Jul 22, 2016
MKUU WA WILAYA YA MBOZI AWATAKA MADIWANI KUWAFUATILIA WALENGWA WA TASAF
Mkuu wa wilaya ya Mbozi Bw. John Palingo amewataka madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Mbozi kufanya ufuatiliaji kwa walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini unaotekelezwa chini ya TASAF awamu ya tatu.
Akitoa salamu za serikali, Mkuu wa wilaya ya Mbozi amesema kuwa hatua hiyo itawarudisha kwenye mstari walengwa kutokana na kuwepo taarifa za matumizi mabaya ya fedha wanazonufaika kupitia mpango huo
Katika hatua hiyo amesisitiza kuwa hatua hiyo itasaidia kutekeleza azma ya mpango huo kufikiwa .
Katika hatua nyingine mkuu huyo wa wilaya ametangaza nia ya kurejesha na kuzifungua barabara za katikati ya mji wa Vwawa na kwamba kitaitishwa kikao cha wadau wa maendeleo mji wa Vwawa ili kujadili jambo hilo mchana wa leo ama kesho asubuhi ili hatimaye kufikia maamuzi ya pamoja ya namna bora ya uendelezaji wa huduma ya usafiri na uchukuzi mjini.
Polisi Songwe yaja na Ligi ya vijana msimu wa mavuno
Jeshi la Polisi kwa kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo wilayani Mbozi katika mkoa wa Songwe wanakusudia kuanzisha ligi ya vijana itakayoanza kulindima mwezi August, 2016
Akizungumza na mtandao huu, Mkuu wa polisi wilaya ya Mbozi Henry Kyssima amesema hatua hiyo inalenga kubaini vipaji vya vijana na hatimaye kutumia ligi hizo kuwaunganisha na timu mbalimbali zinazoanza ligi hivi karibuni
Ligi zinazokusudiwa kuwavizia wachezaji hao ni pamoja na zile za ligi kuu, daraja la kwanza na daraja la pili ambazo tayari kufuatia mwaliko huo kuna ugeni mkubwa ambao umeanza kuvinjali katika wilaya ya Mbozi na vitongoji vyake kwaajili ya kusaka vipaji hivyo
Kyssima amesema anatambua kuwa kipindi cha August kuna shughuli nyingi za kiuchumi zinazoendelea wilayani hivyo katika kuendesha ligi hiyo, itasaidia pia kutumia muda wa mapumziko katika michezo badala ya kuelekeza fedha na mapato yao kwenye matumizi ya dawa za kulevya na uhalifu
Amesema ligi hiyo itaendeshwa kwenye kanda tano na baadaye washindi wa kanda watakutanishwa hadi kupatikana kwa mshindi wa wilaya.