Adverts

Feb 2, 2011

SULUHU NA AMANI : ANA KWA ANA NA HARITH GHASSANY

Mahojiano na mtaalamu, mtafiti na mwandishi wa Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia

Dk. Harith Ghassany ni mwandishi wa kitabu kinachoongelewa Tanzania nzima sasa hivi na huenda kikavuka mipaka na kuingia nchi nane zinazopakana na Jamhuri ya Muungano. Kitabu hiki chenye kurasa 500, kinazungumzia namna gani Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 yalipikwa Dar es Salaam, Algeria na mashamba ya mkonge ya Tanga na kupakuliwa Zanzibar.

Karibia vitabu 70 vimeshaandikwa na wataalamu toka ndani na nje ya Tanzania kutokea mwaka 1964 hadi leo; juu ya Mapinduzi ya Zanzibar; mbali ya maelfu ya makala na maandishi ya taasisi za kidunia.

Dk Harith Ghassany akipanda mnazi. Mwandishi huyu anaihusudu methali ya Kichina isemayo:

“Kama unapanga mwaka mmoja, panda mpunga; kama una mipango ya miaka kumi hadi mia moja panda miti; kama una mipango ya maisha waelemishe watu…”

Kwanini uliamua kuandika Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru?

Nataka ifahamike kuwa mimi binafsi nina damu ya Kiarabu na ya Kiafrika. Nia yangu kukiandika kitabu ni kuziondowa fitina za upotoshaji wa historia ili uhusiano mkongwe baina ya Wazanzibari waliochanganya damu, baina ya Wazanzibari na Watanganyika (Watanzania), na baina ya Waafrika na Waarabu, upate kuendelea kutitirika na kuimarika kwa maslahi ya kujenga amani na neema kwa faida ya walio wengi na vizazi vya baadae vya pande zote. Leo hii Mzanzibari amefika kuweza kumuambia Mzanzibari mwenzake: “Leo nitakuambia nini Nabii Yussuf aliwaambia nduguze: “Leo hakutokuwa na atakayefedheka.” Tusisahau kuwa Nabii Yussuf hakuyasema maneno hayo pale alipotupwa na nduguze ndani ya kisima. Na wala Zanzibar haitoweza kuiambia Tanganyika maneno ambayo Nabii Yussuf aliwaambia ndugu zake wakati sauti yenye kuyarejelea maneno ya hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere ingali ikisikilizana: “Ningekuwa na uwezo, ningevikokota visiwa va Zanzibar nikavitupilia mbali katikati ya Bahari ya Hindi.”

Au Waarabu/Waislam kuendelea kusakamwa kuwa wao pekee walihusika na biashara ovu ya binaadamu wenzao Afrika Mashariki na Kati. Nabii Yussuf aliweza kuwasamehe nduguze baada ya kuwa na nguvu na hadhi kubwa ambazo zingemuezesha kuwaadhibu nduguze waliomdhulumu. Kusamehe kwenye udhaifu ni kuakhirisha uadilifu. Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru hakikuja kupigana au kuwapigania wenye kutaka kuviendeleza vita vya jana na vya juzi, bali kimekuja kuleta suluhu na amani katika Zanzibar na Tanzania.

Akiwa Maktaba Kuu ya Tanga, kwenye shule ya sekondari ya Popatlal alikosoma zamani. ”Sikujua kama ningekuja siku moja kulifumbua fumbo la mapinduzi ya Zanzibar,” anasema. Picha imepigwa na Mtafiti Msaidizi ambaye pia ni mwanahistoria na mwandishi, Mohammed Said.

Wasomaji gani uliowalenga?

Walengwa wakubwa ni vijana wa rika jipya ambao bado hawajaathirika na kuathiriwa na mazoea na wana vipaji vya kuuhakiki ukweli bila ya kushawishiwa. Mara nyengine mtu huona ni bora kwake kuendelea kuukataa ukweli kwa kuamini kuwa akifanya hivyo atajinusuru na kupata wazimu.

Mhojiwa wetu (katikati) akiwa Zanzibar “kwa Mchina” alipowasili mwaka huu na nakala za mwanzo za kitabu chake. Hapa yuko na vijana ambao anaamini ni kizazi muhimu kitakachostawisha maisha ya leo na kesho…. Khalid Gwiji (kushoto) na Mohamed Ghassany. Picha imepigwa na Rashid Omar

Unadhani kuna hisia gani kuhusu Waarabu waliosakamwa na mapinduzi ya 1964?

