Jan 29, 2011

Msuya: Kuna Uwezekano CCM Kung'olewa

Msuya: Kuna Uwezekano CCM Kung'olewa: " WAZIRI Mkuu na Makamu wa Kwanza wa Rais, Bw. Cleopa Msuya amesema kwa jinsi vuguvugu la kisiasa lilivyo kwa sasa nchini, si ajabu chama kingine tofauti na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuchukua hatamu za kuongoza serikali. Mbali na hilo, Bw. Msuya (80) amesema ni wazi kama hatua za dhati hazitachukuliwa kuweka mfumo mzuri wa kutatua matatizo ya wananchi, hususan vijana, hali kama iliyotokea nchini Tunisia na katika nchi nyingine za Misri, Algeria na Ivory Coast, inaweza kutokea Tanzania. Lakini ameonesha matumaini kuwa mjadala wa katiba mpya ambao Serikali ya Rais Jakaya Kikwete imeuridhia, utasaidia hali kama hiyo isitokee kwani baadhi ya mifumo inayoweza kuepusha itajadiliwa kwa kina na hata kuwekwa katika katiba, kwa manufaa ya Watanzania. Kwa mujibu wa Bw. Msuya, katika mjadala unaonedelea nchini juu ya katiba mpya, ni vyema ikafikiriwa kama kuna haja ya kuendelea kuwa na bunge moja, huku yeye akipendekeza kuwapo wa mabunge mawili, kama ilivyo nchini Uingereza. Mzee Msuya aliyasema hayo juzi, alipofanya mahojiano maalum na magazeti ya Kampuni ya Business Times Ltd, inayochapisha Majira, Business Times, Dar Leo na Spoti Starehe, nyumbani kwake jijini Dar es Salaam. Akionekana kufurahishwa na namna Watanzania wengi wanavyoonesha utayari wa kutafuta maisha, alisema hiyo ni changamoto kwa serikali kwani inao wajibu wa kuonesha njia sahihi na kuweka mazingira bora ya wananchi wake kutumia fursa nyingi zilizopo. Pamoja na kuisifia serikali katika baadhi ya maeneo, huku akionesha imani kuwa inaweza kurekebisha ili kulikwamua taifa hasa kwa kutumia fursa anuai ambazo Tanzania imebarikiwa kuwa nazo, Bw. Msuya alionekana kushangazwa na kusuasua kwa ushughulikiaji wa mambo muhimu kiasi cha kuzua minong'ono kwamba 'kuna mkono wa mtu hapo.' Maendeleo yatokane na vipaumbele Mzee Msuya alisema kuwa Tanzania ina kila kitu kinachoweza kuifanya nchi yoyote kuendelea kiuchumi, akisema 'kwa mfano kwa nini tusiwe Qatar ya Afika Mashariki kwa kuzalisha gesi na kuweza kuuza gesi yetu ya asili kwa majirani. Mwalimu alisema kupanga ni kuchagua.' Akifafanua suala la umuhimu wa vipaumbele katika kuiwezesha nchi kuendelea, Bw. Msuya alisema kuwa haiwezekani maendeleo kupatikana kwa kufanya kila kitu kwa wakati mmoja. 'Unajua masuala ya maendeleo you need (unahitaji) kupanga, Mwalimu (Nyerere) alikuwa akisema kupanga ni kuchagua...ukijaribu kufanya kila kitu kwa wakati mmoja huwezi, lazima uwe na specific (malengo) target on some issues. Nitawapatia mfano... 'Kuna wakati baada ya uhuru serikali iliamua kutumia fursa za kiuchumi kwa majirani zetu, ndani ya muda fulani tukaamua kujenga reli ya TAZARA kwenda Zambia kwa msaada wa Wachina, tukajenga barabara ya lami kwenda huko mikoa ya kusini na tukajenga bomba la mafuta, TAZAMA, ilikuwa ni mipango ndani ya muda fulani, mnaacha mengine mna-concetrate. 