Jan 29, 2011

Cairo Kunawaka Moto!

Cairo Kunawaka Moto!: " Ndugu Zangu, JANA niliandika juu ya uwepo wa dalili za Cairo kuwaka moto Ijumaa ya leo mara baada ya swala ya Ijumaa. Na ndivyo ilivyokuwa. Miji ya Cairo, Suez, Alexandria na mingineyo inawaka moto. Waandaamanaji wameingia mitaani kudai mabadiliko. Wanataka Bunge livunjwe, Rais Hosni Mubarak na mwanawe Gamal waondoke Misri. Yale yale ya Tunisia. Naam. Kuna Mapinduzi yanayoongozwa na vijana kwenye Dunia ya Waarabu. ( The Arab World). Tumeona Tunisia. Kule Yemen moto bado unawaka. Na sasa Egypt. Hali si shwari. Vijana wako mstari wa mbele. Hosnu Mubarak amemrisha jeshi kuingia mitaani. Wananchi wamewashangilia wanajeshi. Kwamba idadi ya raia waliokufa mpaka sasa haizidi 20 inatoa tafsiri moja; kuwa jeshi huenda limeasi, maana imeripotiwa pia mapigano baina ya wanajeshi na polisi jijini Cairo. Jengo la Makao makuu ya Chama tawala, PDP liko katika hali ya majivu. Limechomwa moto na waandamani. Kiongozi wa upinzani Mohammed ElBaradei amezuiwa nyumbani kwake baada ya kujaribu kuingia mitaani. Barack Obama inaripotiwa hajapata mawasiliano na Hosni Mubarak. Kuna tahadhari kutoka Washington. Tamko rasmi la Washington kwa sasa ni ' Tuko Pamoja na Misri'. Ni dalili kuwa Marekani inaamini zama za Hosni Mubarak zinakaribia ukingoni. Marekani imeionya Serikali ya Misri isitumie nguvu kukabiliana na waandamanaji. Imetaka pia mawasiliano ya simu na internet yafunguliwe. Kwa sasa yamefungwa. Hosni Mubarak bado hajajitokeza kuongea na wananchi. Kauli yake inasubiriwa kwa hamu.
"