Ni vyema tukajikumbusha kuwa maudhui ya kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru si biashara ovu ya utumwa wa binaadamu. Maudhui ya kitabu ni ushahidi na tafsiri mpya kabisa ya tukio la Mapinduzi ya Zanzibar ya 1964 na athari zake. Sasa utakuta kuna watu wanaohisi kuwa kitabu kimekuja kuwakosha Waarabu ambao wameowana, wameishi na kuzaa na makabila ya Kiafrika, ya Kibantu na yasio ya Kibantu. Hoja ya kitabu haisemi kuwa Waarabu hawakufanya utumwa. Hoja inauliza: kwanini watupiwe matope Waarabu peke yao wakati Wazungu, Wahindi na Waafrika, wote waliohusika na biashara ovu ya utumwa? Kwa nini ikafika hadi hata kutunga uwongo na kuufanya uwe ni kivutio cha kuwalipisha watalii wenye kuizuru Zanzibar shilingi elfu 3 tu na kutojali athari kubwa za fitina na chuki ambazo zimesababisha kuulisha maelfu ya watu Zanzibar?

Mwandishi kasimama mbele ya bao la kuingilia kambi ya mkonge ya shamba la Sakura palipokuwa na mkusanyiko wa wafanyakazi waliokwenda kuipindua Zanzibar – Picha imepigwa na Mohammed Said

Kuna ajenda gani ya kuilenga na kuifitinisha jamii fulani na kuziwacha jamii nyenginezo ambazo zimehusika na biashara ovu ya utumwa? Na si hivyo tu. Sasa tunajuwa kuwa zile zenye kuitwa “slave chambers” za pale Kanisa la Kwa Kimoto Unguja, zilikuwa ni ghala za kuwekea madawa katika jengo ambalo “lilijengwa na mamishionari wenyewe kama ni hospitali, miaka ishirini baada ya soko la watumwa kufungwa.” [i] Kitabu cha Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru kinaizungumzia “propaganda ya utumwa” si kwamba utumwa haukutokea bali “propaganda” ni ile dhana ya kuwavika Waarabu jukumu lote la biashara ya utumwa kana kwamba wao pekee ndio waloihusika au walionufaika. Na utumwa huo huo wa Waarabu ndio wenye kutumika kuyahalalisha Mapinduzi ya Zanzibar wakati Mapinduzi hayo hayakuwashirikisha Wazanzibari walio wengi wenye mizizi mirefu Zanzibar.

Dk Ghassany (“Mzenji na Mashua”) ; akiwa baharini mwaka 2003, Zanzibar. Picha na Ahmed Rashid

Hadi sasa umepata maoni gani kuhusu kitabu?

Maoni ya wasomaji wengi yamejikita katika simulizi za wazee wa mapinduzi na hawajazizingatia rejea za kumbukumbu mwishoni (“endnotes”) zifikazo 400 zenye kurasa 54 na picha 83. Maoni yanatafautiana mara nyingine baina ya mtizamo wa wasomaji na lengo la kitabu. Lengo la kitabu si kuvuana nguo kwa sababu ukikiangalia kwa mtizamo huo utakosa kuiona sura (“vision”) yenye kuitawala kitabu na itakuwa tumesota kule kule kwenye kupigana vita vya jana na vya juzi ambavyo ni vya watu na vya wakati ambao si wa vijana wa rika la hivi sasa.

Chumba chenye meza, vitabu na tarakilishi aliyotumia kuandikia kitabu nyumbani kwake mjini Washington DC. Picha hii aliyoipiga mwenyewe inaonyesha kupitia dirishani kasheshe la majira makali ya barafu (“blizzard”) mwanzoni mwa mwaka 2010.

Kama mwandishi, tuzungumzie fani uliyotumia kutathmini historia kupitia midomo ya wazee waliohusika na matukio ya 1964?

Wako wenye kusema kuwa mfumo wa kitabu wa kuyatumia maneno ya wazee si mzuri na badala yake mwandishi angeliyatumia maneno yao na kukiandika kitabu kwa maneno yake mwenyewe. Wako wenye kusema kuwa kitabu hivovivo kilivo kitakuja kutusaidia sana huko mbele tunakokwenda. Nilibahatika kuwasiliana pembeni na kufanya mahojiano kati ya viongozi wakuu wa Serikali na Mapinduzi ya 1964 na wametoa “maoni” yao jinsi utafiti wangu ulivyojikita na kamilifu ijapokuwa vipo vitu vichache ambavyo sikuviingia “ndani” zaidi ila faida kubwa na nzito zaidi ingelipatikana…labda katika uhakiki wa siku za mbele tutajaribu kujaza vijipengo na vijipengele muhimu.

Je, ipo tafsiri ya kitabu kwa lugha nyingine za kimataifa?

