Adverts

Mar 10, 2013

INDABA NAYO ILICHANGIA MFUKO WA UJENZI WA MIUNDOMBINU RAFIKI KWA WATOTO WA KIKE

Mtendaji wa Indaba Africa Blog na Kampuni zake akizungumza na kutoa ahadi ya kuchangia ujenzi wa miundombinu rafiki kwa watoto wa kike wilayani Mbozi

RISALA YA WANAWAKE WILAYA YA MBOZI KWENYE USIKU WA MWANAMKE WILAYANI MBOZI
TAREHE 07/03/2013
Ndugu mgeni rasmi,
Wanawake wilayani Mbozi tunayofuraha kubwa kuwa nawe katika hafla hii ya usiku wa mwanamke wilayani Mbozi!
Ujio wako unatupa faraja na kutambua kwamba serikali imeendelea kuthamini jitihada mbalimbali zinazofanywa na mwanamke katika kujiletea maendeleo , pamoja na kuchangia katika ustawi wa familia na jamii kwa ujumla
Mheshimiwa mgeni rasmi
Wanawake wilayani MBOZI kwa kushirikiana na asasi za kijamii wameamua kubuni shughuli mbalimbali zenye tija katika ukombozi wa mtoto wa kike ambazo zitakuwa zikitekelezwa kila inapofanyika usiku wa mwanamke. Kwa mwaka 2013 wanawake wamebuni shughuli ya kuchangisha fedha na bidhaa zingine kwaajili ya kufanikisha ujenzi wa miundombinu rafiki yenye mtazamo wa kijinsia kwa watoto wa kike katika shule za sekondari.
Mheshimiwa Mgeni Rasmi
Kabla hatujafafanua utekelezaji wa mpango huu, tutoe angalau kwa ufupi chimbuko la siku ya mwanamke duniani. Kimsingi chimbuko lake ni matokeo ya maamuzi ya dhati ya wanawake kupinga kunyonywa na kudai hali bora katika mazingira ya kufanyia kazi pamoja na ushiriki katika kupiga kura, Mwanamke Clara  Zeltein aliongoza wanawake katika maandamano yaliyofanyika Agosti 26 hadi 27 ,1910 kupinga hali hiyo, na ndipo  march 8, 1957 katika mji wa New York nchini Marekani ilikubalika kuwa kila mwaka maadhimisho ya siku ya wanawake yatafanyika kila march 08 .
Hivyo hatua zinazoenda kuchukuliwa na asasi ya Mbozi society  kwa ushirikiano na SWAAT pamoja na wadau wengine wa maendeleo wilayani Mbozi ni mwendelezo wa harakati hizo.
Ndugu mgeni rasmi,
Kwa ujumla tunakusudia kujenga tanurutaka  kwaajiliya kuchomea taka maalumu zinazotumiwa na wanafunzi wa kike na walimu wao wawapo katika mazingira ya shule, Hatua hii ni muhimu katika kuondoa vikwazo vya kimazingira na miundombinu vinavyowakabili wasichana wawapo kwenye masomo yao, hii inatokana na kipindi cha mabadiliko ya makuzi kuhitaji mazingira na miundombinu rafiki  ili kuwawezesha kutoathiri mwenendo mzima wakati wa kupata elimu.
Tunatambua kuwa wakati huu serikali na wananchi kwa ujumla wanajiuliza  nini kilichopelekea matokeo mabaya ya kidato cha nne kwa mwaka 2012, Sisi  wanawake wa wilaya ya Mbozi tunatambua changamoto ya miundombinu na hasa ile rafiki kwa wanafunzi wa kike ni miongoni mwa mambo yaliyosababisha hali hiyo ya matokeo mabaya.
Ndugu mgeni rasmi
Chukulia shule ina wanafunzi wa kike waliobarehe 500 ambao wanatumia matundu  manne ya vyoo vya shimo, hivi tunategemea katika kipindi chao cha mzunguko wa kila mwezi ni kiasi gani cha taka kitakachoingizwa kwenye matundu ya vyoo hivyo na vitadumu kwa kipindi gani, jambo hili limekuwa halitazamwi sana katika mazingira yetu na hii inachangia pia kuwakatisha tamaa wanafunzi wa kike kutokana na wakati mwingine kuadhibiwa wakati wakisubiliana kupata huduma kwenye vyoo hivyo ambavyo kwa vyovyote vile haviwezi kudumu
Aidha watoto wakike walio katika mabadiliko hayo hawana vyumba maalumu vya kubadilishia taka hizo na matokeo yake wakati mwingine kulazimika kubaki na taka hizo mwilini kwa siku nzima hadi muda mwa masomo kumalizika. Kutokana na changamoto hizo wanawake tumeliona jambo hili kama moja ya changamoto za  elimu wilayani kwetu na tumeamua kuchua hatua kuanza kukusanya raslimali kwaajili  ya ujenzi huo.
Ndugu mgeni rasmi
Tunatarajia kuchangisha kiasi cha shillingi million million Tano katika kipindi cha mwaka mzima kwaajili ya kuwezesha kupatikana kwa miundombinu hiyo kwa baadhi ya shule tutakazozibaini katika maeneo ya ndani ya wilaya ambapo gharama za tanuru taka moja litagharimu shilingi 500,000 na vyumba vya kubadilishia nguo vitagharimu shilingi 800,000/=    
Tunapenda tena kukushuru mgeni rasmi kwa kuwa nasi usiku huu na sasa tunakukaribisha rasmi  katika kuzindua uchangiaji huu

 Ahsante

zainab Majubwa 
Mratibu-Mbozi Society