Adverts

Feb 7, 2011

Nani kama mama-11

Nani kama mama-11: "
Aligeuza kichwa kumwangalia yule mwanamama, kwa wakati huu alikuwa kashajifunika uso wake, na ilionyesha wazi kuwa kazirai, na baba mwenye nyumba , kumbukumbu zikawa zinamjia na kumpandisha hasira , akatamani amumalize huyo mama, humo ndani ili watu wakiingia wajue alikuwa keshakufa, lakini Huruma ikamuingia, na mapenzi ya asili, mapenzi yale yaliyomfanya akose raha, mapenzi ambayo, yalimtesa miaka mingi , yakamwingia, …ikawa hasira, Huruma, mapenzi, …lakini hasira zikazidi kipimo, akachukua chuma kilichokuwepo humo ndani, akidhamiria kufanya lile alilokuwa nalo siku nyingi, kisasi…akainuka, akainua juu kile chuma, na kukiangalia kichwa cha yule mama….! Je jamaa anataka kufanya nini, na ni nini kilimpata mpaka atake kufanya anachotaka kufanya, tuendelee na kisa chetu cha NAMI KAMA MAMA ************** *********** ******** **** ‘Naomba unielewe sana kuwa nafanya hili sio kwasababu sikupendi, ila imenibidi nifanye hivyo, kutokana na uamuzi wa wazazi wangu…sina zaidi ya kukueleza ila usihangaike kuja nyumbani kwani sasa hivi mimi ni mke wa mtu. Kwaheri ya kuonana! ***** Haya yalikuwa maneno mafupi katika kibarua kidogo alicholetewa baba mlezi ambaye ni baba wa kufikia wa mtoto aliyeletwa toka hospitalini! Alikumbuka siku ile vyema, siku mbayo akiikumbuka hukosa raha kabisa, anajiona kama aliachwa uchi mbele ya jamii na marafiki zake, Siku ile, alikuwa kajiandaa na suti nzuri ya kuazima, alishawapata habari marafiki zake na jamaa zake wa karibu, akitamba kuwa, yeye atamuoa Tausi kwa vyovyote iwavyo, na kuwa wazazi wake hawawezi kuwazuia kwani walishapendana toka utoto. Mashabiki walimwambia tena kuwa jamaa ambaye wamesikia anataka kumuoa huyo binti ni tajiri wa ngombe, na kijijini hapo anaogopwa kwa fujo, na asipoangalia anaweza akapata kipigo ambacho hatakisahau. Aliwaambia kuwa ndoa ni kati ya mke na mume wanaopendana, yeye na huyo binti wanpendana, hadhani kuwa binti huyu atamsaliti kwasababu ya utajiri wa huyo jamaa… Basi usiku mmoja wakaongea na kukubaliana ili wasije wakawahiwa wafanye jambo la haraka, wafunge ndoa ya bomani, halafu mengine yatafuta baadaye, wakaenda ofisi za serikali kuomba kuwa wanafunga ndoa ya kiserikali na walioulizwa kwanini wakasema kuwa kuna tajiri mmoja anataka kutumia nguvu, kuvunja penzi lao, na wazazi wao wanashindwa la kufanya, kwahiyo wanaona wafunge ndoa ya kiserikali kwani kutakuwa na sheria ya kuwalinda.Jamaa waliyemkuta akawaahidi kuwasaidia kwani alikuwa akimjua huyo jamaa anayeogopewa. Usiku kucha hakulala , akikumbuka mipangilio yake ambayo alishaipanga, ni wapi wataenda baada ya kufunga ndoa yao, na kazi gani ataifanya ili waweze kuishi. Kwahiyo hakuwa na wasiwasi wa maisha ya baadaye. Alikuwa na akiba ya kutosha kwani aliamua kuuza ngombe zake alizopewa katika familia yao. Aliamua kuziuza zote kwani hakutarajia kurudi nyumbani hapo karibuni, kwasababu aliwajua mzazi wa Tausi wanavyomuogopa huyo mtu. Wao walikuwa na hiari ya yeye kumuoa binti yao, lakini walimuogopa sana huyo jamaa…na jingine kubwa alivyodokezwa kuwa huyo jamaa ambaye anaogopwa hapo kijijini alisema Tausi ataolewa na yeye kwa vyovyote iwavyo, na anayeleta kipngamizi atapambana naye. Alikumbuka maisha yake na Tausi tangia awali,wakiwa shuleni, walikuwa wakipitiana kwenda shuleni, na hakuweza kuondoka kurudi nyumbani mpaka Tausi awe ametoka darasani kwao kwani hawakuwa wakisoma darasa moja, yeye alimtangulia Tausi kwa madarasa mawili. Alipomaliza shule, akawa akimsindikiza Tausi shule na muda wa kutoka ukifika anakwenda hadi