Tafsiri ya kitabu kutoka Kiswahili kwenda Kiingereza inakwenda kwa kasi kubwa. Kitabu pia kitatafsiriwa kwa Kiarabu.

Vipi uliweza kufikia maelezo na mtazamo mpya wa Mapinduzi ya Zanzibar ambao ulikuwa umekosekana kwa takriban nusu karne?

Kuna njia mbili za kulijibu suala lako Freddy.

Njia ya kwanza ni ya kujikweza na kujipigia debe kwa kusema kuwa uhodari wangu ndio ulioniwezesha kuzifikia nyaraka za kimataifa na wazee ambao hawajawahi kufanyiwa majadiliano kabla ya mimi. Njia ya pili pia ina hatari ya kuonekana kuwa najikweza lakini ndiyo yenye ukweli zaidi kuliko njia ya kwanza. Mwenyezi Mungu ametaka mimi niifanye kazi hii kwa sababu ambazo yeye atakuwa anazielewa zaidi. Na zaidi ya hiyo ni kwa sababu kama Mungu ana mikono mia basi tisiini na tisa iko juu ya Zanzibar na Tanzania. Hii namaanisha kuwa kuna Wazanzibari na Watanganyika (Watanzania) ambao wamekuwa wakimuomba Mungu kwa miaka mingi awaonyeshe njia itakayowatoa katika hali ya migogoro na kutofahamiana ya muda mrefu sana.

Mwandishi akiwa na Mzee Mkulima Manuwari, Zanzibar…Picha imepigwa na Ahmed Rashid.

Tukija katika suala la utafiti utakuta kuwa wingi wa maelezo juu ya jambo au tukio fulani kunaweza kusisaidie kulifahamu hilo tukio iwapo patakosekana uwezo wa kuyafanyia hayo maelezo uchambuzi yakinifu. Kukusanya data fulani bila ya kuwa na japo kibatari cha kuzimurikia ni sawa na kukusanya ilimu na kukosa mwangaza wa hikima yake. Wazee wa Dar es Salaam na Tanga ambao nilijuulishwa na marafiki zangu Dkt. Ramadhani K. Dau na Bwana Mohamed Said ndio walionipa ishara za mwanzo ambazo nilipozichanganya na ishara na mafumbo ya ndani ya vitabu na nyaraka za kitaifa, zilinifanya nizinduke ghafla. Lakini suala kubwa lilikuwa: kweli yanaitwa Mapinduzi ya Zanzibar lakini je, yalipangwa Tanganyika au Zanzibar? Wapi yalifanyika mapinduzi hayo haikuwa muhimu kwangu kama wapi yalipangwa, yalifanywa na nani, na uongozi ulikwenda kwa nani. Ilinibidi nijishauri haraka kuwa Mapinduzi ya Zanzibar yana njia zake za kuniwezesha kuyafahamu na njia hiyo haiko katika vichochoro vya Mji Mkongwe wa Zanzibar.

Ulichapa nakala ngapi na kuuza kiasi gani hadi leo mwezi Desemba?

Kitabu kimechapishwa katika mifumo miwili; wa zamani na wa kisasa. Katika mfumo wa kizamani zilichapishwa nakala 2,000 na vimeshauzwa vitabu 1,000 na zaidi kidogo katika miezi mitatu iliopita. Mfumo mpya ni ule wenye kutumiwa na shirika jipya la uchapishaji wa kileo la Lulu.com ambao ni print-on-demand (POD). Kitabu au vitabu huchapishwa ndani ya juma moja tu baada ya kuagiziwa na mnunuzi kwa njia ya mtandao. Hapo unaweza kuchapisha nakala uzitakazo kutokana na maagizo ya wanunuzi. Mwandishi huwa anapelekewa taarifa za vitabu vilivyouzwa kwa njia ya POD wiki 8 au zaidi kuanzia siku aliokabidhi mafaili ya uchapishaji na kukiweka kitabu kunako mtandao wa kampuni ya Lulu.com kwa ajili ya uchapishaji na uuzaji.

Harith ni mpenzi wa muziki wa mpiga gitaa maarufu toka Mexico, Carlos Santana. Moja ya nyimbo zake maarufu “Oye Como Va” (uliotungwa na Mcuba, Tito Puente) ulipendwa sana Tanzania ulipotoka miaka ya Sabini. Harith anaelezea faraja ya maudhui ya maneno ya hekima na furaha ambayo muziki wake Santana umempa yeye kama Mzanzibari aliyelazimika kusafiri nchi mbalimbali za dunia. Hapa kavaa kofia ya Ki-Mexicana inayofuatana na kadhia hii. Picha na Fatma Ghassany.

