Ndani ya kipindi cha takribani miaka 5 iliyopita, kumekuwa kukianzishwa Reality TV Shows mbalimbali nchini kwetu. Miongoni mwa shows hizo ni pamoja na ile ya Maisha Plus ambayo kwa kipindi kifupi tu tayari ilikuwa imejizolea mashabiki lukuki.Bila shaka mafanikio hayo yalitokana na ubunifu na uhalisia uliombatana na kipindi hicho.
Hata hivyo Maisha Plus ni kama vile imepotea ghafla.Kulikoni?Baada ya kupata maswali kadhaa toka kwa wasomaji mbalimbali na hususani mashabiki wa Maisha Plus,BC ilimtafuta Masoud Kipanya ambaye ndiye mwanzilishi na mratibu mkuu wa Maisha Plus ili kupata ufafanuzi kuhusu hatma ya kipindi hicho.Haya hapa mahojiano mafupi na Masoud Kipanya(KP)
BC: Kwa muda sasa tumekuwa tukipokea maswali kadhaa kuhusu Maisha Plus.Wengi wanataka kujua kulikoni mbona hawasikii chochote na muda wa audition ndio huu?Je mwaka huu kutakuwa na Maisha Plus au ndio basi tena?
KP: Asante kaka kwa kunitafuta ili kujua kinachoendelea. Hii inamaanisha kwamba unatujali na unapenda maendeleo yetu.Ni kweli watu wengi wamekuwa wakiulizia kulikoni. Kuna sababu kadhaa ambazo zimesababisha hali iliyopo ya kuchelewesha mambo kiasi kwamba watu wengine kuona kama vile Maisha Plus imekufa. Ukweli ni kwamba Maisha Plus haijafa.Bado ipo. Kuna mambo kadhaa ambayo yalijitokeza na ndio yanachangia ucheleweshwaji huu. Miongoni mwa mambo hayo kubwa zaidi ni namna season 2 ilivyokwenda.Nitafafanua;
Kwanza kabisa naweza kusema wenzetu wa TBC kwa kiasi fulani walituangusha ingawa nashindwa kuwalaumu moja kwa moja kwa sababu mpaka leo hawajapata nafasi ya kukaa nasi meza moja kujua what happened. Tunafahamu walikuwa bize na uchaguzi na hivi karibuni pamekuwa na mtikisiko wa kuondoka kwa DG wao.
Season 2 ilirushwa vibaya sana in terms of timings. Kuna siku kipindi kilikuwa kinarushwa saa 9 mchana, siku nyingine saa 12 jioni, saa 4 usiku na hata saa 6 usiku.Yaani hakukuwa na ‘consistence’. Na kwa kawaida kipindi cha redio au tv lazima watazamaji wajue time moja, kama itatokea dharura basi mabadiliko ya muda huweza kuvumiliwa mfano nyakati za bunge au kama kuna hotuba ya Rais nk.Hii ilichangia kwa kiasi kikubwa season 2 isitazamwe na watazamaji wengi.
Bahati mbaya kwetu hakukuwa na sababu za msingi zilizowekwa wazi. Najua wasomaji wako watajiuliza kuhusu mkataba wetu na TBC, kwa kuwa tulianza kwa kutumia fedha zetu za mifukoni kutokana na kutokuwa na sponsors, tulikubaliana kwa pamoja, sisi kama waandaaji dmb Co.Ltd na TBC kukibeba kipindi kama wanavyofanya wengine mpaka kitakapochanganya na kuanza kuvuta mashabiki ambao ndio husababisha wadhamini kuingia.
Jukumu lao kwa mujibu wa mkataba wetu lilikuwa kurusha kipindi kwa wakati na sisi tulibeba jukumu la kutengeneza kipindi na gharama zake.
Lazima ieleweke, na najua kwa wasomaji wako wenye damu ya ujasiriamali watakuwa wanaelewa hili, kwamba mafanikio huwa hayaji bila ya kupitia hatua ngumu za maumivu na hasara. Pakikosekana uvumilivu, unaweza kuacha.
Kwetu pia tulitaraji tungeumia hata kwa seasons 4 huku tukitoa pesa zetu mifukoni. Kwa faida ya wasomaji wako, season 1 tulitumia karibu TZS 40 million kwa production, season 2 tulitumia karibu 56M.
Nimeyaweka haya bayana kwa niaba ya kampuni kwa sababu tulianzisha Maisha Plus kwa ajili ya watazamaji na ndo maana tumeweza kujibana na kutumia pesa zote hizo bila ya kuhisi maumivu, kwetu furaha tuliyoipata ni namna ilivyopokelewa.
BC: Kwa hiyo mna mkakati gani hivi sasa ili kuhakikisha mashabiki wenu na bila shaka vijana ambao wangependa kushiriki katika Maisha Plus,wanapata fursa hiyo?
KP: Mkakati uliopo ni kuwasubiri wenzetu wa TBC wakishajipanga kiuongozi tukae nao tuone kama watakuwa tayari kuendelea na mtoto wetu Maisha Plus katika mtindo ambao utakuwa na consistence.Endapo wataonyesha shaka basi tutajaribu mazungumzo na TV stations nyinginezo, na endapo patakuwa na mashaka basi tutalifungia wazo letu kabatini.
Kwa sisi tuliotengeneza, season 2, laiti watu wangeiona kwa ukamilifu wake, ilikuwa na improvements kubwa zaidi ya season 1.
Ni matumaini yetu kuwa mambo yatakaa sawa ili 2011 ianze na mchakato wa 3 wa Maisha Plus InshaAllah.
BC: Shukrani Masoud…kila la kheri.
" indaba2010