Adverts

Apr 1, 2013

HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANANCHI, TAREHE 31 MACHI, 2013


 Rais Jakaya Kikwete
--
 
HOTUBA YA MHE. JAKAYA MRISHO KIKWETE, RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, KWA WANANCHI, TAREHE 31 MACHI, 2013 
 --
Ndugu
Wananchi;


Naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu
kwa kutujaalia uhai na kunipa fursa ya kuzungumza nanyi kwa kupitia utaratibu wetu
huu mzuri wa kila mwisho wa mwezi. 
Leo ninayo mambo matatu ninayopenda kuzungumza
nanyi.


Ziara ya Rais wa China Nchini
Tanzania

Ndugu wananchi;



          Jambo la kwanza
ni ziara ya Mheshimiwa Xi Jinping, Rais wa Jamhuri ya Watu wa China aliyoifanya
nchini kwetu kati ya tarehe 24 na 25 Machi, 2013. 
Lengo la
ziara yake ilikuwa kuimarisha uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya China na
Tanzania.  Napenda kuchukua nafasi hii
kuwashukuru wakazi wa Dar es Salaam kwa kumpokea vizuri mgeni wetu na ujumbe
wake.  Wameondoka wakiwa na kumbukumbu
nzuri ya nchi yetu na watu wake. 







Kwa niaba yenu,
nimepokea salamu za shukrani kutoka kwa Rais Xi Jinping akielezea kufurahishwa
na mapokezi mazuri tuliyowapatia. Naomba tuendelee kuonesha moyo wa upendo na
ukarimu kwa wageni wetu wengine mashuhuri watakaotutembelea siku za usoni.


Ndugu wananchi;


Nami pia, nimemshukuru
sana Mheshimiwa Xi Jinping kwa kukubali mwaliko wangu na kufanya ziara ya
kihistoria na yenye mafanikio makubwa kwa nchi yetu.  Ameifanyia nchi yetu jambo la heshima kubwa
na kumbukumbu isiyosahaulika.  Tanzania
imekuwa nchi ya kwanza Barani Afrika kuitembelea, tena siku kumi tu baada ya
kuchaguliwa kuwa Rais wa nchi yake.  Na,
kubwa zaidi ni kutumia fursa ya ziara yake hapa nchini kutangazia dunia Sera ya
China kwa Afrika katika kipindi cha uongozi wake. 


Tumefarijika sana
kusikia kuwa uhusiano na Afrika bado unapewa kipaumbele cha juu na viongozi
wapya wa China.  Pia, kuwa China
itaendelea kukuza biashara na uwekezaji na kuongeza misaada ya maendeleo kwa
Afrika ikiwemo kutoa nafasi 18,000 za mafunzo kwa vijana wa Kiafrika.  Kama mtakumbuka nchi zetu mbili zilitiliana
saini mikataka 16 ya ushirikiano katika nyanja mbalimbali.  Misaada ya maendekeo kwa maeneo yetu ya
kipaumbele nayo imejumuishwa.


Ndugu Wananchi;


Rais Xi Jinping
alielezea na kusisitiza dhamira yake na ya Serikali na Chama cha Kikomunisti
cha China ya kudumisha na kukuza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na
China. Kama mjuavyo uhusiano huo ulianzishwa mwaka 1964 na waasisi wa nchi
zetu, yaani Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyekuwa Rais wa kwanza wa
Tanzania na Mwenyekiti Mao Zedong aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa China na Waziri
Mkuu wake Chou En Lai. 


Rais wa China aliahidi
kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Tanzania katika medani ya kimataifa
na kuchangia katika jitihada zetu za kujiletea maendeleo kwa kuongeza misaada
ya maendeleo.  Katika miaka 49 ya
uhusiano na ushirikiano na China nchi yetu imepata misaada mingi ya maendeleo
ikiwemo Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere ambao ulizinduliwa
na Rais Xi Jinping wakati wa ziara yake.


