Adverts

Sep 10, 2012

NO maandamano Mikoani! Polisi watahadharisha


Maandamano yaliyopangwa na wanahabari nchini kote kufanyika kesho asubuhi huenda yasifanikiwe kwa mikoani baada ya taarifa za ndani kuonyesha kupenyezwa taarifa kutoka ngazi za juu za jeshi la polisi   zikitaka makamanda kuhakikisha hayafanyiki.
Taarifa kutoka mikoa mbalimbali zinaonyesha kuwa maandamano hayo yamekosa vibali kutoka polisi ambapo mikoa ya Mbeya na  Dodoma hadi saa nne usiku kulikuwa na taarifa za kusitishwa kwa maandamano hayo.
Mkoani  Mbeya wandishi wa habari walikutana kwenye ofisi yao leo jioni ambapo katika hali ya kushangaza watu wanaojiita wadau wa sekta ya habari walifika kuungana na wandishi kupanga namna ya kuandamana ambapo miongoni mwake walishtukiwa kuwa ni askari wa idara ya upelelezi ya jeshi la polisi.
Kutokana na hali hiyo wandishi waliwataka wadau hao wasubiri mazungumzo ya wanahabari yamalizike ndipo waruhusiwe, lakini baadaye wanahabari walikubaliana kutoshirikisha watu wengine kwenye maandamano hayo kwani yanahusu wana taaluma wa habari tu.
Hatua hiyo pia imelenga kuepusha mwendelezo wa ajenda mpya zinazozaliwa kutokana na tukio la kifo cha mwandishi wa habari Daud Mwangosi ambapo wanasiasa na makundi mengine ya jamii yanaweza kutumia fulsa hiyo kupenyeza ajenda zao.
Habari kutoka Dodoma zimesema, wandishi wa habari wa Mkoani humo walipanga kutekeleza maandamano ya amani ya kimya kimya lakini polisi imetoa taarifa kuwa haitaruhusu maandamano hayo kwani hayana kibali kutokana na kuchelewa kuombwa kibali hicho ndani ya saa 12.
Vivyo hivyo Mbeya ambao pia waliomba kibali kwa kuchelewa nao wamepewa taarifa za kuzuiwa maandamano hayo kwa siku ya kesho na kutakiwa kujiandaa kwa keshokutwa jambo ambalo litaenda kinyume na tangazo la muungano wa vyama vya wanahabari na vyombo vingine vilivyotangaza kuandamana kesho.