Adverts

Feb 4, 2014

SIKU YA SHERIA MBOZI- OFISA UPELELEZI ALIA NA KUTOWEZESHWA

WATU MBALIMBALI WALIOSHIRIKI MAADHIMISHO WAKIWA KWENYE PICHA YA PAMOJA
 HAKIMU MFAWIDHI MAHAKAMA YA WILAYA MBOZI RAHIM MUSHI KATIKATI MWENYE JOHO AKIWA NA WAGENI WAALIKWA KWENYE MAADHIMISHO YA SIKU YA SHERIA
 WAKILI BW. DEOGRATIUS NCHIMBI AKIZUNGUMZIA UTENDAJI WENYE KUWAJIBIKA
 Afisa Upelelezi wilaya ya Mbozi Bw. NICKOBAY MWAKAJINGA alizungumza
 wadau wa mahakama wakifuatilia hotuba ukumbini

Na Danny Tweve –Mbozi
Mkuu wa upelelezi wilayani Mbozi OCCID BW NICKOBAY MWAKAJINGA amesema ucheleweshaji wa haki kwa idara ya upelelezi ni matokeo ya hali mbaya inayoikabili jeshi la polisi kwa kukosa vitendea kazi.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya sheria, iliyoadhimishwa mahakama ya wilaya ya Mbozi, Bw Mwakajinga amesema hali hiyo wakati mwingine imefikia hatua ya kulidhalilisha jeshi kutokana na askari kuvaa mchanganyiko hasa kwenye maeneo ya baridi kutokana  na kukosekana masweta na makoti maalumu wakati wa kazi na badala yake kuvaa nguo za mitumba mchanganyiko.

Amesema huwezi kuamini hadi filimbi za kukamatia mwizi siku hizi tunanunua madukani hizi za mgambo” alieza mahakamani hapo na kuwataka wadau wa mahakama kulisaidia jeshi hilo vitendea kazi ili liweze kutoa huduma bora
Amefafanua kuwa wakati mwingine imejitokeza kushindwa kuwahi maeneo yenye matukio kutokana na kukosekana mafuta, hali ambayo pia wakati mwingine kuchangia kuharibu ushahidi pale ambapo uchunguzi unahitaji pia mamlaka nyingine kama madaktari.

Hata hivyo amepongeza hatua ya kuwaandalia mafunzo ya mara kwa mara ambayo yamewawezesha polisi wa upelelezi kujifunza mbinu mpya za kukabiliana na uhalifu, hata hivyo wakati mwingine wamekuwa wakishindwa kuunganisha mafunzo hayo na hali halisi kutokana na kukosekana vitendea kazi kwenye ngazi za chini.

Kwa upande wake hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Mbozi Mh Rahim Mushi ameeleza kuwa katika kipindi cha mwezi Disemba mwaka jana mahakama hiyo baada ya kubaini uwepo wa kesi nyingi ililazimika kuitisha kikao na wadau wa mahakama ambapo walikubaliana kumaliza kesi 100 kwa mwezi, hatua ambayo katika utekelezaji wake iliwezesha kupunguza kesi 107 mahakamani hapo.

Alisema ikiwa mahakama zitafanya kwa malengo na kujadiliana na wadau wao, basi ni dhahiri suala la utoaji haki mahakamani litatendeka pasipo malalamiko.
Akifafanua baadhi ya changamoto, Hakimu Mushi amesema,suala la upelelezi wa mashauri kuchukua muda mrefu, kutopatikana kwa mashahidi kwa wakati na kuchelewa kwa vielelezo muhimu hasa vinavyohusiana na vinasaba na tafsiri zake vimesababisha mahakama kulaumiwa mara nyingi licha ya changamoto hizo kuwa nje ya mikono yake
Kuhusu uchakavu wa baadhi ya majengo ya mahakama wilayani humo, Hakimu mfawidhi huyo amesema, hali imekuwa mbaya zaidi kwa mahakama za mwanzo Kamsamba, Tunduma na  Ndalambo ambako inafikia wakati hakimu hulazimika kuhama hama na meza yake huku mashauri yakiendelea mahakamani kutokana na kuvuja kwa mapaa yake kunakotokana na uchakavu.
Maaadhimisho hayo yamehudhuliwa na marafiki wamahakama wakiwemo viongozi wa dini ambao waliendesha maombezi na dua kwa watendakazi wa idara hiyo, jeshi la polisi, TAKUKURU, na vyombo vingine vya utoaji huduma.