Adverts

Oct 30, 2013

MPANGO WA UTOAJI WA CHAKULA MASHULENI BADO WASUA SUA


 Mmoja wa madiwani Mh Kalonge kutoka kata ya Igamba akiwasilisha taarifa ya utendaji na uwajibikaji kwa kata yake

Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya Mbozi Mh Allan Mgula kushoto akiwa na kaimu Mkurugenzi Mtendaji Mbozi Bwana Zabron Lulandala  kwenye kikao cha jana

Na Danny Tweve wa Indaba Africa
Mpango wa utoaji chakula shuleni katika wilaya ya Mbozi , umeendelea kupanuka ingawa kwa meeneo mengi umekuwa ukifanyika kwa vipindi maalumu imebainika.
Katika kikao cha kuwasilisha taarifa za utendaji toka ngazi ya kata zilizowasilishwa na madiwani ikiwa ni utaratibu wa halmashauri kupima  uwajibikaji wa waheshimiwa madiwani, baadhi ya kata zimefanikiwa kueneza mpango huo kwenye vijiji vyote
Kulingana na taarifa hizo kuna kata zenye akiba ya chakula cha miezi 8 kwaajili ya kuhudumia wanafunzi kwenye shule za msingi na  kata zingine bado hazijatekeleza mpango huo kabisa.
Kulingana na taarifa zilizowasilishwa kuna jumla ya gunia 206 za mahindi zilizochangwa na wananchi kuwezesha utoaji wa huduma ya chakula mashuleni hasa kwenye ngazi ya elimu ya msingi, hata hivyo kulingana na idadi ya wanafunzi uwiano wa chakula  hicho kwa idadi ya wanafunzi waliopo wilayani ni sawa na  mlo wa siku mbili ambapo wastani kwa siku mtoto anakula 0.11 kg za wanga.
Wilaya ya Mbozi ina jumla ya wanafunzi 91,311 ambao kati yao 648 ni wa kutoka shule mbili binafsi za msingi na wengine 90,663 ni kutoka shule 155 za serikali.
Hali hii inaonyesha kurudi nyuma katika utoaji wa huduma ya chakula ikilinganishwa na robo ya mwaka iliyopita ambapo taarifa zilizowasilishwa zilionyesha baadhi ya kata zilikuwa zimefikia kuchangia gunia 70 za mahindi.
Kulingana na mwelekeo wa uchangiaji, ni dhahiri katika kipindi hiki cha kuelekea masika, uchangiaji utapungua badala ya kuongeza kwa kuwa kipindi cha mavuno (Julai hadi Septemba) hapakuwekwa msukumo mkubwa kwa wananchi kuchangia chakula  cha watoto mashuleni.
Kata ambazo zimeonekana kufanya vizuri katika uchangiaji huo ni pamoja na Myovizi ambayo shule zake zote saba zinatoa huduma ya chakula, Isandula ambayo shule tano kati ya nane zinatoa chakula, Isansa ambayo shule 6 kati ya 16 zinatoa chakula, Ipunga shule Mbili zinatoa chakula kati ya 5 na Mlowo shule 2.
Zingine ni Vwawa shule 2, Nyimbili shule mbili, Iyula shule 3 na Itaka shule 3. Kulingana a na takwimu hizo kuna baadhi ya kata ambazo katika robo ya kumalizia mwaka wa fedha 2012-2013 ziliweza kutoa chakula lakini sasa zimerudi nyuma zikiwemo Nanyala, Halungu, Igamba na Ruanda.

Ili kuongeza msukumo kwenye usimamizi wa suala la chakula, vikao vya  mabalaza ya madiwani  vya kivyama ambavyo huketi kabla ya baraza la madiwani la halmashauri, vinapaswa kujadili kwa upana suala hilo ili kuweka msukumo wa makusudi katika kuwezesha utekelezaji wa mpango wa uchangiaji chakula mashuleni uweze kutekelezwa.