Kwa hiyo sasa hivi siwezi kusema vitabu vingapi vimenunuliwa kupitia mfumo huo wa kisasa. Wanunuzi wa kitabu wanaonunua kutoka mtandao wa Amazon.com huwa wanakinunua kupitia mfumo wa POD. Kitabu pia kinapatikana bure katika tovuti la http://www.kwaherikwaheri.com/ Vile vile wasiliana na mwandishi : info@kwaherikwaheri.com

Tafadhali waeleze wasomaji vitabu vinapatikana wapi…

Kwa upande wa Tanganyika (Tanzania Bara) kitabu kinauzwa katika sehemu zifuatazo:

Jiji la Dar es Salaam:

Emalaseko Super Market Dar es Salaam (Pamba House) kupitia Bwana Kafiti 0755095086;Tanzania Publishing House (TPH) Samora Avenue Dar es Salaam, ongea na Bi. Winnie 0715684504; Ibn Hazim Bookshop, misikiti wa Mtoro, Dar es Salaam, kupitia bwana Kim- 0773777707/0754287537; Ibn Hazim Bookshop, msikiti wa Manyema, wasiliana na Bwana Abdulswamad- 0658864888.

Mikoani

Kase Bookshop, Arusha

Wasiliana na Bwana Francis B. Kagengere 0754376825

Chuo Kikuu cha Dodoma

Wasiliana na Khamis Mkanachi- 0784855444

Tanga

Mohamed Said, 0787 265766

Salim Mohamed

Barabara ya 12 Tanga (duka la stationary) mkabala na Kituo cha Petroli 0784502929

Kwa Zanzibar:

Masomo Bookshop – Zanzibar. Wasiliana na Nizar 0715 878 697 au

Mwandishi wa habari Salma Said 0777 477 101

Mtandaoni:

Kitabu pia kinauzwa Amazon.com, na Lulu.com

Harith akizungumza nyumbani kwake sikukuu ya Idi, mjini Washington DC. Picha na Fatma Ghassany

Wasomaji wamesema nini hadi sasa?

Baadhi ya dondoo za maoni ya wasomaji nilizoletewa:

1-”Ushahidi uliomo ndani [ya kitabu] unazifanya hoja zake ziwe na mashiko madhubuti na zisizoweza kukanushika. Na hata kama kutokana na chuki, baadhi ya wasomi na watafiti watajitia kutozikubali hoja hizo, basi bado hawatoweza kukwepa ukweli wa kukiri kwamba utafiti alioufanya mwandishi na mfumo alioutumia kuwasilisha matokeo ya utafiti huo umefikia kiwango cha juu kabisa cha usomi.”

Msomaji mwingine kaandika kwa Kiingereza:

2-“Just wish to let you know that I have had the chance to indulge in Kwaheri Ukoloni… I find that the more I read the more I realize how ignorant I have been about facts surrounding the “revolution”…however, amidst all the gripping info I feel like I want to both finish the book but also quit reading it at the same time because some of the horrific revelations are causing me sleepless nights.”

3-“Angalau sisi wenye historia tofauti kuhusu Zanzibar tutapata mawazo mapya. Tunayosoma katika mitaala yetu katika ngazi mbalimbali hayatuonyeshi mambo halisi kuhusu Zanzibar na historia yake kwa ujumla.”

4- “Kiukweli, nilichokiona kwanza kimenipa maswali mengi, tumepotoshwa sana na hizì historia tunazofundishwa na kuzisoma, halafu mtindo uliotumìa sio wakawaida, ufasaha wako wa lugha ni mkubwa sana, kitabu kimesheheni rejea nyingi sana!…Nna imani mchango wako utathaminiwa na taifa letu jipya la Zanzibar.”

5-“…kitabu chako hiki…kimetoa fora na mwangaza wake umeondoa giza kubwa lililokuwa limetugubika…Sasa umetuthibitishia zaidi kuwa uhuru wetu na masikilizano ya asili yako usoni kwetu.”

Mtafiti alipokwenda mjini Cairo mwaka 2006 …kukutana na Mohammed Faiq (kulia) aliyekuwa mshauri wa Rais wa zamani wa Misri hayati Gamal Abdel Nasser Hussein, kuhusu masuala ya Afrika. Nasser alifariki Septemba, 1970.