Ndugu
wananchi;


Kuna miradi kadhaa
mikubwa inayoendelea kutekelezwa nchini, Bara na Zanzibar, kwa msaada wa
Serikali ya China.  Wakati wa ziara yake,
Rais Xi Jinping iliahidi kuendelea kutusaidia miradi mingine ya maendeleo kama
tulivyoomba wakati wa mazungumzo yetu licha ya ile ambayo ilitiwa saini siku
ile. 


Ajali ya Kuporomoka Jengo la Ghorofa


Jijini Dar es Salaam




Ndugu Wananchi;



         Jambo la pili ninalotaka kuzungumzia ni ajali ya kuporomoka
kwa jengo la ghorofa 16 lililokuwa
linajengwa katika jiji la Dar es Salaam.
Ajali hiyo iliyotokea juzi tarehe 29 Machi, 2013 imeleta msiba na
simanzi kubwa nchini.  Mpaka sasa maiti
za ndugu zetu 30 zimepatikana.  Watu 17
waliweza kuokolewa, wanne kati yao bado
wanaendelea na matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.  Wengine walitibiwa na kuruhusiwa.  Kazi ya kufukua eneo la ajali inaendelea na
sasa inakaribia kufikia ukingoni. 


Ndugu Wananchi;



         Mimi na viongozi wenzangu tulipata nafasi ya kwenda kuangalia
eneo la ajali.  Hali niliyoiona pale
imenihuzunisha sana.  Lazima nikiri, hata
hivyo, kwamba nimeridhishwa sana na juhudi kubwa za uokoaji zilizokuwa
zinafanywa na wanajeshi wetu wakishirikiana na taasisi, mashirika binafsi na
wananchi.  Napenda kutumia nafasi kutoa
shukrani maalum kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Ndugu Saidi Meck Sadick kwa
uongozi wake madhubuti.  Pia nampongeza
Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ndugu Raymond Mushi, na Kamanda wa Polisi Kanda Maalum
ya Dar es Salaam, Ndugu Suleiman Kova pamoja na Maafisa na askari wa JWTZ, na
wale wote walioshiriki na wanaoendelea kushiriki katika juhudi za uokoaji. 



         Nawapongeza pia madaktari na wauguzi wa Hospitali ya Taifa
ya Muhimbili na hospitali nyinginezo kwa jitihada zao za kuokoa maisha ya
waliojeruhiwa.  Nawapa pole wale wote
waliofiwa na wapendwa, ndugu na jamaa zao katika ajali hii.  Nawaomba wawe na moyo wa subira huku sote
tukiungana nao kuwaombea marehemu wetu wapate mapumziko mema peponi.  Kwa waliojeruhiwa, tunawaombea wapone
upesi. 


Ndugu Wananchi;



         Maneno mengi yanasemwa kuhusu chanzo cha ajali ile.  Alimradi kila mtu ana dhana yake.  Niliagiza vyombo na mamlaka husika wachukue
hatua zipasazo kuchunguza sababu za ghorofa hilo kuanguka na watakaothibitika
kusababisha maafa hayo  wachukuliwe hatua
zipasazo.  Wa kushtakiwa Mahakamani
washitakiwe na wa kufutiwa leseni za kufanya shughuli za ujenzi au taaluma zao
wafutiwe bila ajizi.  Jambo la msingi la
kusisitiza ni kuwa mamlaka zinazohusika na usimamizi wa ujenzi lazima zitimize
ipasavyo wajibu wake.  Naamini kama
mamlaka hizo zingetimiza ipasavyo wajibu wake ajali hii ingeepukika.  Halmashauri za miji na wilaya zina wajibu
maalum kwenye ujenzi katika maeneo yao.
Watimize wajibu wao.  Yaliyotokea
Dar es Salaam yawe fundisho kwa wote. 



