane kisawasawa katika hayo. Pia naomba tutambue kuwa wenzetu wana mkakati maalum wa kuzua mambo kila siku ili watutoe kwnye mstari tuache kutekeleza Ilani ili waje kusema kiko wapi. Tujenge uwezo wa kujibu hoja lakini tusiache kutekeleza mipango yetu.
Katiba
Ndugu Wana-CCM na Ndugu Wananchi;
Mwaka huu CCM inapotimiza miaka 34, sehemu moja ya Muungano (Tanzania Bara) inatimiza miaka 50 tangu ipate Uhuru wake kutoka kwa Wakoloni. Nilishaelekeza kuwa tuisherehekee siku hiyo kwa heshima inayostahili kama taifa lililofikisha umri huo. Naomba viongozi na wananchama wa CCM kushiriki kwa ukamilifu katika sherehe hizi. Ni sherehe zetu sote kwani ukiandika historia ya Uhuru wa Tanganyika lazima uitaje CCM kwa maana ya TANU iliyoungana na ASP kuanzisha CCM. Kila Tawi, kila Kata, kila Wilaya na kila Mkoa waandae namna watakavyosherehekea siku hiyo adhimu.
Ndugu Wana-CCM na Ndugu Wananchi;
Miongoni mwa mambo mengine ambayo tutayafanya mwaka huu ni kuanzisha mchakato wa kuitazama upya Katiba ya nchi yetu kwa nia ya kuihuisha na hatimaye kuzaa Katiba mpya inayolingana na taifa lenye umri wa miaka hamsini na itakayotupeleka miaka 50 ijayo. Kiserikali matayarisho yanaendelea ya kupeleka Bungeni Mswada wa Sheria wa kuanzisha mchakato huo ikijumuisha kuundwa kwa Tume ya kuongoza mchakato huo.
Kuanzishwa kwa mchakato huo kutazima kiu za wananchi waliotaka mchakato huo uanze. Napenda kuwahakikishia wananchi wenzangu kuwa sisi katika Serikali na CCM ni miongoni mwa wadau wakubwa wanaotaka Katiba ihuishwe kukidhi mahitaji ya wakati tulionao na matarajio yetu ya baadaye. Sisi sote ni wadau wa mabadiliko ya Katiba yetu ya sasa. Hata kama kusingekuwepo mapendekezo ya CUF, CHADEMA na wengineo ilikuwa ni dhamira yetu kufanya hivyo.
Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi wananchi kuwa watulivu na subira. Aidha, niwaombe kuwa wakati huo ukifika wana-CCM na wananchi kujitokeza kwa wingi katika kutoa maoni na katika kupiga kura ya maoni itakayoidhinisha Katiba hiyo. Katiba ni mali ya wananchi hivyo tunataka tuwashirikishe kwa ukamilifu katika hatua zote muhimu.
Utawala wa Sheria
Ndugu Wana-CCM na Ndugu Wananchi;
Katika hotuba yangu ya mwisho wa mwaka 2010, nilidokeza taarifa ambazo vyombo vya usalama vinazo kuhusu mipango ya makusudi ya uvunjifu wa amani kwa kutumia njia ya migomo na maandamano. Niliwatanabaisha ndugu zangu kutambua njama hizo na kuepuka kushiriki katika maandamano au migomo ya aina hiyo. Wanaoandaa wana agenda yao ya kisiasa iliyojificha nyuma ya jambo linalotangulizwa kama sababu. Wanataka kujitengenezea mazingira ya ushindi mwaka 2015 kwa vurugu. Nilitahadharisha kuwa watu wajiepushe kugeuzwa mbuzi wa kafara kwa kuendeleza maslahi ya kisiasa ya watu fulani fulani.