6-“Baadhi ya mambo uliyoyafichua hakuna aliyewahi kuyadhukuru, kwa mfano mchango wa ndugu Tupendane katika mapinduzi. Ninawakumbuka vizuri wakipita mjini — hivi ninavyoandika naona kama picha akilini mwangu ikinionyesha wakati mmoja walipokuwa wakipita nje ya Majestic Cinema, bega moja juu, moja chini na suruwali zao. Katu sikuwahi kusikia kwamba walikuwa ni nguvu ya kisiasa. Hivyo umepiga hatua kubwa katika jaribio lako la kulifumbua fumbo la mapinduzi. Njia uliyotumia ya kuwaacha wahusika watoe masimulizi yao bila ya kuingiliwa kati imefana na kukiacha Kiswahili walichokitumia wenyewe kumezidi kunifanya nistaladhi na masimulizi yao. Bila ya shaka kuna suala la makumbusho na masimulizi ya kihistoria. Unawezaje mtu kuhakikisha kwamba unayoyakumbuka ni sawa? Unawezaje kutegemea unayoyakumbuka wewe kuwa ni ya ukweli? Inawezekana watu wawili wakaona kitu kimoja au wakashuhudia tukio moja na baadae wakatoa maelezo tofauti kuhusu tukio lile lile moja. Hili limenidhihirikia wazi katika masimlizi ya kaka yetu Salim kuhusu mkutano nliokuwa nao pamoja naye na Hanga. Mengi aliyoyasimlia kuhusu mkutano wetu ni sahihi. Lakini kuna maelezo flani flani ambayo mimi nnayakumbuka vingine na nathubutu kusema kwamba makumbusho yangu ni sahih kabisa kwa vile nimekuwa nikiweka kumbukumbu na nimeandika mswada kuhusu mkutano ule. Tofauti hizo kati ya simulizi hizo mbili, ya Salim na yangu, hazibadili namna ambavyo Salim alimuelezea Hanga. Ninachotaka kusisitiza hapa…ni kwamba zipo hizo tofauti kati ya wenye kukumbuka. Tofauti nyingine ya makumbusho niliyoiona ni katika maelezo ya jinsi Babu alivyokimbizwa kutoka Unguja. Nijuavyo mimi hakuvalishwa buibui wala mke wa Marhemu Saleh Saadallah hajakuwako kwa Babu wakati wa yeye Babu kukimbizwa kama alivyohadithia Aboud Mmasai. Waliokuwapo hapo walikuwa Saadallah, Twala, Ashura aliyekuwa mkewe Babu, mtoto wao mdogo Saira ambaye siku ya Alkhamis alipondwa na gari na kufariki na Jumapili yake pakatokea mapinduzi.”

7-“Zaidi, kama msomaji wa kitabu chako ningependa kutoa feedback ya machache ambayo binafsi nilikuwa na matumaini ya kuyasoma ndani ya kurasa za Kwaheri…

Mbali na ushahidi wa uvamizi kutoka Tanganyika, nilitegemea sana kupata sababu za ndani (mbali za ushindani wa kisiasa baina ya ASP/ZNP/ZPPP/Umma) za kijamii ambazo zilipelekea kwa WaZanzibari wa makabila (race) tofauti kufikia kuchochewa kirahisi hadi kufikia kufanyika mabadiliko ya kisiasa ya umwagaji damu. Visingizio kama vile vya kung’oleana mimea na kukataliana kuteka maji visimani kwangu mimi bado haingii akilini kuwa ndizo sababu hasa za watu kuuwana kwa kulipizana kisasi. Je, ulikuwaje uhusiano wa kijamii baina ya Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu na Wazanzibari wenye asili ya Kiafrika? Kweli serikali ya Sultan na baadae serikali ya ufalme wa kikatiba uliwabagua Wazanzibari wenye asili ya Kiafrika katika elimu, huduma za kijamii, umiliki wa ardhi nk? Binafsi nina wasiwasi na hili kwa vile, kwa mfano, picha nyingi nilizowahi kuziona za shule za mjini wanafunzi wake wengi walikuwa Wazanzibari wenye asili ya Kiarabu na Kihindi. Majuzi niliona filamu ile ya ‘lost arab kingdom (or something like that) ambayo ilionyesha kukaribishwa kwa Princess Ann wakati wa reign ya Sayyid Khalifa na vikundi vya sanaa vilokuwepo kumlaki vilikuwa ni vya sanaa/muzeka wa asili ya Kiarabu vitupu!”

Dk Ghassany akisafisha barafu nje ya nyumba yake baada ya kipindi cha baridi kali ya mwaka huu wa 2010. Hii ni moja ya hali halisi za maisha yanayowakumba Wazanzibari ughaibuni. Picha na Fatma Ghassany.

