Adverts

Oct 8, 2012

KUPANDA OVYO KWA BEI YA MAFUTA KWACHANGIA MWITIKIO MDOGO WA MATUMIZI YA TREKTA MBOZIMbozi

Kupanda ovyo kwa gharama za mafuta kumetajwa kuwa na athari za kiwango cha juu katika uendeshaji wa kilimo cha kisasa na hasa matumizi ya zana kama trekta na vikokotozi maarufu kama powertillerkwenye wilaya maarufu kwa kilimo cha mahindi imefahamika.

Katika taarifa ya utafiti  aliyoiwasilisha Chuo cha Mipango Dodoma kwaaajili ya kuhitimu  stashahada ya uzamili katika mipango ya Mikoa, mtafiti Danny Tweve ameeeleza kuwa, katika  sampuli ya watu 103 walioshiiriki kwenye utafiti huo ni watu 4 tu waliokiri  kutumia teknolojia ya kisasa katika kulima mashamba yao.

Asilimia 98 ya washiriki wa utafiti walikiri kutumia jembe la mkono na wanyama kazi , na walipohojiwa sababu za kutotumia trekta ama powertiller kwa sehemu kubwa sababu zilizotolewa zilielekezwa kwenye gharama za mafuta kutovutia watu kuendelea kutumia teknolojia hiyo licha ya kutambua ukweli kwamba hurahisisha kazi.

Ingawa katika miaka ya 80 wilaya ya mbozi iliweza kupandisha idadi ya watumiaji wa teknolojia ya trekta kupitia mipango ya vijiji vya Ujamaa, gharama za mafuta, ukosefu wa vipuli na gharama za bidhaa hizo zilirejesha nyuma mwitikio wa wananchi hatua ambayo wengi wa wakulima walihamia kwenye matumizi ya jembe la mkono na wanyama kazi.
Utafiti huo uliofanywa katika vijiji vya Ivwanga na Mbimba unaonyesha kuwa kutokana na hali hiyo wananchi wengi wanapenda kubadili kilimo chao kutoka kile cha jembe la mkono kwenda kilimo cha kutumia zana za kisasa, hata hivyo suala la bei ya mafuta linaendelea kuwa kikwazo kwakuwa Dar es salaam ambako hawalimi ndiko mafuta yanakouzwa kwa bei ya chini ikilinganishwa na mikoani ambako mahitaji kwa shughuli za kilimo ni makubwa zaidi.
Bei ya Diesel katika wilaya ya Mbozi kwa wakati ambapo utafiti huo ulikuwa unafanywa ilikuwa ni shilingi 2300 ilihali mafuta hay ohayo jijini Dar es salaam ilikuwa 2005  kiwango ambacho kinathibitisha kuwa serikali haijaweka nia ya dhati kumsaidia mkulima kuondoknaana kilimo cha jembe la mkono.
Kutokana  na gharama kubwa za vilainishi, trekta bado limeendelea kuwa zana ya usafirishaji zaidi kuliko kutumiwa kama zana ya uzalishaji shambani ambapo idadi ya matrekta 79 yaliyopo wilayani humo kwa sehemu kubwa yanatumiwa kwaajili ya kusafirisha mizigo na kubebea mazao baada ya kuvuna, huku wamiliki wakillalamikia kukosa watu wa kukodisha hasa wananchi wa kawaida.
“ili uwe na uhakika na kurejesha mkopo wa trekta, ni lazima kwanza uwe na eneo la kutosha kwaaajili ya kujilimia mwenyewe na kuzalisha mahindi mwenyewe kwani ukitegemea kukodishwa kwa wananchi hawa wa kawaida itakula kwako” anaeleza mmoja wa wamiliki wa zana hizo bwana Mwazembe.
Aidha ufuatiliaji mdogo miongoni mwa makampuni yanayosambaza mbegu za mahindi umetajwa kuchangia kupunguza mwitikio wa wananchi katika kutumia mbegu za kisasa . Inaelezwa kuwa huduma za ugani kwa makampuni hayo na hasa ushauri umekuwa ukisitishwa mara tu wanapofanikiwa kutangaza mbegu  wanazozizalisha na kutoweka.
Hatua hiyo inapoteza dhana ya mwendelezo kwa mkulima hasa pale anapokumbana na changamoto mpya kutokana na matumizi ya mbegu husika, hivyo kupendekeza kuwepo kwa mfumo wa uratibu wa makampuni yanayosambaza mbegu kwa wakulima  kama njia ya kuyafanya yawajibike kwa bidhaa yanazozisambaza hii ikiwa ni pamoja na dawa  za kuulia wadudu na uhifadhi  wa nafaka.
Changamoto zingine zilizobainishwa kwenye utafiti huo ni pamoja  na ongezeko la malalamiko ya usambazaji wa bidhaa feki msimu hadi msimu ambapo mbegu za mahindi, Mbolea na dawa za kuulia wadudu vimekuwa  vikiwaingiza hasara wananchi kutokana na usimamizi mbovu wa soko la bidhaa hizo katika mikoa iliyopo mipakani.
Baadhi ya mbinu ambazo zimebainishwa na wananchi kwa upande wa mbegu za mahindi ni pamoja na wafanyabiashara kuchanganya mahindi yaliyohifadhiwa kwenye magunia na kuyaweka rangi zinazofanana na mbegu zinazopendwa na wakulima na hatimaye kuchapisha mifuko katika nchi jirani ambayo hutumia kusambaza mbegu hizo zikiwa na sura halisi ya mbegu zinazozalishwa na makampuni ya ndani
Kwa upande wa Mbolea imedaiwa kuwa wafanyabiashara wamekuwa wakichanganya na chokaa, chumvi na majivu ili kupata mifuko mitatu ya mbolea kutoka katika mfuko mmoja halali, wakati ambapo kwa upande wa dawa za kuulia wadudu, majivu, unga wa mahindi na rangi vimekuwa vikitumika kuwahadaa wakulima.

sehemu ya matokeo ya utafiti huo yamo kwenye taarifa ya utafiti "adoption of improved maize technologies among farmers in Ivwanga and Mbimba Villages in Mbozi District.