Zipo siku ambazo hapa BC huwa tunapenda kujikumbusha mambo mbalimbali yaliyojiri hapo zamani.Hapo ndipo huwa tunapata muda wa kujikumbusha miziki ya kale. Hapo ndipo tunapopenda kuwakumbuka mashujaa wetu ambao kupitia utumishi wao kwetu na kwa dunia kwa ujumla,leo hii tupo tulipo. Huwa ni wakati adimu kwetu tunapowakumbuka mashujaa wetu,walio hai na waliotangulia kwa Mola kwani ni watu kama hao ambao kwa kufanya kile walichokifanya,kwa kujitolea vile walivyojitolea,leo hii wanatufanya sote “tujisikie” na u-utanzania wetu.Kichwa mbele,mabega juu.
Katika mlolongo wa uchambuzi wetu huo,leo jina ambalo limetujia ni lile la John Stephen Akhwari. Kama ulizaliwa miaka ya hivi karibuni inawezekana kabisa ukawa hujawahi kulisikia jina la Akhwari. Siwezi kukulaumu.Bado hatuna mfumo mzuri wa kuwakumbuka na kuwaenzi mashujaa wetu ipasavyo.Tunahitaji kuunda mfumo huo.
John Stephen Akhwari ni mtu anayekumbukwa sana katika ulimwengu wa michezo hususani ile ya Olympic. Huyu bwana,alishiriki katika mchezo wa riadha akiiwakilisha Tanzania katika michezo ya Olympic iliyofanyikia nchini Mexico mwaka 1968.
Wakati akichuana,Akhwari alianguka na kuumia vibaya gotini. Madaktari wakamwendea na kumfunga bandeji huku wakidhani kwamba jamaa ndio amefikia mwisho wa mashindano na atajitoa. Mambo yalikuwa tofauti.Akhwari akasimama na kuendelea kukimbia. Bila shaka wauguzi wale na hata mashabiki waliomuona waliona jamaa wazimu ushampanda. Hakujali fikra za watu wengine.Alijua anachokifanya.
John Stephen Akhwari
Huku watu wakiwa washaanza kuondoka wakijua mambo yeshakwisha maana zaidi ya saa moja lilishapita tangu mshindi wa kwanza avuke kamba na giza likiwa lishaanza kuingia,Akhwari akatokea. Wa mwisho! Jumla ya washindani walikuwa 74 lakini waliofanikiwa kumaliza walikuwa 57 huku John Stephen Akhwari akichukua namba hiyo ya 57.
Walioshuhudia wakati mtanzania huyu jasiri akimalizia mbio, walishikwa na mshangao.Kwanini huyu bwana hakujitoa ingali ameumia namna hiyo na anajua fika kwamba nambari moja,mbili au tatu si zake? Waandishi wa habari wakamzunguka kutaka kujua. Huku akihema na kutokwa na jasho, Akhwari akawaambia waandishi…
Nchi yangu haikunituma kutoka umbali wa zaidi ya maili 500o kuja hapa kuanza tu mbio bali kumaliza.
Ingawa alishindwa,John Stephen Akhwari, akawa ametoa mfano mkubwa sio tu kwa wanamichezo bali watu wote.Unapoingia katika mashindano,yawe ni michezoni au katika maisha,huna budi kushindana mpaka mwisho. No quitting!
John Stephen Akhwari akionyesha jinsi ya kukimbia katika mojawapo ya matangazo ya kuhamasisha Olympic ya China mwaka 2008
Wakati wa mashindano ya Olympic mwaka 2008 yaliyofanyikia huko nchini China,jina lake lilivuma kwa mara nyingine.China ilimtumia katika mambo mbalimbali ya uhamasishaji wa Olympic. Pengine ndio maana walizoa medali nyingi namna ile.Who knows?
Heshima kwako John Stephen Akhwari. You taught us never to quit,but to make sure we finish.Thank You.
FINISH THE RACE-PERSONAL STORY OF COURAGE
Photo Credits: Crienglish
" indaba2010