        


Ndugu Wananchi;



         Ni matumaini yangu kuwa Bodi ya Usajili wa Wakandarasi na
Bodi ya Usajili wa Wahandisi itakamilisha mapema uchunguzi wake ili ukweli
ujulikane.   Bodi ya Usajili wa Wasanifu
Majengo na Wakadiriaji Majenzi na Baraza la Taifa la Ujenzi nao washirikishwe
kwa ukamilifu ili ukweli upatikane na hatua stahiki zichukuliwe.  Pia naomba washauri namna bora ya kukomesha
ajali za aina hiyo siku za usoni.


Uhusiano wa
Wakristo na Waislamu


Ndugu
Wananchi;



          Jambo la tatu ninalopenda kuzungumza nanyi leo ni uhusiano
wa Waislamu na Wakristo nchini.  Jambo
hili nimeshalizungumzia mara kadhaa siku za nyuma, lakini nalazimika kulisemea
tena kutokana na hali ilivyo sasa.
Tumefikia mahali ambapo kama viongozi na waumini wa dini hizi kubwa
mbili hawatakubali kubadili muelekeo wa sasa, tunakoelekea ni kubaya.  Nchi yetu nzuri tutaivuruga na sifa yake ya
miaka mingi ya Waislamu na Wakristo kuishi pamoja kidugu, kwa upendo,
ushirikiano na kuvumiliana itatoweka.
Tanzania itaacha kuwa kisiwa cha amani na kuingia katika orodha ya nchi
zenye migogoro na hata vita vya wenyewe kwa wenyewe.


Ndugu
Wananchi;


Nyaraka na kauli kali kali zinazotolewa na viongozi wa dini za Kikristo na
Kiislamu zinanishawishi kuamini haya niyasemayo.  Nyaraka na kauli hizo zina mambo mawili
makuu.  Kwanza, kwamba kila upande
unatuhumu, kushutumu na kulaumu upande mwingine kwa kufanya vitendo viovu dhidi
ya dini yake.  Kauli na mihadhara ya
kudhalilisha dini za wengine, kunajisi vitabu vitakatifu, kuchoma moto nyumba
za ibada, mzozo kuhusu nani achinje na kuuawa kwa viongozi wa dini ni baadhi ya
mambo yanayotolewa mifano.



 Na, pili kwamba kila upande unailamu
Serikali kwa kupendelea upande mwingine. Wakristo wanalaumu kwamba mihadhara ya
kudhalilisha Ukristo inaendeshwa na Serikali haichukui hatua.  Aidha, Wakristo wanateswa na viongozi wao
kuuawa na Waislamu, lakini Serikali haichukui hatua.  Kwa ajili hiyo wanadai kuwa Serikali
imeshindwa kulinda uhai wa raia wake.
Wanasema pia kwamba Serikali inapendelea upande wa Waislamu. 


Ndugu
Wananchi;


Waislamu nao wanadai kuwa kitabu chao kitakatifu, yaani Quran Tukufu,
kinadhalilishwa kwa kuchanwa, kuchomwa moto na kukojolewa na Wakristo na
Serikali haichukui hatua yo yote ya maana. Waislamu wananyanyaswa katika nchi
yao, wanakamatwa ovyo, hawapewi fursa sawa na kwamba Serikali inawapendelea
Wakristo.  Wanasema nchi inaendeshwa kwa
mfumo wa Kikristo. Mimi binafsi wananishutumu kuwa napendelea kushiriki zaidi
kwenye shughuli za Wakristo kuliko za Waislamu kama vile harambee za kujenga
Makanisa na shule za Makanisa.  Naambiwa
kuwa mwepesi kushiriki maziko ya Maaskofu kuliko Masheikh wanapofariki. Ipo
Misikiti mitatu hapa Dar es Salaam wamenisomea itikafu nife.  Katika itikafu hiyo wamewajumuisha Inspekta
Jenerali wa Polisi, Said Mwema na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es
Salaam, Kamishna Msaidizi Mwandamizi Ndugu Suleiman Kova.