8-“Katika mlango wa 20/21 kunako historia ya ‘Mapinduzi dhidi ya Aboud Jumbe, binafsi nahisi kuwa umechelea kuandika ukweli wote ambao ungejumuisha tuhuma za kuhusika Mhe. Maalim Seif katika kutumiliwa na marehemu Mwalimu Nyerere katika kumuondoa madarakani. Tena, sina ushahidi wowote kwa mimi binafsi kutoa hadharani walakin kutomhusisha kabisa Maalim Seif na ‘mapinduzi dhidi ya Jumbe’ huenda akaoenaka kwa wengi wanaoamini tuhuma hizo kama ni njia ya kulikimbia hilo kwa kukwepa lawama. Halikadhalika, tuhuma hizo zinalingana sana na zile za Mwalimu Nyerere kuhusika na mauwaji ya Rais Abeid Karume bila ya kuwepo na ushahidi kamili na haikuwa sababu ya kutoandikwa ndani ya Kwaheri. Ukiliangalia tukio la Jumbe, umuhimu wa kuwepo na ukweli usio na shaka kutaweza kutufunza sisi WaZanzibari kuhusu matatizo yanayotakana na sisi wenyewe na hasa viongozi wetu ambayo ndiyo yanayowapa urahisi wasiotutakia mema kuendelea kututawala kwa khadaa. Lengo la kujua ukweli huo si la kutaka kumjua mchawi nani kwa vile sote tunajua kuwa viongozi wetu wote (including Mzee Jumbe as confessed in the Partner-ship) wamechangia Zanzibar kufika katika hali tulinayonayo sasa ya kukosa uhuru wa kujiamulia wenyewe katika ujenzi wa taifa letu.”

9-“…hii ni mara ya kwanza kuyasikia moja kwa moja kutoka kwa wale ambao wanasema walikuwa ‘jikoni’, wakiandaa na kusaidia mapishi ya mapinduzi, ingawa kwa maoni yangu, tatizo ni vipi kuweka mezani sawa, baina ya ukweli na maelezo ya hadithi za watu ambao pengine wanapenda kujinata na kujitutumuwa tu kuwa wao ndio waliohusika…the challenge to a reader is how to balance the truth with effective narratives, particularly if narrated by those who want to glamorize and romanticize their roles at the expense of the truth. A typical problem with oral histories. Kwa jumla, kitabu hiki kitasaidia kwa ukubwa sana kufunguwa macho ya watu wengi hususan kizazi cha sasa ambacho kwa muda mrefu na kwa makusudi kimefungwa macho yao wasione au hata kusikia vipi mapinduzi yalivyotokea.”

Wazee wa Kimakonde, Mzee Joseph Bhalo (katikati) na Mzee JJ Mchingama wakiwa na mwandishi…habari zao zaidi zimo kitabuni.

10-“Kuna mapungufu katika maelezo kuhusu mchango wa Wamakonde katika Mapinduzi ya Zanzibar.”

11-“Kitabu ni kikubwa sana na inayachukuwa macho ya msomaji muda mrefu kuyafikia manyama na minofu anayoyatafuta. Badala ya kurasa 500 kitabu kingelipendeza kama kingelikuwa kidogo zaidi na chenye kurasa zisozidi 250. Kuna baadhi ya wazee wanapenda sana kusema wakati hakuna faida kubwa ambayo anaipata msomaji.”

12-“[Hichi ni]… kitabu ambacho huenda kikabadilisha fikra sio za Watanzania Wazanzibari na Watanzania wa Bara tu bali watu wote wapendao ukweli ulimwenguni kote. Mimi nakisoma kitabu hichi kwa sasa hivi na naona vigumu kukiacha kwa sababu mbili: Mosi: Nataka kujua ukweli wa mapinduzi ya Zanzibar kama mwanahistoria ambaye alikuwa nchini wakati mapinduzi haya yalipotokea. Pili: Nataka kukitumia kitabu hichi kuwafundishia wanafunzi wangu Kiswahili kwa sababu sijaona kitabu ambacho kimeandikwa kwa Kiswahili fasaha kama hichi…”

13-“Niseme nini? Hatimaye nimekitia mkononi kitabu cha ‘Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru!’. Ni khatari. Ukianza kukisoma hutataka kukiacha tena. Kina addiction ya ajabu. Fanyeni bidii muweze kukiagizishia na kukipata na mkisome. Kila sentensi unayoisoma ni elimu ya aina yake ya kumfanya Mzanzibari ajijue na ajitambue na atambue namna tulivyochezewa akili kwa zaidi ya miaka 50 sasa.”