Niliyoyasema yametokea Arusha na dalili zipo za mipango ya namna ile kuandaliwa kutokea sehemu nyingine hapa nchini. Napenda kurudia tena kuwasihi Watanzania wenzangu msiwasikilize wala kuwafuata wanasiasa hao. Wanawasakizia kwenye hatari ambayo mnaweza kuiepuka. Naomba muwakumbushe tena kuwa wanayo fursa Bungeni na kwenye majukwaa mbalimbali kutoa hoja zao badala ya kuwagombanisha nyinyi na vyombo vya dola. Niwaombe wanasiasa wenzangu kutumia fursa tele walizonazo badala ya njia ya uvunjifu wa amani na kuhatarisha maisha na mali za watu pamoja na kuharibu sifa ya nchi yetu.
Dowans
Ndugu Wana-CCM na Ndugu Wananchi;
Jambo ninalotaka kulizungumzia sasa sikutaka kulizungumza kwa sababu Waziri Mkuu alishalifafanua baada ya semina ya Wabunge wa CCM na hata Mheshimiwa John Chiligati, Katibu wa Siasa na Uenezi Taifa alishalizungumzia. Sikuona umuhimu wa kufanya hivyo kwa sababu viongozi wenzangu hao wameelezea kwa ufasaha uamuzi wa Kamati Kuu na ule wa kikao cha pamoja cha Wabunge wa CCM.
Lakini, yapo maneno mengi ati mbona Rais yupo kimya sana, hatujamsikia kusema chochote? Niseme nini zaidi na hao wote wameshasema kwa niaba yangu. Wapo wanaosema nipo kimya kwa sababu nahusika na Downs na ati ndiyo mwenyewe hasa. Wapo wanaosema niko kimya au nashindwa kuchukua hatua, kwa sababu marafiki zangu wamehusika. Nawalinda. Kwa sababu hiyo, nikaona nami nisema angalau watu wanisikie lakini sina la ziada ni yale yale yaliyokwishasemwa.
Kwanza niseme wazi kwamba ule msemo wa wahenga wa akutukanae hakuchagulii tusi hapa umetimia. Napenda kuwahakikishia wana-CCM na wananchi wenzangu kuwa sina uhusiano wowote wa kimaslahi kwa namna yoyote ile na kampuni ya Dowans. Sina hisa zozote wala manufaa yoyote yale. Pia sina ajizi wala kigugumizi cha kuchukua hatua kwa sababu ya rafiki yangu au hata kama angekuwa ndugu yangu kahusika. Maamuzi yaliyofanywa na Kamati Kuu na Kamati ya Chama ya Wabunge wa CCM yalifanywa chini ya uogozi wangu. Ni uthibitisho tosha wa ukweli huo. Waliokuwepo kwenye vikao hivyo wanajua ukweli wa haya ninayosema. Ningekuwa na maslahi au hofu tusingefanya uamuzi ule.
Wana-CCM Wenzangu na Wananchi Wenzangu;
Kama mtakavyokumbuka tulipoingia madarakani nchi ilikuwa na tatizo kubwa la ukame mkali sana ambao haujawahi kutokea. Mavuno ya chakula yalikuwa mabaya tukawa na njaa kali na watu 3,776,000 walilazimika kuhudumiwa na Serikali. Aidha, mito mikubwa na midogo ikapungukiwa sana maji na mingine kukauka kabisa. Matokeo yake ni mabwawa yetu yote ya kuzalisha umeme yakakosa maji hivyo uzalishaji wa umeme ukaathirika vibaya sana na nchi ilikuwa gizani.
Ili kukabiliana na tatizo hilo ushauri ulitolewa na TANESCO nasi tukaukubali kuwa wakodishe mitambo ya kuzalisha umeme kutoka nje. Serikali tukaombwa kugharamia ukodishaji huo. Taratibu za kisheria zikafanywa, tenda zikatangazwa na washindi wakapatikana Aggreco, Richmond na Alstom. Kampuni za Aggreco na Alstom zilileta mitambo yao kwa wakati lakini kampuni ya Richmond ikawa inasuasua. Wakati huo huo maneno mengi yakawa yanazagaa kuhusu Richmond kutostahili kupewa tenda kwa sababu ya kutokuwa na uwezo kwa kampuni hiyo na kampuni hiyo kutokuwa hai. Ikadaiwa kuwa wamepewa tenda kwa sababu ya kubebwa na baadhi ya viongozi Serikalini. Maneno hayo yalifanya Wizara ya Fedha wasite kutoa fedha za kuanzia kwa kampuni hiyo. Aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini wakati ule alipokuja kuniomba niingilie kati ili kampuni hiyo ilipwe malipo ya awali (down payment) nikataa na kumwambia Waziri aachane nao kwani kampuni hiyo ni ya mashaka. Hivyo kampuni ya Richmond haikulipwa down payment, wakashindwa kutimiza mkataba. Maneno yakazidi kadri makali ya kukosa umeme yalivyoendelea kuuma.