Ndugu
Wananchi;



          Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa mimi na
Serikali ninayoiongoza, hatupendelei upande wo wote.  Hatufurahishwi na kitendo cha mtu
kudhalilisha dini ya mwenzake ndiyo maana wapo wahadhiri wa dini ya Kiislamu na
wahubiri wa dini ya Kikristo wamekamatwa na kufunguliwa mashtaka kwa nyakati
mbalimbali.  Vyombo vya usalama
vinatambua wajibu wake huo na kama haifanyiki ni ulegevu wa mtu tu katika
kutimiza wajibu wao na siyo kwamba ni sera na maelekezo yangu au ya
Serikali.  Mtakumbuka kuwa mara kadhaa
nimewakumbusha Wakuu wa Mikoa na Wilaya na wakuu wa vyombo vya usalama kuacha
ajizi katika kutimiza wajibu wao kwenye suala hili.


Ndugu
Wananchi;


Mimi binafsi sibagui, hushiriki shughuli za Waislamu na Wakristo kila
ninapoalikwa labda nikose nafasi kwa sababu nyinginezo.  Nimeshafanya shughuli nyingi za Waislamu kama
vile Maulid ya Mtume Muhamad S.A.W., safari za Hija, ujenzi wa misikiti na
madrasa na mengineyo mengi.
Nimeshashiriki mazishi ya Masheikh kama nifanyavyo kwa Maaskofu na watu
mbalimbali Waislamu na Wakristo.  Pale
ambapo sikushiriki mazishi ya Sheikh au Askofu itakuwa ni kwa sababu ya kubanwa
na shughuli nyingine ambazo lazima nifanye mimi, au taarifa ilikuwa ya muda
mfupi.  Kwa upande wa Waislamu desturi
yetu ya kuzika mara mtu anapofariki huwa kikwazo kwangu kushiriki hasa ikiwa ni
nje ya Dar es Salaam kwa sababu ya taratibu za kumsafirisha Rais kutoka mahali
pamoja kwenda pengine siyo nyepesi.   Wakristo
hawana utaratibu huo, huwa wanaweza kusubiri hivyo huniwia rahisi kushiriki.


Ndugu
Wananchi;


Napenda kuwahakikishia kuwa Serikali yetu haijashindwa kulinda usalama wa
raia wake au viongozi wa dini na nyumba za ibada.  Kama ingekuwa hivyo, tungeshuhudia mauaji ya
raia, viongozi wa dini na matukio ya kuchomwa nyumba za ibada yakiwa mengi hapa
nchini.  Lakini hivyo sivyo.  Nawasihi sana ndugu zangu Wakristo na
Waislamu kuwa tusiyachakulie matukio ya kuuawa kwa Mchungaji Mathayo Kachila
kule Buseresere, Geita, na Padri Evaristus Mushi kule Zanzibar, au kumwagiwa
tindikali Sheikh Fadhili Soroga, Naibu Mufti wa Zanizbar, kupigwa risasi Padri
Ambrose Mkenda na kuchomwa moto kwa Makanisa Zanzibar na Mbagala, Dar es Salaam
kuwa ni kielelezo na ushahidi wa Serikali kushindwa kutimiza wajibu wake.


Kila tukio lina mazingira yake, hakuna ushahidi wa vyombo vya Serikali
kuzembea.  Hakuna ushahidi wa matukio
hayo kuunganika.  Mpaka sasa hatujapata
ushahidi wa kuwepo kikundi cha Waislamu wanaopanga kuua viongozi wa Kikristo na
kuchoma moto Makanisa hapa nchini. 


Ndugu
Wananchi;


Kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila wa Buseresere ni matokeo ya vurugu
zilizosababishwa na mzozo kati ya Wakristo na Waislamu kuhusu kama nyama
iliyochinjwa na Wakristo Kanisani nayo iuzwe kwenye bucha iliyopo pale kijijini
ambayo kwa mazoea huuzwa nyama iliyochinjwa na Waislamu.  Katika ugomvi na vurumai hizo ndipo watu
kadhaa wa pande zote walijeruhiwa na Mchungaji kupoteza maisha.  Si tukio unaloweza kulihusisha na mengineyo
nchini.  Ni la pale pale Buseresere na
limeanzishwa na kuhusisha Wakristo na Waislamu wa Buseresere kwa sababu
zao.  