hapo shuleni kuhakikisha ametoka salama na kuhakikisha kuwa kamfikisha nyumbani kwao salama. Hali hii ikajulikana kwa wazazi, na wazazi walijua kama watakua hivyohivyo, basi ndoa yao itakuwa ya kweli. Maisha yalivyo hayatabiriki, wazazi wa Tausi wakakumbwa na balaa la njaa, wakajikuta wakiuza mifugo na kuandamwa na madeni mengi. Wakawa wanakopa kwa jamaa mmoja mwenye ngombe wengi, na waliposhindwa kulipa wakapewa masharti kuwa, wamuoze binti yao kwa huyo jamaa, na jamaa akawa tayari kuongeza ngombe wa ziada. Na wazazi wakawa hawana jinsi, ila kumuoza binti yao kwa huyo jamaa. Tausi alipofahamishwa, aligoma kabisa, lakini alivyoelezwa hali halisi, ikabidi anywee, kwani wazazi ndio hao, wanadaiwa na usalama wao upo mashakani. Alipoenda kumueleza mwenzake hakumuelewa, na ndipo mpango wa ndoa ya harakaharaka ikapangwa, hili lilifanyika kwa siri sana ila kwa wapmbe wachache sana waliojua, na siku ilipofika binti hakuonekana. Jamaa alisubiri toka subuhi mpaka jioni na jioni ilipofika akaletewa hicho kibarua kifupi. Hakuamini yaliyoandika, kwani yalikuwa kama kisu kikali kilichopenyezwa kwenye moyo wake. Hakuamini kabisa maneno kwenye ile barua, akaamua kwenda kwa huyo binti, alipofika alikuta hayupo na akaambiwa kesha pelekwa kwa mumewe, kwani ilibidi wafunge ndoa kwanza ya harakaharaka, kwani wamesikia kuwa kuna mpango wa kumtorosha huyo binti, halafu sherehe itafuta baadaye!. Jamaa alilia mbele ya wazai wa familia ya binti, akalaani na kulaani kuwa wamemfanyia unyama ambao hataweza kuusahau maishani, Na akaapa kuwa siku akimuona binti yao atamfanyia kitu kibaya sana kwa kumsaliti. Jamaa alikaa wiki mbili akiwa hataki kula, akawa kama mgonjwa, na hali ilipomzidi jamaa zake wakaona watafute njia ya kumuhamisha eneo hilo. Na ndio akahamia meneo karibu na mjini. Akiwa katika mateso haya ndipo akakutana na mama mlezi wa mhusika wetu mkuu, na huyo mama mlezi naye alikutwa na kisanga kama chake, kuwa walipanga kuoana na jamaa yake, na siku ya ndoa jamaa hakuonekana kabisa. Binti huyo karibu ajiue, lakini kutoka na kushawishiwa na wazazi na jamaa wanaompenda akatulia, lakini akasema hataki kuolewa tena, na kweli alikaa karibu mwaka, kila anayekuja kumposa anamtolea nje na kwa bahati nzuri akakutana na jamaa yetu huyu aliyesalitiwa na Tausi Walipoelezana visa vyao wakajikuta wanapendana, na urafiki wao ukaanzia hapo, haikuchukua muda wakaoana . Kwa kweli walipendana sana, kwani binti alikuwa na tabia njema sana na bwana alikuwa mtu wa busara, mpole kwahiyo walishibana sana, lakini katika maisha yao wakakutana na tatizo la kukosa uzazi, na ndipo walipompata huyo mtoto wa kufikia. ****** Baba mwenye nyumba alipokikumbuka hiki kisa, alitamani ammalize Tausi kwa kila chuma alichokuwa kakishika mkononi, lakini alikumbuka kuwa Tausi hakuwa na kosa kubwa kiasi hicho, kwani wazazi wao walikuwa hawana nguvu ya kufanya lolote, lakini kilichomuuma ni kuwa kwanini Tausi asiweze kutoroka kama walivyoahidi, ina maana aliona mali ni bora kuliko yeye masikini, hasira zikamshika na alipokiinua kile chuma kufanya alilokusudia bahati mlango ambao ulikuwa umelegea kwa kuvunjwa ukadondoka na kumdondokea mgongoni, akajikuta akidondoka na huo mlango. Na pale alipodondoka ni pale pale alipolala Tausi, akainuka haraka na kulaani, kuwa kagusa kitu asichotaka kukigusa tena, akataka kugeuka kuondoka, lakini sauti ya mguno wa Tausi ulimshitua kageuka kumwangalia. ‘Vipi baba mwenye nyumba tuje kukusaidia..’ sauti ikaita toka nje na kumshitua kuwa wapo watu nje wanamsubiria yeye. ‘Ingieni mumchukue bado yupo hai…’ akajikuta akisema, na watu wakaingia na haikuchukua muda huyo mama akawahishwa hospitalini. Kwa hali aliyokuwa nayo huyo mama ailibidi apelekwe kwenye hospitali ya mkoa, na huko akapokewa na manesi namoja kw a moja akapelekwa kwenye chumba maalumu, kwani hali yake ilikuwa mbaya, kwa majeraha ya moto na majeraha ya mapanga. Kwa muda huo alikuwa keshazindukana, ila alikuwa akigugumia kwa maumivu na damu ilikuwa inamvuja. ‘Huyu mama anahali mbaya sana, kwani wamemkatakata na mapanga, halafu kaungua sehemu kubwa ya mwili..uzuri ni kuwa damu haikupungua sana, kwahiyo haina haja ya kumuongezea damu, ila anahitaji matibabu ya haraka’ akasema dakitari. ‘Halafu huyu mama hasemi na wala hakumbuki kitu gani kimemtokea, ina maana ana matatizo mengine, ambayo yanahitaji utaalamu zaidi, ama ya akili au ana tatizo kusahau…’ akasema dakitari. Siku ya pili yake wakaja ndugu waliokuwa wakiishi naye, yaani mama mlezi wa mtoto na jirani yao, baba hakufika, wakapitia wodini kumtafuta mgonjwa lakini hawakumuona, ikabidi waulizie, na wakaona jambo jema ni kumtafuta mdogo wake,ambaye ni nesi katika hospitali hiyo. Walimkuta akiwa katika hekaheka za kuwahudumia wagonjwa wa chumba maalumu, na alipowaona jamaa zake akapata mwanya wa kumpumzika kidogo. ‘Vipi kuna tatizo jamani, mbona sina tarifa…’ akauliza ‘Ndio yupo mama mmoja tulikuwa tukiishi naye, unakumbuka nilikuambia kuwa yule mafanyakazi wa nyumbani alishindwa kazi na mwisho tuakaona tumpe kazi mama mmoja ambaye watu walikuwa wakimuita mama wa mitaani, tuligundua kuwa hana tatizo kama watu wanavyofikiria, na aliweza kuishi vyema kabisa na mtoto wetu, na mtoto mwenyewe anampenda kama mama yake vile…’ ‘Sasa ikawaje…maana simnaona nipo juu, kwa juu…’ akauliza nesi ‘Basi siku mbili zilizopita, wakaja wahuni, nawaita wahuni kwasababu eti wanadai huyu mama ni mwanga, wakampiga na kuchoma nyumba moto, ili wamteketeze, bahati nzuri tukawahi na kuuzima huo moto…’ ‘Mungu wangu , ina maana nyumba yetu imeteketea…, na mtoto alikuwa wapi…? Akauliza nesi ‘Kiliungua sehemu ndogo ya chumba cha uani, alichokuwa akilala huyu mama, na…mtoto hana matatizo, ninalala na yeye mama yake, atalalaje na mtu baki…, ndio tukamuokoa akiwa katika hali mbaya, ameletwa yupo hapa..hujamuona mama aliyeungua sana…?’ akauliza dada mtu! ‘Kwakweli wagonjwa kama hawo siku hizi ni wengi, wa majeraha, kuungua…na unachojali ni kusaidia , sio kumtizamam huyu ni nani, kama ningekuwa namjua kwa sura, ingekuwa rahisi kumgundua, mnakumbuka kila nikija huko nyumbani namkuta hayupo pale nyumbani, mara kaenda sokoni, mara kaenda kuteka maji…kwahiyo, labda nimemhudumia, lakini sikumbuki kumhudumia mama wa namna hiyo jana, ….sikumbki kabisa…ngoja nitaulizia, mnasema anaitwa nani vile?’ ‘Jina lake?...hutaamini hakuma mtu anayejua jina lake, ukumbuke yeye ukimuuliza anaitwa nani hajijui sana, hajui kabisa wapi alipotokea, na nini kilimkuta huko nyumba, sisi tunamuita mama wa mitaani, wengine mama mwenye mkono wa Baraka na sasa wanamuita mama mwanga…’ akasema dada mtu ‘Jamani achene imani hizo, atakuwaje mama mwanga…haya ngoja nikaulizie halafu nitawajulisha nini kinaendelea..’