Adverts

Jan 19, 2012

JAJI AKATAA KUKIMBIZA MCHAKAMCHAKA KESI YA HAMAD

MAHAKAMA KUU Kanda ya Dar es Salaam imesema kwamba Bunge ni chombo makini haliwezi kuamua jambo wakati likijua jambo hilo liko mahakamani na halijatolewa maamuzi.
Jaji Agustino Shangwa alisema hayo katika kesi iliyofunguliwa na mbunge wa Wawi, Hamad Rashid dhidi ya wadhamini wa CUF akijaribu kuonyesha kwamba hakuna uharaka wowote katika kuendesha kesi hiyo bunge litasubiri maamuzi ya mahakama kwanza ndipo liendelee na hatua zake.
Kesi hiyo leo ilikuja mahakamani hapo kwaajili ya kusikilizwa maombi ya kina Hamad yaliyoiomba mahakama hiyo kuwataka kamati ya wadhamini ya CUF kujitetea kwanini wasitupwe jela kwa kukiuka maamuzi ya mahakama yaliyosimamisha kikao cha kamati kuu kilichowavua uanachama, ombi jingine ni kutaka mahakama itamke wao ni waanachama halali wa CUF.
Jaji Shangwa alitoa uamuzi Januari 4 mwaka huu Baraza Kuu la CUF lisitishe kuwafukuza uanachama Rashid na wenzake ikiwa ni pamoja na kuendelea kuwajadili wakati wa mkutano wake uliofanyika Zanzibar siku hiyo.
Uamuzi huo ulitoka kufuatia maombi ya Rashid na wenzake kuomba mahakama hiyo iamuru mkutano huo ambao ulikuwa na lengo la kuwafukuza uanachama usitishwe hadi kesi yao ya msingi itakaposikilizwa na kuamuliwa.
Wakili wa CUF, Twaha Taslima alidai kuwa, walipokea samasi ya maombi hayo Ijumaa ya tarehe 13 Januari mwaka huu mchana na kuanza kuifanyia kazi Januari 15, alidai ilibidi kutafuta mawakili jambo lililofanyika Juzi na jana hivyo wanaomba muda wa wiki mbili kujiandaa kwa majibu.
Wakili wa kina Hamad na wenzake 10, Augustino Kusalika akijibu hoja hiyo alidai kuwa hana pingamizi lakini anaomba isiwe muda mrefu kiasi hicho wapewe wiki mmoja inatosha ikizingatiwa maombi hayo yaliletwa chini ya hati ya dharula.
Jaji shangwa alisema, “Sio ugomvi wa kuamuliwa haraka haraka huu, huu ni ugomvi mkubwa ulivyoibuka sisi hatujui, sawa inahitaji haraka lakini si kiasi hicho cha kupata kiharusi!”
Alisema kama inavyoeleweka kazi ya mahakama ni kuamua migogoro ya watu anakubaliana na ombi la walalamikiwa waweze kuleta hati ya kiapo cha pingamizi ndani ya wiki mbili yaani Januari 27 na Januari 6 watajibu hoja walamikaji.
Alisema Februari 13 maombi yatasikilizwa hata hivyo alisema mahakama hiyo inapanga hadi kufikia Machi 13 maombi hayo yawe yamekamilika kutolewa maamuzi labda ibaki hatua ya mahakama ya Rufaa kama kutakuwa na watakaotaka kwenda huko.
Jaji huyo alisema hakuna haja ya umati kufurika mahakamani kama ilivyokua leo kwasababu haina haja, alisema hoja zitawasilishwa katika tarehe hizo kwa maandishi na ni mawakili tu ndio watakaoleta isipokuwa watakaotaka kuhudhuria iwe tarehe ya hukumu.
Baada ya kesi kumalizika mahakamani, Julias Ntatiro ambaye ni naibu katibu mkuu wa chama hicho alisema kuwa maamuzi ya mahakama yanaheshimiwa hivyo wanasubiri, hata hivyo chama chake hakina mpasuko ni imara yasisikilizwe maneno ambayo ni propaganda.
“Wachache walikosa maadili wakachukuliwa hatua kikatiba, katiba ya CUF itaendelea kufuatwa,” alisema Ntatiro.
Alisema Mahakama hata kama uamuzi itakaoutoa utakuwa kuwapokonya uanachama kina Hamad ilifanyika kimakosa, Hamad atabaki mbunge, atafanya majukumu ya ubunge lakini ndani ya chama mjadala umefungwa.
Wafuasi wa chama hicho waliokuwa mahakamani, halikuwa jambo la kufichika kuwa ni makundi mawili tofauti, moja likiwa kundi la Hamad ambalo lilikuwa likijigamba kuwa ikifikia Hamad anavuliwa uanachama na ubunge basi kadi zao wameshamkabidhi zinarudishwa CUF na wao kumfuata atakakokuwa.
“Nakwambia mwandishi tunachoma bendera hapa hapa mahakamani hapo nje na hatuna haja na CUF, CUF bila Hamad Rashid hakuna chama” alinukuliwa mwanachama mmoja aliyekuwa kajifunika bendera ya CUF.
Hoja zingine katika maombi hayo ni wadaiwa CUF iliwasilisha barua kwa Spika wa Bunge inayohusu kumvua uanachama Hamad maamuzi ya kikao chao ambacho ni batili kilichofanyika saa 9.05 alasiri januari 4 mwaka huu.
Aidha Januari 15 mwaka huu kamati ya uongozi wa Bunge itakutana Dar es Salaam kujadili Hamad kuhusiana na barua ya CUF ya kumvua uanachama hivyo hastahili kuwa mbunge na maamuzi ya kikao batili kilichofanywa hata baada ya kuzuiwa na koti.
Na kwamba wapigakura wa Wawi watakosa haki yao ya kuwakilishwa na mbunge wao huyo. Kwamba kilichofanywa na CUF ni mchezo mchafu.