Jan 31, 2011

Meya CCM abwanga manyanga

Meya CCM abwanga manyanga: "
Meya CCM abwanga manyanga Sunday, 30 January 2011 21:22 Mussa Mwangoka, Sumbawanga MEYA wa Manispaa ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, Samweli Kisabwiti kupitia CCM ametangaza kujiuzulu wadhifa wake, zikiwa zimepita siku 45 tu tangu alipochaguliwa kushika nafasi hiyo. Hatua ya hiyo ya Meya Kisabwiti imekuja siku chache tangu naibu meya wa jiji la Arusha, Michael Kivuyo kujiuzulu wadhifa wake kufuatia mchafuko yaliyosababisha damu kumwagika wakati polisi waluipopambana na waandamanaji wa Chadema. Kwa upande wake Kisabwiti alijiuzulu kwa kile kinachosemekana ni ubatili wa matokeo ya kura yaliyofanyika mjini hapo Desemba 18, mwezi uliopita. Alisema amechukua fursa hiyo kulinda heshima yake binafsi na ya chama chake, baada ya kuandamwa kuwa ana elimu duni. Meya Kisabwiti amedumu kwenye nafasi hiyo kwa mwezi mmoja na nusu tangu alipochaguliwa kushika nafasi hiyo Desemba 17, mwaka jana ambapo alikuwa mgombea pekee baada ya mgombea wa Chadema kujitoa. Alishinda kwa kupigiwa kura za ndiyo na hapana, ambapo kura 12 zilimkubali na kura 9 kumkataa. Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga ina jumla ya madiwani 21 kati ya hao 16 ni wa CCM, wanne wa Chadema na mmoja ni diwani kupitia tiketi ya DP. Hii inamaanisha kwamba miongoni mwa waliopiga kura za hapana ni madiwani wa CCM. Akizungumza na waandishi wa habari jana nyumbani kwake mjini Sumbawanga, alisema amefikia uamuzi huo baada ya kung’amua kwamba uongozi katika nafasi kubwa kama meya ni kitu muhimu sana katika kufanya kazi kwa ufanisi na hivyo anahitaji muda wa kutosha ili aweze kujifunza. "Kwahiyo nimeona nipate muda wa kujifunza na kupata uzoefu kupitia nafasi yangu ya udiwani wa kata ya Katandala na kupitia vikao mbalimbali hivyo basi nivema nikaachia ngazi ili kutoa nafasi kwa wengine wenye uzoefu kwani nafasi hiyo ni nyeti sana na inahitaji uzoefu na elimu ya kutosha,’’alisema. Kwa mujibu wa Meya huyo alisema tayari amekwishamuandikia barua mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga kumueleza uamuzi wake wa kujiuzulu na kwamba ofisi ya Mkurugenzi imepokea barua hiyo rasmi Januari 28 mwaka huu. Aliongeza kusema kuwa pia amepeleleka nakala ya barua hiyo kwa taarifa kwa Katibu wa CCM wa Taifa, Katibu wa CCM wa mkoa wa Rukwa na katibu wa CCM wa wilaya ya Sumbawanga. Alisema amefikia uamuzi huo kwa hiari yake mwenyewe bila kupata shinikizo lolote kutoka sehemu yeyote ile isipokuwa aliendela kusisitiza kuwa amefanya hivyo kwa kuendelea kulinda heshima yake binafsi na chama chake kutokan na maneno mengi yaliyozagaa mjini Sumbawanga kwamba hana sifa ya kuwa kiongozi wa siasa. Alisema awali alipopata nafasi ya udiwani alikubalika lakini baada ya kugombea na kushinda nafasi ya umeya wa Manispaa hiyo ndipo yalipoanza kuibuka maneno na tuhuma mbalimbali kwamba yeye hana elimu ya kutosha ya kumwezesha kushika nafasi hiyo nyeti. Meya huyo alisema kutokana na maneno yaliyozagaa mjini hapa yeye binafsi siyo rahisi kuendelea kuliongoza baraza la madiwani ambalo nalo kuna baadhi ya madiwani hawamkubali na kumwona kuwa ana haja ya kusoma na hivyo wanaona ni bora aachie ngazi hiyo ili apatikane msomi wa kuwaongoza tofauti na yeye ambaye ana elimu ya shule ya msingi darasa la saba. “Awali ya yote kusudio langu kubwa lilikuwa kujiuzulu kuanzia nafasi ya udiwani hadi umeya lakini rafiki zangu wa karibu na wanachama wa chama changu walinisihi nijiuzulu nafasi ya umeya kwani kama ningejiuzulu na udiwani ingelazimu uchaguzi mdogo ufanyike kitendo ambacho huenda CCM ingeipoteza kata hiyo,"alisisistiza. Akifafanua alisema "Pamoja na kuandika barua ya kujiuzulu endapo chama changu kikisita kunikubalia siwezi kubadili uamuzi huu nilioufikia wa kujiuzulu nafasi hiyo,”alisema. Alieleza kuwa changamoto alizozipata kwa kipindi cha mwezi mmoja na nusu akiwa meya ni pamoja na kukosa usingizi na kwamba hata biashara zake zimedorora kwa kiasi cha kutisha. Meya huyo ambaye anamiliki maduka kadhaa ya nyama mjini, hapa alikiri kuwa nafasi hiyo sio tu ni nyeti bali pia ni dhahabu kwamba kama angekuwa hana pengine pa kushikia asingeweza kuthubutu kujiuzulu. Naye Mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Sumbawanga mjini Charles Kabanga alipohojiwa alidai kuwa yeye binafsi kama ofisi hawajazipata rasmi taarifa yake hiyo ya kujiuzulu lakini alisema Meya huyo ana hiari ya kufanya hivyo na iwapo itatokea basi chama CCM kitafuata taratibu na atapatikana Meya mwingine kuziba pengo hilo . Aliongeza kuwa kujiuzulu kwa Meya huyo hakutakiathiri chama chao kisiasa kwa sababu kama kiongozi anaona nafasi imemshinda au ameshindwa kuimudu ni bora awajibike ili kutoa fursa kwa wengine wenye uwezo kuliko kuendelea na hatimaye kuharibu.
"