Hivi kama kusingekuwepo na mzozo wa nyama ile kuuzwa katika bucha ile
kuumizana kule na mauaji yale yangetokea? Kabla ya mzozo ule Wakristo na
Waislamu wa Buseresere hawakuwa na ugomvi baina yao.  Walikuwa wanaishi kidugu na kushirikiana
katika shughuli zao za kujitafutia riziki huku kila mmoja akimuabudu Mungu kwa
misingi ya dini yake.  Hivyo kutumia
tukio hilo kutoa wito kwa Wakristo wote kuwa kuuawa kwa Mchungaji Kachila ni
sawa na kuuawa kwa Wakristo wote nchini kulikofanywa na Waislamu ni kulikuza
tatizo isivyostahili.  Busara ituongoze
kutafuta njia ya kuwapatanisha Wakristo na Waislamu wa Buseresere wazungumze, waelewane
na waendelee kuishi pamoja kama ilivyokuwa awali.  Hata mzozo wa kuchinja wanaweza
kuumaliza.  Mbona bucha za kitimoto zipo
na watu hawajapigana. Kutumia mzozo wa Buseresere kueneza chuki kati ya
Wakristo na Waislamu nchi nzima si sawa.
Hatuwatendei haki Watanzania.   


Ndugu
Wananchi;



          Kuuawa
kwa Padri Evaristus Mushi wa Zanzibar ni tukio linalojitegemea halina uhusiano
kabisa na lile la Buseresere, Geita.
Hapakuwa na mzozo kuhusu nani achinje.
Bado uchunguzi wake unaendelea na tumehusisha vyombo vya upelelezi vya
nje vishirikiane na vyetu kufanya uchunguzi.
Tumefanya hivyo kwa sababu ya ugumu uliopatikana katika uchunguzi wa
matukio ya kabla yake.  Yaani ile la
kupigwa risasi na kujeruhiwa kwa Padri Ambrose Mkenda na kumwagiwa tindikali
kwa Naibu Mufti wa Zanzibar Sheikh Fadhili Soroga.  Bado hakuna mafanikio ya kutia moyo.  Na bado tunajiuliza kama matukio hayo matatu
yanahusiana.  Je, Makanisa kuchomwa moto
kule Zanzibar nako kuna uhusiano wowote na matukio yale matatu?  Uchunguzi unaoendelea unaweza kufumbua fumbo
hilo. 



 Kuna watu wanadhani yanahusiana na
kwa sababu nzuri.  Lakini inabaki kuwa ni
dhana ya kibinadamu mpaka ukweli halisi utakapobainika.  Bado kazi ya uchunguzi inaendelea kufanywa na
vyombo vya usalama vya nchi yetu wakishirikiana na wenzao wa nje.  Katika mazingira hayo, ni mapema mno
kumnyooshea kidole mtu ye yote na kuilaumu Serikali ya Muungano au Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar.    Serikali siyo
mshirika katika mauaji hayo, na haina sababu ya kufanya hivyo.  Ndiyo maana tunahangaika usiku na mchana
kupata jawabu.


Ndugu
Wananchi;



          Hali kadhalika tukio la
Makanisa ya Mbagala, Dar Es Salaam kuvamiwa, kubomolewa, mali kuibiwa na
kuchomwa moto tarehe 12 Oktoba, 2012 nalo lina mazingira yake maalum.  Chanzo chake ni mzozo uliotokana na tukio la
kusikitisha la kijana mmoja Mkristo kukojolea Kitabu Kitakatifu cha Waislamu,
yaani Quran Tukufu.  Pamoja na maelezo
kuwa walikuwa na ubishi wa kitoto na kijana mwenzake, lakini kitendo hicho
kiliwakasirisha Waislamu.  Kijana huyo
alifikishwa kituo cha Polisi.  Baadhi ya
Waislamu wenye msimamo mkali walifika kituoni hapo wakidai wapewe huyo kijana
wamuadhibu wao.  Jeshi la Polisi
lilikataa.  Kukatokea mzozo kati ya
waumini hao na Polisi na baada ya kushindwa walichokitaka baadhi yao walipotoka
pale, wakaenda kufanya uhalifu wa kuvunja, kuiba na kuchoma moto Makanisa. 


