Adverts

Feb 2, 2011

Tanzania kusuluhisha mgogoro wa Ivory Coast

Tanzania kusuluhisha mgogoro wa Ivory Coast: "

Ivory Coast katika vita ya mafahali hawa wawili walioshinda uchaguzi kila mmoja kwa kutumia tume yake

TANZANIA imeteuliwa kuwa moja ya nchi tano zinaounda kamati ya Umoja wa Afrika ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kisiasa nchini Ivory Coast kati ya Rais Laurent Gbagbo na Alassane Ouattara.

Nchi zingine katika Kamati hiyo ni Chad, Mauritania, Nigeria na Afrika Kusini, ambazo zitaungana na Burkina Faso ambayo tayari inashughulikia mgogoro huo.

Kamati hiyo ilifanya mkutano wake wa kwanza juzi jijini Addis Ababa na kukubaliwa kuwa kila nchi iteue mwakilishi katika kamati ndogo ya wataalamu ifikapo kesho ambao watakwenda Ivory Coast kuangalia na kutathmini hali ilivyo.

Baada ya hapo Kamati ya wataalamu itatakiwa kutoa taarifa na ushauri kwa viongozi ambao hatimaye watakwenda nchini humo kukutana na viongozi hao wawili wanaogombea madaraka.

Wakati huo huo, Rais Kikwete alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Maendeleo na Ushirikiano wa Kimataifa wa Uingereza, Andrew Mitchell.

Katika mazungumzo yao Mitchell alimhakikishia Rais Kikwete kuwa Uingereza itaendelea kuisaidia Tanzania katika bajeti yake na sekta mbalimbali zikiwamo za elimu na afya.

Katika mazungumzo yao, viongozi hao kwa pamoja walikubaliana kufanya kazi itakayoonesha mafanikio na majibu yatakayoleta manufaa kwa watu wake.

Rais Kikwete alimweleza Mitchell dhamira yake ya kuongeza jitihada katika kukuza elimu nchini na kuongeza upatikanaji wa huduma ya afya kwa wananchi karibu na makazi yao.

Mitchell alisema Uingereza itamsaidia na kushirikiana naye katika kutimiza azma hiyo ambapo wataongeza msaada katika sekta hizo muhimu. Rais Kikwete alirejea nyumbani jana mchana.

CHANZO ::: Habari Leo

"