14-“Ahsante kwa ujumbe wako, ambao umenifanya nitokwe na machozi. Sio kwasababu umenitonesha kidonda, laa hasha. Nimekua na chuki juu ya chama tawala CCM na viongozi wake na hata kuwachukia Watanganyika na baadhi ya wa Unguja waliolisaliti Taifa la Zanzibar. Baada ya kusoma kidogo tu ujumbe wako huu nimefunguka macho, imani na kuosheka moyo wangu, na kuyasahau yaliopita kama unavo tusisitiza. Bila ya kuendeleza chuki hizi za Utanganyika na U CCM, lilobakia ni kudumisha Umoja wetu na amani ambayo tokea mwanzo ndio jambo nililokua naliomba katika kila sala.”

Nje ya Umoja wa Mataifa, New York. Picha na Fatma Ghassany.

Nini maoni yako kuhusu mustakbal wa Zanzibar na Tanzania?

Suala zuri na gumu. Mustakbal wa Zanzibar na wa Tanganyika (Tanzania) utakuwa mzuri iwapo utajiri mkubwa wa kihistoria na wa kijiografia wa Zanzibar, ambayo kabla ya Muungano ikiitwa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar, na wa Tanzania Bara, ambayo kabla ya Muungano ikiitwa Jamhuri ya Tanganyika, yenye kupakana na nchi 8 muhimu, utatumika kujenga muungano na mashirikiano ya kiuchumi na bara la Afrika na la Asia. Jambo la kwanza ni Baraza adhimu la Wawakilishi la nchi ya Zanzibar kuipitia na kuifanyia marekebisho Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuyarejesha na kuyalinda maslahi ya Zanzibar na kuonyesha njia mpya ya Muungano wa Jamhuri ya Tanzania. Tatizo kubwa ambalo baadhi ya uongozi na viongozi wa kihafidhina wa Tanganyika/Tanzania Bara na wa Zanzibar, ni pale wanapojiona kuwa ni watetezi wakubwa wa Muungano wa Jamhuri ya Tanzania na kushindwa kuwapitikia, wacha kukubali, kuwa wao ndio wamekuwa tatizo kubwa katika kuikataa Zanzibar kuwa ni mshiriki sawa ndani ya Jamhuri ya Muungano.

Kwanini Zanzibar na Jamhuri ya Muungano yenye kupakana na nchi 8 isiweze kuzitumia rasilmali za historia, jiografia, mali asili na akili za Wazanzibari na za Watanganyika, na za Kiafrika na Kiarabu kujenga mustakbal mpya wa amani na kiuchumi Afrika Mashariki na Kati? Inawezekana iwapo kutakuwepo na uongozi na viongozi ambao ni tafauti na wanasiasa waliozoweleka ambao wamekuwa na hadhi na mapato makubwa katika jamii kuliko walimu, madaktari, viongozi wa dini, na wataalamu wengine.

Ukiangalia utaona kuwa jina la kitabu limeanza na Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! na limefuatiliwa na Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia. Mustakbal wa Zanzibar na wa Tanzania kwa ujumla uko katika kuukubali mchanganyiko wa kikabila wa Kiafrika na wa Kiarabu wa Zanzibar – Afrabia. Lengo la Afrabia si kuupamba “Uwarabu” na kutaka kuonesha kuwa maendeleo ya kweli Zanzibar na Tanzania hayawezi kupatikana pasi na mahusiano mazuri na Waarabu. Lengo la Afrabia ni kuuendeleza uhusiano mkongwe wa kihistoria na wa kijiografia ili kujenga mafanikio makubwa ya kiuchumi na Waarabu, Waturuki, Wairani, Wamalaysia, Waindonesia, Wahindi, Wachina, kwa sababu wote hao wamekuwa na mahusiano makubwa na ya muda mrefu na Zanzibar. Hali kama hiyo haitoweza kufikiwa iwapo historia ya Mapinduzi ya Zanzibar na historia ya utumwa wa Afrika Mashariki na Kati itaendelea kupotoshwa na kuwafarikisha Wazanzibari, Wazanzibari na Watanganyika (Watanzania), na Waarabu na Waafrika, pamoja na Waislam na Wakristo.

Dk Harith Ghassany akiwa na Rais Mstaafu wa Algeria, mheshimiwa Ben Bella (kushoto), ambaye ni mchangiaji mkuu wa ukombozi wa nchi za Kiafrika na mapinduzi ya Zanzibar. Picha na askari wake Mzee Ben Bella.