Ndugu
Wananchi;


Baada ya tukio la Mbagala hapajakuwepo na tukio la kuchomwa Kanisa mahali
popote kwa upande wa Bara.  Aidha,
hapajawahi kuwepo tishio lililothibitika la watu kutaka kuchoma Kanisa popote.  Lakini maneno ya vitisho vya kuchoma Makanisa
yako mengi hasa kupitia mitandao ya simu za mkononi.  Kila ujumbe wa namna hiyo ulipofikishwa
kwenye vyombo vya usalama uchunguzi umefanywa na hata hatua za tahadhari
kuchukuliwa lakini hakuna hata taarifa moja iliyothibitika kuwa na chembe ya
ukweli.  Hata dalili hazijakuwepo. 


Tulichojifunza ni kuwa ujumbe na vitisho vya aina mbalimbali hupelekwa
kote, kwa Wakristo na Waislamu.  Upo
unaowalenga Wakristo ukiwaambia wenzao Waislamu wanapanga kuwadhuru.  Na upo wanaopelekewa Waislamu wakiambiwa
Wakristo wanao mipango mibaya dhidi yao. 
Watanzania wenzangu nawaomba mtanabahi na mjue kuwa wapo watu wanacheza
mchezo mchafu wa kuwagonganisha na kutaka kuwagombanisha Wakristo na Waislamu
kwa sababu wanazozijua wao na kwa faida yao.
Wanapandikiza chuki kwa lengo la kutaka Wakristo na Waislamu
wagombane.  Wanapandikiza chuki baina ya
Serikali na waumini wa dini zetu kuu mbili ili ionekane Serikali imewatelekeza
raia wake.  Ni mchezo mbaya, tusikubali
kucheza ngoma tusiyoijua. Hivi ndugu zangu mmekaa chini na kujiuliza kumetokea
nini kipya hata leo kuwa na mhemko kama huu kati ya Wakristo na Waislamu na
kutishia kuleta vita baina nchini kote? 


Ndugu
Wananchi;



          Serikali haijapuuzia kila
palipotokea matukio ya uhalifu. Watu 76
wanaotuhumiwa kuharibu na kuchoma moto Makanisa kule Mbagala na kufanya fujo
kituo cha Polisi wamekamatwa na kesi zao zinaendelea Mahakamani.  Kwa upande wa tukio la Buseresere
lililosababisha kifo cha Mchungaji Mathayo Kachila, watu 17, wakiwemo waumini wa dini ya Kikristo na Kiislamu walikamatwa na
kesi zao zinaendelea. Wapo walioshitakiwa kwa mauaji na wapo walioshitakiwa kwa
kufanya vurugu.  Jeshi la Polisi bado
linawatafuta watu wengine waliohusika na uhalifu huo ili na wao wakamatwe. Kwa
upande wa Zanzibar, watu 10
wanaotuhumiwa kuchoma Makanisa wamekamatwa na kesi zao zinaendelea.  Bado hajakamatwa mtu kwa tukio la mwisho la
kuchoma Kanisa baada ya kuuawa Padri Evaristus Mushi.  Uchunguzi unaendelea.


Ndugu
Wananchi;


Kwa upande wa kujeruhiwa kwa Padre Mkenda, bado uchunguzi haujakamilika
pamoja na kuwapo taarifa kadhaa zinazoendelea kufanyiwa kazi.  Kuhusu uchunguzi wa mauaji ya Padre Mushi,
baada ya jitihada kubwa kufanyika ikiwa ni pamoja na kushirikisha nchi zilizobobea
katika uchunguzi wa makosa ya aina hii, hatua ya kutia moyo imefikiwa.  Mtu mmoja amekamatwa na wengine wanaendelea
kutafutwa. 


