Adverts

Jan 21, 2012

MADEREVA WA MALORI NA WAAJIRI WATAKA WAZIRI NUNDU NA NAIBU WAKE WAJIUZULU

Waziri wa uchukuzi Omary Nundu Naibu waziri za uchukuzi Dkt Athuman Mfutakamba
WAKATI sakata la migomo isiyokwisha kwa madereva wa malori ya mizigo nchini ikiendelea kuchukua sura mpya kila kukicha ,madereva hao wa malori ya mizigo na waajiri wamemgeukia waziri wa uchukuzi Omary Nundu na naibu wake Dkt Athuman Mfutakamba wadai wameshindwa kusimamia maagizo yao wenyewe na hivyo kuwataka wajiuzulu nafasi zao mara moja . Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tofauti madereva hao walisema kuwa sababu ya wao kuendelea kugoma mara kwa mara ni kutokana na ahadi za serikali iliyotolewa na wizara hiyo ya uchukuzi kushindwa kutekelezwa kwa wakati . Akizungumza kwa niaba ya wenzake Michael Sanga ambaye ni dereva wa lori linalofanya safari zake kati ya Malawi na Dar es Salaam alisema kuwa wakati wa mgomo wao wa kwanza ambao waziri wa uchukuzi alifika kuwasikiliza walikuwa na madai sita ambayo waliomba yatekelezwe ili wao kuweza kusitisha mgomo wao. Alisema kuwa kati ya madai hayo sita madai matano yalikuwa upande wa serikali na dai moja kwa waajiri wao ila wanashangazwa kuona serikali inaendelea kuchelewa kutekeleza ahadi zake katika madai hayo matano na kusimamia kwa nguvu zote utekelezaji wa dai moja la waajiri kutoa ajira kwa madeva hao. Sanga alisema kuwa mgomo huu wa mwaka huu ambao uliitishwa na madereva haukuwa ni mgomo wenye tija kwao kwani bado ulilenga suala hilo moja la madereva kuajiriwa na kufunika madai matano ya serikali na kuwa sehemu kubwa ya mgomo huo ulihamasishwa na baadhi ya viongozi wa serikali na madereva deiwaka (wasio na kazi) ambao wananyemelea kazi. Hivyo alisema kuwa ufike wakati watendaji wa serikali akiwemo waziri wa uchukuzi Omary Nundu na naibu wake Dkt Athuman Mfutakamba kuepuka kutoa ahadi ambazo kwao ni vigumu kutekelezwa na kuwa kufanya hivyo ni sawa na kuichafua serikali nzima chini ya Rais Jakaya Kikwete . "katika maazimio yetu tulianzimia mambo sita ambayo ni kuondoa usumbufu wa mizani kutoka mizani nane iliyopo hadi kufika mizani minne ama mitatu kutoka Dar es Salaam hadi Tunduma, Askari wa usalama barabara kupunguzwa kutoka vituo 20 vya sasa toka Dar es Salaam hadi Tunduma, vituo vya ukaguzi wa magari (Check Point ) kupungua zaidi ,Kucheleweshwa boda ya Tunduma kwa wiki 2-4 na TRA, kuchelewa kupakia mizigo bandarini kati ya siku 2-3 na waajiri kutoa ajira kwa madereva" Alisema kuwa hadi sasa mfano kwa upande wa askari wa usalama barabarani badala ya kupungua ndio wameongezeka katika mikoa yote kutoka Dar es Salaam hadi Tunduma . Aidha alisema wanawashukuru waajiri kwa upande wao wameanza kutoa ajira kwa madeva na sumatra imekuwa ikiwabana waajiri hao kwa nguvu zote huku serikali ikishindwa kutimiza hata ahadi yake moja kati ya madai matano yaliyoelekezwa kwa serikali. Kwa upande wake Ally Kalinga ambaye ni dereva wa Lori linalofanya safari zake kati ya Zambia na Dar es Salaam aliasema kuwa ili mawaziri hao na manaibu mawaziri waendelee kusimamia vema wizara zao ni vema waziri wa uchukuzi na naibu wake kujiuzulu kwa kushindwa kuiongoza wizara hiyo . Mmoja kati ya waajiri ambaye hakupenda kutajwa jina lake alisema kuwa madai ya madereva ni ya msingi na ndio sababu ya wao kama waajiri wameanza kutekeleza kwa nguvu zote dai lao kubwa la kutaka kupewa ajira na kuwa hadi sasa zaidi ya madereva 2700 kote nchini wamepatiwa ajira zao. Pia alisema serikali inao uwezo wa kutimiza madai ya madereva hao madai hayo matano haraka iwezekanavyo na kuwa iwapo waziri mwenye dhamana ya wizara hiyo na naibu wake wameonyesha kushindwa kusimamia ahadi zao wenyewe ni vema kutangaza kujiuzulu ili kumfanya Rais Kikwete asiendelee kuchafuliwa na utendaji mbovu wa baadhi ya mawaziri wake. Katika ahadi yake kwa madereva hao wakati wa mgomo wa kwanza uliofanyika mwaka jana mjini Tunduma mkoani Mbeya ,waziri Nundu aliwaahidi madereva hao kuwa madai yao yatafanyiwa kazi haraka zaidi na kuahidi baada ya miezi miwili mizani barabarani kupunguzwa na kubaki na mizani miwili pekee kutoka Dar es Salaam hadi Tunduma mkoani Mbeya,huku Trafiki alidai watakuwepo katika mizani pekee na ukaguzi ungefanyika katika mizani hiyo ila hadi sasa kimya