Jan 29, 2011

Mradi mkubwa zaidi wa kilimo (SAGCOT)kubuniwa na kuanzishwa katika Tanzania .

Mradi mkubwa zaidi wa kilimo (SAGCOT)kubuniwa na kuanzishwa katika Tanzania .: "

MRADI mkubwa zaidi wa kilimo kubuniwa na kuanzishwa katika Tanzania wa Southern Agricutural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT) umezinduliwa kwenye ngazi ya kimataifa leo, Ijumaa, Januari 28, 2011, kwenye moja ya vikao vya Mkutano wa Uchumi Duniani (WEF) mwaka huu, mjini Davos, Uswisi.

Mradi huo umezinduliwa kwenye mkutano ulioandaliwa kwenye hema la Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WHO) katika shughuli iliyohudhuriwa na watendaji wakuu wa makapuni 17 yanayounga mkono mradi huo kwa njia mbali mbali na viongozi wengine duniani.

Rais Kikwete alikuwa mmoja wa wazungumzaji kwenye mkutano huo ambako mzungumzaji mkuu alikuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Mheshimiwa Ban Ki Moon na kuhudhuriwa na watu mbali mbali mashuhuri duniani akiwamo Mheshimiwa Kofi Annan, aliyekuwa katibu mkuu wa UN.

Mradi huo wa Tanzania umeanzishwa kwa pamoja na mradi mwingine kama huo katika Vietman, nchi mbili zilizochaguliwa duniani kutekeleza miradi ya mfano wa kilimo yenye lengo la kupunguza umasikini, kujenga uwezo wa kupambana na njaa, na kuleta usalama wa chakula kitaifa na kimataifa.

Mbali na Serikali za Tanzania na Vietnam, Serikali nyingine inayoshiriki moja kwa moja katika kufanikisha mradi huo ni Serikali ya Marekani ambayo katika mikutano ya hapa imekuwa inawakilishwa na Mtawala wa Shirika la Maendeleo la Marekani (USAID), Dkt. Rajiv Shah.

SAGCOT ambao utatekelezwa kwa njia ya ushirikiano wa sekta za umma na binafsi, unalenga pia kuongeza uzalishaji wa chakula na faida kwa mkulima mdogo kwa kufanya mageuzi makubwa katika jinsi mkulima mdogo anavyoendesha kilimo chake na kumwezesha kutumia zana za kisasa katika shughuli zake za kilimo.

Mradi huo kwa nchi zote mbili za Tanzania na Vietnam umezinduliwa katika kikao ambacho mada yake ilikuwa ‘Leveraging Public-Private Investment to Achieve a New Vision for Agriculure” (Jinsi ya Kutumia Uwekezaji wa ushirikiano wa Sekta ya Umma na Binafsi Kujenga Visheni Mpya kwa Ajili ya Kilimo).

Mara baada ya uzinduzi rasmi, kazi ilimwangukia Rais Kikwete kuupigia debe mradi huo siku yote nzima katika mikutano mbali mbali aliyohudhuria mjini Davos. Mikutano hiyo ilikuwa ni pamoja na kwenye chakula cha mchana cha viongozi wa nchi mbali mbali wanaohudhuria mkutano huo ambako mada yake ilikuwa “ Towards a New Growth Model.”

Mkutano wa mwaka huu umevutia kiasi cha viongozi wa nchi na Serikali kutoka nchi 38 na viongozi wengi maarufu wa zamani akiwamo Rais Bill Clinton wa Marekani na Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza, Tony Blair wa Uingereza.

Afrika inawakilishwa na nchi tatu tu – Tanzania, Afrika Kusini, Zimbabwe na Ethiopia. Tanzania imewakilishwa na Rais Kikwete, Afrika Kusini imewakilishwa na Rais Jacob Zuma, Zimbabwe na Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai na Ethiopia na Waziri Mkuu Meles Zenawi.

Baadaye, Rais Kikwete aliendelea kuuza mradi huo wa SAGCOT kwenye mkutano wa jumla ambako yeye pamoja na viongozi na wataalamu wengine walijadili mada iitwayo: “Genuine Green Growth: Development through Agriculture”

Jioni, Rais Kikwete aliongoza viongozi na watalaam wengine kuhutubia mkutano wa waandishi wa habari kuzungumzia SAGCOT.

Utekelezaji wake utashirikisha, kwa mara ya kwanza katika jitihada za maendeleo duniani, wadau wote wa sekta ya kilimo yaani wakulima wadogo, wakulima wakubwa, wafanyabiashara na sekta binafsi, sekta ya umma, Serikali na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali ambayo yanahusika na kilimo.

Mradi huo utakaotekelezwa katika mikoa ya Tanzania inayozalisha chakula kwa wingi ukiwamo Morogoro, Iringa, Mbeya na Rukwa utashirikisha baadhi ya mbinu ambazo zimekuwa zikitumiwa katika kutekeleza miradi mingine ya kilimo nchini kama vile Agricultural Sector Development Programme (ASDP) na Kilimo Kwanza.

Mradi wa SAGCOT ni matokeo ya uamuzi uliochukuliwa wakati wa Mkutano wa WEF-Africa uliofanyika Mei mwaka jana mjini Dar es Salaam na kabla ya hapo dhana ya uanzishwaji wa maeneo (corridors) ya kilimo iliyobuniwa na kupitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UN) iliyopitishwa mwaka 2008. Ni dhana hiyo ya UN iliyopelekea kuanzishwa kwa Beira Corridor Initiative katika Mozambique.

Kiasi cha dola za Marekani bilioni 3.4 zitatumika kuwekeza katika Mradi wa SAGCOT – ikiwa ni wastani wa kiasi cha dola za Marekani milioni 175 – kila mwaka kwa miaka 20 ijayo.

Inabashiriwa kuwa ifikapo mwaka 2030 kiasi cha hekta 350,000 zitakuwa chini ya kilimo cha kisasa, nyingi kati ya hekta hizo zikiwa mikononi mwa wakulima wadogo na sehemu kubwa ya eneo hilo ikiwa inalimwa kwa kumwagiliwa.

Inatarajiwa kuwa baada ya kuwekeza kiasi hicho cha dola bilioni 3.4, mradi huo utaweza kuwa na mapato ya kiasi cha dola za Kimarakeni bilioni 1.3 kila mwaka, utaweza kuajiri kiasi cha watu 420,000 na kuweza kuwatoa kiasi cha watu milioni 2.3 kwenye umasikini.

Lengo ni kuhakikisha kuwa kwa kadri mradi huo unavyoonyesha mafanikio, mradi wa namna hiyo unaanza kusambazwa katika sehemu nyingine nchini na katika nchi nyingine masikini zinazoendelea.
"