. Huyo nesi akaondoka kwa muda na baada ya nusu saa akarudi, na kuwajulisha kuwa huyo mgonjwa anahamishwa kwenda wodini, lakini kwa hivi sasa hatakiwi kusumbuliwa na ile hali mbaya imeshaondolewa kilichobakia ni matibabu ya kawaida, waje siku nyingine kumwangalia na kama kuna lolote jipya atawajulisha. Basi mama na mwenzake wanaondoka, lakini kabla hawajafika mbali nesi akawauliza mbona shemeji yeye hakufika? ‘Shemeji yako baada ya hilo tukio, kabadilika ghfla, na wala hataki kusema ni kwanini….na hataki kabisa kusikia habari za huyu mama, na amesema hangependa akipona arudi tena kwake, sijui ni kwasababu ya hilo tukio kuwa linaweza likaleta balaa jingine, kuwa hawa watu wanaweza wakaunguza nyumba nzima…lakini nadhani kuna kitu kingine ambacho hataki kutuambia kwa sasa. Unamjua shemeji yako, hapendi kuongea kitu kwa kubahatisha, anaweza akajua jambo hawaambii, eti mpaka apate uthibitisho…ngoja tusubiri hadi hapo atakapotaka kutuambia, lakini nina uhakika kuna jambo ambalo linamkera na huenda linahusiana na huyu mama…ngoja tusubiri, kwaheri nenda wasije wakakufukuza kaza..’ wakaagana na kuondoka. Matibabu ya yule mama ya kawaida yaliendelea, na akaanza kuinuka na siku hiyo alipoweza kuinuka, alikuwa kazungukwa na madakitari, wakikabdidhiana, yeye aliinuka kama kawaida na alipotizama ile hali ya watu kumzunguka, alitulia kwa muda na mara akakurupuka, na kuanza kukimbia, ikawa mshike mshike, na madakitari kwa utaalmu wao wakamuweka sawa, nafikiri ni kutokana na huko kupigwa, kwahiyo bado alikuwa akihisi watu hawo wapo karibu! Lakini baadaye hiyo hali ilitulia.na wakamhamishia kwenye wodi ya wagonjwa wa kawaida, Siku ya pili yake akawa na nafuu, na akaweza kuinuka na kwenda kujisaidia mwenyewe, ila akiwa katika uangalizi wa karibukaribu. Na siku hiyo mdogo wa dada mtu akawa yupo zamu, na alipofika kwa huyu mama akaanza kumuulizia hali yake. Yule mama alikuwa akijibu kimkatomkato, hakuwa anaongea sana, na maswali mengine akiulizwa alikuwa akishangaa, hata jina alikuwa hajui kuwa yeye ni nani… ‘Naomba uondoe hicho kitambaa ulichojifunika usoni, kwani napo kwenye uso kuna majeraha, na yasiposafishwa utapata shida…’ akamuomba yule mama ajifunue. Madakitari wa mwanzo walikuwa wakimsafisha na kukirudia kile kitambaa cheusi kama kilivyo, wakiamini kuwa huenda ni imani ya huyo mgonjwa hataki kuacha kichwa na uso wake wazi. Yule mama alipoambiwa kuwa akiondoke kile kitambaa, akaangaliwa huku na kule, alisita kujifunua lakini baadaye akakionda taratibu kama vile anaogopa kujitonesha. Yule nesi alimwangalia yale majeraha, na wakati anafanya hivyo, akili yake ikamkumbusha kitu, …akashikwa na butwaa, na kumwangalia yule mama vyema usoni..huku anamsafisha huku anamwangalia usoni, hadi yule mama akatizama pembeni. Alipomaliza kufanya hiyo kazi, akasogea pembeni akamtizam vyema yule mama, huku kumbukumbu zikimjia kwa mbali, na baadaye akakimbilia kwa dakitari mmoja, dakitari huyu ni wa siku nyingi hapo, madakiari wengine waliopo ni wageni. Akiwa njiani kuelekea ofisi ya huyo dakitari akakumbuka vyema jinsi ilivyokuwa siku ile, … ******* Je alikumbuka nini na huyu mama ndio nani, na ana siri gani …`Nani kama mama’ inakujulisha kuwa kisa hiki ni mchanganyiko wa matukio mengi, ni mateso na shida zilizomkumba mama mhusika wa kisa hiki na ni kieleelzo cha madhila ya akina mama wengi katika nchi hizi za Afrika. Wapo akina mama wamekumbwa na mabalaa kama haya lakini kutokana na huduma na mtizamo wajamii, wameachwa na wengine hata kupoteza maisha. Wapo akina mama au hata akina baba wanapita mitaani, na wote tuna-amini kuwa ni watu wenye upungufuu wa akili(vichaa), lakini huenda kuna tatizo dogoo ambalo kama lingeshughulikiwa mapema huenda wangeliweza kuwa katika hali yao ya kawaida,… swali ni nani wa kuwafuatilia watu kama hawo, kama ndugu zao wa karibu wamewatelekeza…? Naomba tuwe watulivu na kisa hiki na tukisome kwa makini, ukikifuatilia kwa makini utagundua nini tunachotaka kukifichua…KARIBUNI SANA Ni mimi: emu-three
http://miram3.blogspot.com/feeds/posts/default?alt=rss

"