Adverts

Feb 7, 2011

Serikali kuwaondoa Watanzania wote Misri

Serikali kuwaondoa Watanzania wote Misri: "
Serikali kuwaondoa Watanzania wote Misri Sunday, 06 February 2011 21:51 Israel Mgussi, Dodoma KUTOKANA na hali tete inayoendelea nchini Misri, Tanzania imelazimika kuufunga ubalozi wake nchini humo na kuwarejesha maofisa wote wa ubalozi kwa kutumia ndege maalumu ya kukodi. Kwa mujibu wa Waziri wa Mambo ya Nje na ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, Tanzania pia imewatambua na kuwakusanya Watanzania wengine 80 wengi wao ni wanafunzi ili kuwarejesha nchini hadi hapo hali ya usalama nchini Misri itaporejea. “Hali ya Misri kiusalama ni mbaya, kutokana na hali hiyo tumelazimika kufunga ubalozi wetu nchini Misri ndani ya saa 24 na imepelekwa ndege ya kukodi ili kurudisha maofisa wetu wa ubalozi pamoja na familia zao,”alisema Membe na kuweka wazi kuwa kwa sasa Misri hapatamaniki. Membe ambaye alikuwa akizungumza na wanafunzi wa wanachama wa CCM tawi la Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) katika mkutano mfupi uliofanyika juzi katika ukumbi wa Kilimani mjini Dodoma alisema kuwa hadi sasa hakuna Mtanzania yeyote aliyeripotiwa kujeruhiwa na hata kupoteza maisha kutokana na maandamano yanayoendelea nchini Misri. Alisema ingawa hakuna taarifa mbaya kuhusiana na raia wa Tanzania ikiwemo maofisa wake wa ubalozi, Serikali imeamua kufunga ofisi zake za ubalozi na kufanya jitihada za kuwarejesha Watanzania wote waliopo nchini humo ili kuwaepusha na madhara ambayo yangeweza kuwakumba kama wangeendelea kubaki. “Hakuna taarifa za maafa kuhusiana na Watanzania wanaoishi nchini humo,hata hivyo kutokana na ukweli kwamba hali ya Misri kwa sasa sio shwari, hatungeweza kusubiri madhara dhidi ya raia wenzetu wa Tanzania waliopo humo hivyo tumefunga ubalozi, tumekodi ndege kwa ajili ya kuwarudisha maofisa wetu wa ubalozi Misri na mpango wa kuwarudisha wanafunzi Watanzania 80 wanaosoma Misri umekamilika hivyo hadi kesho(leo) wote watakuwa wamerejeshwa nyumbani,”alisema Membe. Alisema hatua ya kuwarejesha raia wake ilichukuliwa juzi, lakini nchi zingine ikiwemo Kenya na Rwanda zilishawarudisha raia wao ikiwemo kufunga ofisi zao za ubalozi. “Hatua hizi Tanzania imechua leo (juzi) lakini wenzetu Kenya na Rwanda walishawarudisha raia wao tayari hivyo hata sisi hatungeweza kusubiri madhara zaidi, lakini jambo jema ni kwamba hadi sasa hakuna taarifa ya Mtanzania ambaye amepoteza maisha wala kujeruhiwa,"alisema Membe. Alisema Maafisa wa ubalozi wanaorudishwa nchini wapo 21 pamoja na familia zao na kwamba zoezi la kukodi ndege lilishakamilika hivyo Watanzania wawe na uhakika na usalama wa Watanzania wenzao kuwa watarudi salama.
"