Ndugu
Wananchi;


Kwa upande wa kanda na vituo vya redio nako pia Serikali imechukua
hatua.  Watu kadhaa wamekamatwa na
kufikishwa Mahakamani katika maeneo mbalimbali hapa nchini kwa kurekodi na
kusambaza kanda zinazochochea chuki na vurugu za kidini.  Wapo Waislamu na Wakristo. Wapo watu wengine
ambao wanaendelea kutafutwa.  Zipo taarifa
kuwa baadhi yao wamekimbilia nchi za nje. Jeshi la Polisi limeomba msaada wa
Polisi wa Kimataifa, yaani Interpol, kusaidia kuwatafuta na kuwarejesha
nchini.  Vituo viwili vya radio yaani Kwa
Neema FM cha Sengereme na Radio Imani cha Morogoro vimefungiwa kwa muda wa
miezi sita.  Baada ya muda huo kupita,
Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano itaamua ipasavyo.


Ndugu
Wananchi;



          Nimeyaeleza haya kwa kirefu
kuwahakikishia kuwa Serikali inajali usalama wa raia wake wa mali zao na amani
na utulivu wa nchi yetu.  Kamwe
hatujashindwa kulinda raia wa nchi wa yetu na yapo mambo mengi yaliyofanyika na
yanayoendelea kufanyika kuhakikisha kuwa Watanzania wa dini zote, makabila
yote, rangi zote na mahali po pote walipo wako salama.  Tunataka kuona watu wanaendelea kuishi kwa
amani, upendo, ushirikiano na mshikamano kama tulivyokuwa tunaishi siku
zote.  Tunapenda kuona Watanzania
wanaepuka mambo yanayowabagua na kusisitiza yale yanayowaunganisha.  Tujiepushe kuyapa kipaumbele yale
yanayotugawa.


Ndugu
Wananchi;



          Athari za mzozo kuhusu kuchinja kule Geita iwe fundisho
kwetu sote.  Tuazimie sote kuwa
yaliyopita si ndwele, tugange yajayo.
Hebu tufikirie maisha yetu Watanzania yatakuwaje kwenye shughuli za
kijamii kama vile sherehe, harusi, ngoma na misiba iwapo tutaanza kuwa na
chakula tofauti kwa Waislamu na Wakristo. Fikiria itakuwaje kwenye hospitali,
shule na  vyuo pawe na majiko mawili au
labda hata mabwalo mawili ya chakula kwa Waislamu na Wakristo. Jeshini nako
kuwe na majiko na mabwalo ya Waislamu na Wakristo.  Hali iwe hivyo hivyo kwenye migahawa na
maeneo mengine yenye huduma ya chakula.


Ndugu zangu, tunataka kuipeleka wapi nchi yetu? Tunataka kujenga nchi ya
namna gani? Mimi naamini tukifanya hivyo huo utakuwa ndiyo mwanzo wa kubaguana
kwa kila kitu na kila jambo na kuligawa taifa kwa namna ambayo hatutakuwa
wamoja tena.  Huko tunakoelekea siko, ni
kubaya. Tubadilike, na wakati ni huu.
Viongozi wa dini waongoze njia wawaepushe waumini wao na taifa letu na
janga hili.  


Ndugu
Wananchi;



          Bado narudia kusisitiza umuhimu wa viongozi wa dini zetu
kubwa mbili kukutana na kuizungumzia hali hii na kuipatia ufumbuzi.  Ni wao kuliko mtu mwingine ye yote wenye
majawabu ya matatizo haya.  Ni masuala
yanayohusu imani za dini na yanafanywa na viongozi wa dini na wafuasi wao kwa
jina la dini zao.  Serikali ina wajibu wa
kulinda amani. Kazi yetu itakuwa rahisi kama waumini hawatafanya vitendo
vitakavyosababisha uvunjifu wa amani. Wa kuongoza waumini lipi jema na lipi
baya ni viongozi wa dini. 


