Jan 30, 2011

MAREKANI YAIMWAGIA TANZANIA DOLA MILIONI MBILI KWA AJILI YA MRADI WA KILIMO.

MAREKANI YAIMWAGIA TANZANIA DOLA MILIONI MBILI KWA AJILI YA MRADI WA KILIMO.: "
Serikali ya Marekani ya Rais Barack Obama jana, Ijumaa, Januari 28, 2011, ilitangaza kuwa inatoa kiasi cha dola za Marekani milioni mbili (sawa na zaidi ya sh bilioni mbili) kwa ajili ya kuanzisha mfuko wa uwezeshaji wa Mradi wa Uendelezaji Kilimo Kusini mwa Tanzania wa Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT).

Hatua hiyo ya Serikali ya Marekani ambayo kwa pamoja na Serikali za Tanzania na Vietnam inasaidia kusukuma utekelezaji wa mipango mipya ya kuboresha kilimo katika Tanzania na Vietnam, chini ya visheni mpya ya “A New Vision for Agriculture”, ni moja ya hatua nyingi zilizochukuliwa na Serikali hiyo kuunga mkono jitihada za Tanzania kufanikisha Mradi huo.

Mchango huo mkubwa wa Marekani ulitangazwa jana na Mtendaji Mkuu na Mtawala wa Mfuko wa Misaada ya Maendeleo ya Kimataifa wa Marekani (USAID) Dkt. Rajiv Shah wakati alipoungana na Rais Jakaya Mrisho Kikwete katika kuutangaza Mradi huo kwenye mkutano wa kimataifa wa waandishi wa habari mjini Davos, Uswisi.

Katika mkutano huo wa waandishi wa habari ambako Dr. Shah pamoja na viongozi wengine wakuu wa mashirika makuu ya kibiashara 17 duniani wanaoshiriki katika utekelezaji wa Mradi huo waliunga na Rais Kikwete, kiongozi huyo wa USAID alitangaza:

“Tunakushukuru Rais Kikwete kwa kutushirikisha katika mkutano huu wa kwako na waandishi wa habari hasa wakati huo ambako bei za vyakula duniani zinaonyesha dalili za kuanza kupanda tena. Marekani inayo kila dhamira ya kuunga mkono Mradi huu ili uweze kufanikiwa na kufikia malengo yake,” alisema Dkt. Shah na kuongeza:

“Ili kuonyesha dhamira ya Serikali ya Marekani katika kuunga mkono Mradi huu, ninayo furaha ya kutangaza mchango wa nyongeza wa Marekani katika mfuko wa uwezeshaji wa Mradi huu wa kiasi cha dola za Marekani milioni mbili.”

Tanzania inahitaji kiasi cha dola za Marekani milioni 50 kama mfuko wa kuanzisha SAGCOT ambayo uwekezaji wake unatarajiwa kufikia kiasi cha sola za Marekani bilioni 3.4 katika miaka 20 ijayo. Mradi huo unatarajiwa kutekelezwa katika mkoa ongozi katika kilimo cha chakila ambayo ni Morogoro, Iringa, Mbeya, Rukwa na Ruvuma.

Mshiriki mwingine kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, Hugh Grant ambaye ni Mwenyekiti, Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Mansanto ya Marekani inayojihusisha na kilimo duniani alisema kuwa mpango huo wa kilimo katika Tanzania na Vietnam utatumia mbegu za asili katika nchi hizo na siyo mbegu zilizotengenezwa kisayansi za GMO.

“Kwa sasa mipango yetu ni kutumia mbegu za jadi katika nchi hizo mbili – mbegu za asili, mbegu safi, mbegu zinazoweza kuhimili magonjwa na wadudu katika nchi hizi mbili. Hizi ndiyo mbegu zinazoweza kuwa za maana katika Mradi huu.“ Grant aliwaambia waandishi wa habari.

Kuhusu uwezekano wa makampuni 17 ya kimataifa yanayoshiriki katika kufanikisha Mradi huu kupanga bei za mazao yatakayozalishwa chini ya Mradi huu, Rais Kikwete aliwaambia waandishi wa habari:

“Kiasi kikubwa cha mazao kitakachozalishwa chini ya Mradi huu kitakuwa kwa ajili ya kuhakikisha kuwa Watanzania wanapata chakula cha kutosha. Kama kuna ziada, basi bei za mazao hayo ya ziada, zitaamuliwa na kiwango cha bei kwenye soko la kimataifa.”

Naye Paul Polman, Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Unilever katika Uingereza alisema kuwa mazao yatayozaliwa katika Tanzania chini ya Mradi huu yatakuwa na soko kubwa ndani na nje ya Tanzania.

“Kuna mahitaji makubwa ya chakula duniani. Baadhi ya watu wanaishi kwa kutegemea kiasi kisichofikia dola moja ya Marekani kwa siku. Kuna watu wanatumia kiasi cha asilimia 70 ama 80 cha kipato chao kununua chakula. Lazima dunia izalishe chakula zaidi kwa sababu dunia isiyokuwa na chakula cha kutosha itakuwa ni dunia isiyokalika.”

Baada ya mkutano huo na waandishi wa habari wa kimataifa, Rais Kikwete alikutana na kuwa na mazungumzo na Mtoto wa Malkia wa Uingereza, Prince Andrew ambaye ni mwakilishi maalum wa Uingereza kuhusu masuala ya biashara ya kimataifa na uwekezaji.

Katika mkutano huo, viongozi hao wawili walizungumzia nafasi za Uingereza kuwekeza katika Tanzania na jinsi Tanzania inavyoweza kuwekeza katika uchumi wa Uingereza kama inataka na inao uwezo huo.

Baadaye jioni ya jana, Rais Kikwete alikutana na Waziri Mkuu wa Norway, Mheshimiwa Jens Stoltenberg na pia kukutana na Bwana na Bibi Bergman ambao wamekuwa wasaidia huduma za afya katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na hasa Kitengo cha Tiba ya Meno.

Kabla ya kuondoka mjini Davos kwenda Addis Ababa, Ethiopia leo kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika, Rais Kikwete alikuwa na mfululizo wa mikutano kwenye Hoteli ya Sheraton ya mjini Davos alipokuwa amefikia.

Rais Kikwete amekutana na Mkurugenzi Mtendaji wa Accenture Development Partnership, Bwana Gib Bulloch kujadili jinsi gani teknolojia ya kisasa ya habari inavyoweza kutumika katika ufundishaji wa masomo katika shule za Tanzania.

Rais pia amekutana na kuzungumza na Bwana John Davies, Makamu wa Rais wa Kampuni ya Kimataifa ya Intel anayeshughulikia na masoko na pia amekutana na Dkt. Nkosana Moyo, Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kuzungumzia jinsi gani benki hiyo inavyoweza kuchangia maendeleo ya SAGCOT.

Rais Kikwete pia amekutana na kufanya mazungumzo na Bwana Richard T Clark, Mwenyekiti wa Kampuni ya Kimataifa ya Dawa ya Merck ambako mazungumzo yaliyohusu kuhusu maandalizi ya kupatikana kwa dawa ya kuwezesha chanjo ya kinga la kansa ya shingo ya kizazi dhidi ya akinamama wa Tanzania iliyopangwa kuanza mwaka ujao.

"