Baada ya hapo kampuni ya Richmond ikauza mkataba wake kwa kampuni ya Dowans ambayo ilileta mitambo na uzalishaji wa umeme ukafanyika na kupunguza kabisa makali ya mgao. Tuhuma kuhusu Richmond ziliendelea kulindima mpaka hatimaye Tume ya Bunge ikaundwa na kugundua kuwa Kampuni iliyouziwa haikuwa hai na ni ya mfukoni. Hatima ya Tume hiyo tunaijua sote. Aliyekuwa Waziri Mkuu na Mwawaziri wawili waliwajibika. Zile tuhuma za yeye kuwa ndiye mwenye kampuni hazikuthibitika lakini aliwajibika kwa sababu yeye ndiye aliyetoa kauli ya kukubali ipewe tenda ili kuepusha nchi isiwe gizani.
Miezi kadhaa baadaye, likazuka sakata la Dowans ifutiwe mkataba kwa hoja kuwa wamerithi mkataba na kampuni ambayo haikupata kihalali mkataba wake. Kamati ya Bunge ilisema hivyo na wanasheria wa TANESCO pia walishauri hivyo. TANESCO ikavunja mkataba. Dowans hawakuridhika, wakashitaki kwenye Baraza la Usuluhishi kama yalivyo masharti ya mkataba waliotiliana sahihi. Madai yamesikilizwa na TANESCO imeonekana ni mkosaji hivyo wakatozwa fidia ya Dola za Marekani 64 milioni.
Taarifa hiyo imetushtua wengi. Niliuliza na kupewa ushauri mbali mbali. Wapo waliosema lazima tulipe, wapo waliosema tusilipe, wapo waliosema tusiharakishe kulipa kwani kuna uwezekano wa kutokulipa kwa kutumia sheria. Uamuzi wangu ukawa tusiharakishe kulipa, tutafute njia za kuepuka katika kulipa. Ndiyo maana ya taarifa ya Mheshimiwa Chiligati na ile ya Waziri Mkuu.
Ni mzigo mkubwa mno kwa TANESCO kubeba, hivyo tufanye kila tuwezalo tuepuke kulipa. Tumewataka wanasheria wetu wasaidiane na wale wa TANESCO kuhakikisha hilo halitokei. Nataka kuwahakikishia kuwa na mie ni miongoni mwa wale wasiotaka TANESCO ilipe, hivyo kauli za kuhusika na Dowans inanishangaza maana nisingeamua hivyo katika Kamati Kuu na Kamati ya Wabunge wa CCM. Ama kweli akutukanae hakuchagulii tusi.
Hitimisho
Ndugu Viongozi, Wanachama, Wapenzi na Washabiki wa CCM na Ndugu Wananchi;
Nimesema mengi, nisingependa kuwachosha zaidi kwa hotuba ndefu. Nimalize kwa kuwasihi nyote, kila mmoja katika mazingira anayoishi kuendelea kukisemea, kukipigania na kukupigia debe Chama chetu. Tuhakikishe tunapata wanachama wengi zaidi, hususan vijana. Tuendelee kuwa na upendo, umoja, mshikamano ili tusimamie utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM ya mwaka 2010-2015 na ahadi tulizozitoa kwa wananchi. Naamini kila mmoja wetu akitimiza wajibu wake tutaendelea kuaminiwa na wananchi na kupewa heshima ya kuongoza nchi yetu hata katika chaguzi zijazo.
Asanteni kwa kunisikiliza!
Kidumu Chama cha Mapinduzi!
"