Tizama Brazil inavoekeza Afrika yenye kuzungumza Kireno. Tizama mradi mkubwa wa daraja litakaloyaunganisha mabara ya Afrika na Asia kupitia Yemen na Djbouti. Kwanini Muungano baina ya Zanzibar na Tanganyika ushindwe kupata kiongozi, viongozi, na uongozi wenye kutambua kuwa historia inaweza ikapewa msukumo mpya wenye kuangalia mbali na kuzipa maendeleo makubwa ya kiuchumi na kiilimu nchi zenye utajiri mkubwa wa mali asili na akili za Afrika Mashariki na Kati?

Ukweli ni Muungano wa Zanzibar na Tanganyika (Tanzania) chini ya uongozi wa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete una kila sababu za kurekebishika na kuiamarika iwapo nia ya Zanzibar na ya Tanganyika itakuwa ni kuzidai na kuzilinda haki za Kikatiba za washiriki walio sawa kwa lengo la kuujenga uchumi imara wenye kutegemea ilimu bora katika ngazi zote, ambao neema zake zitakuwa ni kivutio kwa nchi nyengine za Afrika Mashariki na Kati.

Mustakbal wa Zanzibar na wa Tanzania utategemea sana uzingatiaji na ufumbuzi wa matatizo matatu makubwa ambayo yamesimama juu ya maadili ya usawa, ukweli, na amani.

  1. 1. Usawa: Kuendelea kuitizama Zanzibar kwa macho ya Uafrika na Uwarabu badala ya mchanganyiko mkubwa wa Kiafrika na wa Kiarabu walio sawa ni kuendeleza mfumo wa kiakili ambao kwa kujua au kwa kutokujua utaendelea kuihujumu misingi ya Jamhuri ya Muungano wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar na Jamhuri ya Tanganyika – Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Wazanzibari wenyewe wameshaamua kuipiga fundo fitina ya muda mrefu ambayo imekuwa ikiwagawa kwa muda mrefu. Maridhiano yanarudisha usawa na suluhu inaleta amani.
  2. 2. Ukweli: Ufisadi ni matokeo ya matunda ya muda mrefu ambayo mbegu zake zilipandwa ndani ya ardhi ya siasa ya Ujamaa na Kujitegemea. Azimio la Arusha lilizingatia maadili mazuri ya miko ya uongozi lakini ubovu ulikuwepo kutokea mwanzo katika sera dhaifu za kilimo na viwanda va kileo ambazo zilisababisha kuanguka kwa uzalishaji na uchumi ambao ukitarajiwa kuziinua hali za wananchi masikini walio wengi. Kutofaulu kwa siasa ya Ujamaa kumekubalika kimtazamo lakini ukweli wa athari zake juu ya uongozi na waongozwa katika awamu tafauti haujazingatiwa ipasavyo.
  3. 3. Amani: Kero za Muungano zitabakia kuzungumzwa kama ni mmremeto wa maji jangwani wenye kutoa matumaini ya uwongo kwa mwenye kiu iwapo suala la chimbuko la Taifa la Tanzania litaendelea kutenganishwa na mapinduzi ya Zanzibar yaliopikwa Tanganyika na kupakuliwa Zanzibar.

Ufumbuzi wa matatizo yote matatu pia utategemea kujiepusha kufanya kosa ambalo lilofanywa na Urusi la kutaka kuubadilisha mfumo wa kisiasa kwanza kabla ya kuanzisha mfumo wa kiuchumi wa kileo. Uchina uliliona kosa la Urusi na mapema na ikaweza kujinusuru na matokeo yake imeweza kuwaletea mamilioni ya wananchi wake maendeleo makubwa ya kiuchumi ndani ya kipindi kifupi cha historia. Muhimu kuwepo na uongozi wenye kubebwa na maadili ya usawa, ukweli, na amani. Huo ndio ujumbe wa Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia. Kama nchi zisizo za Magharibi zimeweza, kwa mfano Japan, South Korea, Hong Kong, Taiwan, Singapore, Malaysia, Indonesia, Uchina, India, Uturuki, Iran, Brazil, Dubai, UAE, Qatar, Oman, nk, zimeweza kupiga hatua kubwa za maendeleo katika wakati mfupi, basi, Zanzibar na Tanzania zenye utajiri wa ndani na nje, pia zinaweza!

Mwandishi na wanae wakishughulika katika shamba la matunda ya “Blueberries” , Maryland, Marekani. Picha na Ghassan Ghassany

i] Jonathon Glassman “Racial violence, universal history and echoes of abolition in twentieth-century Zanzibar.” In Abolition and Imperialism in Britain, Africa, and the Atlantic, edited by Derek R. Peterson. Ohio University Press, 2010, uk. 178-179

Dk Harith Ghassany, Kijiji cha Kipumbwi, mwaka 2003. Picha na Mohammed Said

"