Ndugu
Wananchi;



 Nimeshakutana na viongozi kadhaa wa
madhehebu na taasisi za dini za Kikristo na Kiislamu kuzungumza nao kuhusu
jambo hilo.  Nimepata faraja kuona kuwa
wote wanasikitishwa na mambo yanayotokea hivi sasa na wameona busara ya
viongozi wa dini kuzungumza ili kuondoa tofauti zilizojitokeza.  Wanakiri kuwa hali ilivyo sasa siyo ya
kawaida kwa Tanzania na Watanzania.  Kuna
upepo mbaya wa shetani unapita ambao viongozi wa dini wana wajibu wa
kuhakikisha kuwa hali ya hewa inasafishwa na kurejesha nchi yetu na watu wake
katika maisha tuliyoyazoea.  Maisha
ambayo waumini wa dini tofauti wanaishi pamoja kwa udugu, upendo, ushirikiano
na mshikamano kwa misingi ya ubinadamu wao na Utanzania wao.


Waziri Mkuu, Mheshimiwa Mizengo Pinda, ameshaeleza dhamira ya Serikali ya
kuitisha mkutano wa viongozi wa dini mapema mwezi ujao.  Ni matumaini yangu kuwa wote watashiriki
wenyewe bila ya kutuma wawakilishi.
Lazima tupate jawabu kwa maslahi ya taifa letu na watu wake.


Ndugu
Wananchi; 


Kabla ya kumaliza hotuba yangu napenda kutumia nafasi hii kuwaomba na
kuwasihi waandishi wa habari wasaidie kuliepusha taifa letu kuingia katika vita
vya kidini.  Waache kushabikia taarifa
zinazochochea na kujenga uhasama baina ya waumini wa dini zetu.  Nawaomba wapime athari za taarifa zao kabla
ya kuziandika au kuzitangaza.  Wawe
makini na maneno wanayotumia.  Katika
hali tuliyonayo sasa lazima sote tuazimie kuondoa tofauti za kidini na kujenga
umoja miongoni mwa Watanzania wa dini zote.
Wasipofanya hivyo, wataliingiza taifa katika mgogoro mkubwa ambao hauna
msingi kama ilivyotokea katika nchi jirani.
Nawaomba wamiliki wa vyombo vya habari kutambua kuwa wanao wajibu wa
kuhakikisha vyombo vyao havitumiki kuleta mifarakano kwa kuchochea uhasama
baina ya Wakristo na Waislamu.


Hitimisho


Ndugu
Wananchi;



          Naomba kumaliza kuwa kusisitiza kuwa wananchi wote
kudumisha umoja na mshikamano wetu.  Tuishi
kwa upendo, umoja, mshikamano na ushirikiano bila kujali tofauti ya dini zetu,
kabila, rangi au mahali atokako mtu.
Hizo ndizo tunu za taifa letu la Tanzania ambazo hatuna budi kuzienzi,
kuzilinda na kuzidumisha. Narudia kuwahakikishia kuwa Serikali haipendelei dini
yo yote na wala haina mpango wa kushiriki kuangamiza dini yo yote au waumini
wao.  Serikali kupitia vyombo vyake vya
usalama itaendelea kuhakikisha ulinzi na usalama wa raia wake na mali zao kama
inavyofanya siku zote.  Kama kuna mtu
anaona kuwa maisha yake au mali zake zipo hatarini, aende kutoa taarifa
Polisi.  Hatua zipasazo zitachukuliwa.


Ndugu
Wananchi;


Mwisho nawatakia sikukuu njema ya Pasaka.
Tusherehekee kwa amani na utulivu.
Tusherehekee pamoja.




Mungu Ibariki Afrika!


Mungu Ibariki Tanzania!


Asanteni kwa Kunisikiliza.