Adverts

Apr 5, 2014

ZAMBI SASA AWA MUUMINI WA MBOLEA YA MINJINGU, AHIMIZA MASHAMBA DARASA KUELIMISHA WANANCHI


 Mh Zambi akionyeshwa namna vipandikizi vya miti vinavyooteshwa na mtafiti wa TACRI MBIMBA bwana Charles Mwingira wakati Naibu waziri huyo alipofanya ziara leo kwenye kituo cha utafiti wa kahawa Mbimba
Na Danny Tweve –Mbozi
Naibu waziri wa Kilimo na Ushirika Mh Godfrey Zambi hatimaye ameungana na watafiti kuunga mkono matumizi ya Mbolea ya Minjingu na kuwataka wananchi kuwa tayari kushiriki mashamba darasa yanayokusudiwa kufanywa kwenye maeneo ambayo mbole hiyo imekuwa ikilalamikiwa.
Akizungumza na watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi kabla ya kuanza ziara ya kikazi ya siku tatu wilayani humo , Mh Zambi amesema hatua hiyo haitokani na uteuzi wake kuhofia kutofautiana na serikali yake bali ni kutokana na matokeo ya utafiti ya kitaalamu yaliyowasilishwa na taasisi zinazoaminika
 Mh Zambi amesema licha ya kutafsiriwa kuwa ni mpinzani wa mbolea ya Minjingu, bado jukumu lake kubwa kama mtetezi wa wananchi ilikuwa ni kuisukuma serikali kusikiliza malalamiko ya wananchi na kwamba hatua ya sasa ya kuanzisha mashamba darasa italeta suluhu ya tatizo hilo.

Alisema ni dhahiri mbolea hiyo bado inalalamikiwa, lakini njia bora ni kutoa elimu kwa wananchi namna ya kuitumia na kwamba mkakati wa  majaribio zaidi kupitia mashamba darasa kwenye maeneo ambayo mbolea hiyo imeonyesha udhaifu utaweza kutoa matokeo bora badala ya malalamiko yasiyo na takwimu za kitaalamu.

Amesema juzi akiwa ziarani kutembelea kiwanda cha minjingu pia amekutana na malalamiko hayo hayo kwenye kijiji ambako kiwanda kimejengwa na kwamba  malalamiko pia  yamethibitishwa pia kupokelewa na uongozi wa kiwanda  juu ya matumizi ya mbolea ya minjingu mazao.
Hata hivyo amesema walichokubaliana na uongozi wa kiwanda hicho  kuanzisha mashamba darasa ya kutosha katika kila eneo linalolalamikiwa kuwepo utendaji usioridhisha wa mbolea hiyo.
Ameeleza kuwa awali uongozi wa kiwanda cha minjingu  walimweleza   wazi kuwa walikuwa na hofu juu yake baada ya kuteuliwa kwenye wizara ina uhusiano wa moja kwa moja na bidhaa yao, huku akiwa ni miongoni mwa wabunge waliokuwa misumari bungeni kwa kuwa na misimamo mikali kuhusiana na mbolea ya minjingu
Mh Zambi amesema tayari wameshapokea matokeo ya utafiti kutoka chuo Kikuu cha Kilimo SUA mbao wamethibitisha utendaji mzuri wa mbolea ya minjingu ikilinganishwa na Mbolea ya DAP inayopigiwa debe na wananchi wa wilaya ya Mbozi .
Amesema njia pekee ya kuwashawishi wananchi ni kuanzisha mashamba darasa  mengi kadiri iwezekanavyo ili kuthibitisha matumizi sahihi ya Mbolea hiyo  na kwamba changamoto za mbolea hiyo zitatatuliwa kupitia maonyesho hayo na kwamba ushirikiano baina ya serikali kuu,watafiti, kiwanda cha minjingu na halmashauri za wilaya
Kuhusiana na utaratibu wa utoaji wa pembejeo kwa njia ya ruzuku, Naibu waziri amesema kwa msimu ujao serikali haitatoa tena ruzuku kwa utaratibu wa vocha na badala yake pembejeo zitapitia vyama vya ushirika ambavyo sasa vitasimamiwa na sheria mpya ya mwaka 2013.
Amesema katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo ya utoaji ruzuku ya Mbolea kwa njia ya vocha jumla ya vocha zenye thamani ya shilingi Bilion 70 zimebainika kuibiwa ama kutumiwa kinyume na taratibu na kwamba kamati ya bunge ya Kilimo imemwagiza Mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za serikali kufanya ukaguzi ili hatua zichukuliwe

Amesema ni vyema halmashauri za wilaya kuanza kuwaandaa wananchi katika mfumo mpya wa kupata pembejeo ambao hautahusisha vocha na akawataka maafisa ushirika kujenga uwezo kwa vyama vya ushirika ili kuviandaa katika utoaji huduma hiyo.