May 3, 2009

HONGERA DOROTH MWANYIKA, MBOZI WANAKUKUMBUKA KWA KUSIMAMIA VYEMA TANZA KESHO

Rais aliwaapisha pia Makatibu tawala wa mkoa wa Mwanza Bi.Doroth Mwanyika na katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara Bwana Yusuf Athumani Matumbo. Bi Mwanyika anakumbukwa vyema na wananchi wa wilaya ya Mbozi kwa jinsi alivyoweza kusimamia mradi wa TANZA KESHO-ama CAPACITY 21 uliokuwa ukitekelezwa na halmashauri ya wilaya ya Mbozi kwa ushirikiano na UNDP. Utendaji wake unatajwa kuwa ndiyo mafanikio yaliyomwezesha kufanya kazi maeneo mbalimbali, ofisi ya katibu tawala mkoa wa mbeya, UNICEF na sasa huko kwenye ukatibu TAWALA. Picha kwa hisani ya Blog ya Mawasiliano Ikulu.

MBEYA PRESS YAPATA VIONGOZI WAPYA

Mwandishi wa TBC bwana NICO MWAIBALE jana aliibuka kwa ushindi wa kimbunga kuwa mwenyekiti wa chama cha wandishi wa habari mkoa wa mbeya. Katika uchaguzi huo ambao haukupata uwakilishi kutoka Umoja wa Vyama vya wandishi wa habari mikoani UTPC, ulifanyika kwa amani katika ukumbi wa chuo cha wafanyakazi Mbeya. Mwaibale ambaye katika nafasi ya uenyekiti alikuwa akishindana na mwenyekiti aliyemaliza muda wake bwana Christopher Nyenyembe, aliibuka na kura 26 dhidi ya 10 za Nyenyembe. Makamu mwenyekiti alichaguliwa Jane Lawa ambaye hata hivyo hakuhudhulia kwenye uchaguzi huo kwa kulamba kura 20 dhidi ya 15 za Richard Kilumbo. Katibu mkuu alichaguliwa Patrick Kossima (27) na kumshinda Kenneth Mwazembe (9), Katibu msaidizi alichaguliwa Merali Chawe kwa kura 31 za Ndiyo kati ya 36 zilizopigwa.(chawe hakuwa na mpinzani). Mweka hazina alichaguliwa Pendo Fundisha aliyepata kura 31 za Ndiyo na kura 3 za hapana baada ya kukosa mshinani, wajumbe wa kamati kuu walichaguliwa Danny Tweve aliyepita bila kupingwa baada ya kuwania nafasi hiyo peke yake. Wajumbe wengine katika kamati hiyo waliochaguliwa kwa kushindanishwa ni pamoja na Ester Macha, Sada Matiku. Kamati zingine waliochaguliwa ni Charles Mwakipesile(Nidhamu), Festo Sikagonamo (Mafunzo na Ujenzi) na Emanuel Simfukwe (Uchumi). Kwa uchaguzi huo Chama cha wandishi wa habari mkoa wa Mbeya kimetimiza masharti na maelekezo mapya ya UTPC kwa kila klabu kuwa na uwakilishi sawa kijinsia katika nafasi zote za maamuzi. Tunamshukuru bwana Christopher Nyenyembe kwa Uongozi wake kwa kipindi cha miaka 3 iliyopita ambapo ameiwezesha klabu kupata heshima ndani ya nchi kutokana na wanachama wake watatu akiwemo yeye mwenyewe kutwaa tuzo za uandishi bora wa habari za uchunguzi kwa miaka miwili.MBEYA PRESS CLUB >>> PEOPLE’S VOICE

WANDISHI MBEYA WASIKITISHWA NA VIFO VYA WENZAO

Mkutano mkuu wa Chama cha wandishi wa habari mkoani Mbeya, umepokea kwa masikitiko taarifa ya vifo vya wanachama wake 6 katika kipindi cha miaka 3 iliyopita. Kifo cha hivi karibuni ni cha Mhariri Mkuu wa Radio Uhuru Deogratius Kiduduye aliyefariki Lagos Nchini Nigeria alikoenda kwaajili ya maombi katika Kanisa la Synagogue church of All Nation linaloongozwa na Nabii Tb Joshua. Deo alikuwa mwanachama wa chama hicho hadi alipohamia jijini Dar es salaam kuchukua majukumu ya uhariri katika kituo cha Radio Uhuru, ambapo katika kipindi chote cha uhai wake amekuwa akitoa ushauri namna ya kuiendeleza klabu hiyo. Wanachama wengine waliofariki dunia ni pamoja na Niko Mwakatumbula, John Lubungo, Silvester Kikungwe, Rose Nkuba, Albano Wikedzi, Erasto Palick na Mariam Ngole ambao kwa pamoja wamefariki katika vipindi tofauti vya miaka mitatu ya uongozi uliomaliza muda wake hapo jana. Wanachama waliozungumza na blog hii wamesema katika jumuiya ya wanachama 60 kupotelewa na wanachama wake 8 ni jambo la kusikitisha na kumwomba mungu awatunze na kuwafikisha mahala salama marehemu wote hao. AMEN