'You have to select priorities (lazima uwe na vipaumbele). Imekuwa ikiniuma sana mimi, lakini ni changamoto, maana sasa tunazo raslimali zaidi kuliko tulivyokuwa wakati ule, tunao watu, lakini results (matunda) hayaonekani, sisi sio landrocked kama walivyo baadhi ya majirani zetu, sisi si nusu jangwa kama kama Kenya kwa mfano. Huku akinukuu maneno ya Balozi wa Ujerumani, Bw. Guido Hertz, ambaye aliwahi kuhojiwa na gazeti moja nchini na kuonesha mshangao juu ya umaskini uliokithiri wa Watanzania pamoja na utajiri wa raslimali zilizopo, akisema 'ni vigumu kuelewa wala kuielezea hali hii,' Mzee Msuya aliongeza; 'Tuna kila kitu kinachohitajika...kuna haja ya kujitazama upya, tuna raslimali za kila aina zikiwemo za asili, are we putting them on the best use (tunazitumia inavyostahili ?)...tuna gesi ya asili, tuna akiba ya kutosha ya dhahabu, utalii pia...kuna hili ka kilimo kwanza, serikali imeshatamka ingawa kwa kuchelewa kidogo. 'Lakini nalo hatujalianza vizuri (la kilimo kwanza) kwa sababu hiyo hiyo ya kutopanga na kukosa vipaumbele...viwanda ni muhimu, suala la umeme ni critical (tatizo sugu) sasa lakini kuna possibilities (uwezekano) wa kugeuza coal (makaa ya mawe), umeme wa upepo na ule wa Rufiji ambao unazidi hata mahitaji yetu,' alisema na kuongeza. 'Kinachotakiwa ni vipaumbele...sasa tuna raslimali watu ambazo zina ujuzi, maarifa na mafunzo. Suala la infrastructure (miundombinu)...ingawa serikali imejitahidi katika hili kwa kujenga barabara nyingi, lakini kuna tatizo la usafiri wa reli. Kuna kila haja ya kushughulikia reli ya kati, TAZARA na reli ya Tanga. 'Tujenge hizo ili mizigo kutoka bandarini isafirishwe, nasikia sasa wanajenga bandari sijui wapi, nyingine ya nchi kavu hapa...suala si kujenga bandari za nchi kavu, muhimu ni kujenga reli ili tuweze kuzifikia nchi jirani...ni changamoto ya kuanza kwa kutumia fursa zote hizo. 'Mimi nafurahi sana siku hizi unawaona Watanzania wanahangaika huku na huko, kila ukipita...hata hii ya machinga ni namna gani wananchi wanajitahidi, tunapaswa kuiona hiyo kama changamoto si laana, maana yake ni kuwa wananchi wako tayari kwa mabadiliko ya haraka, serikali inapaswa kusaidia hapo. 'Tufufue miundombinu yetu, hasa reli, spirit (ari) ya ujenzi wa barabara iliyopo sasa iendelezwe...concetrate on few key issues (kujikita katika mambo machache ya msingi) lazima tujue hilo...lazima tujue tunaondoka vipi kwenda mbele baada ya miaka 50 ya uhuru,' alisema Bw. Msuya, ambaye pamoja na umri wa miaka 80 bado anaonekana kuwa na nguvu. Akijibu swali juu ya ukuaji wa uchumi kitakwimu na kuongezeka kwa umaskini miongoni mwa wananchi walio wengi, alisema pamoja na kuwa serikali haiwezi kuwawekea watu fedha mfukoni, isipokuwa mpaka wanapojishughulisha kwa ajili ya kujipatia kipato, serikali inapaswa kuweka mazingira maridhawa ya shughuli hizo. Alisema ni watu wachache wanaoweza kupata ajira rasmi za ofisini katika sekta ya umma na binafsi, kwani wengi wa Watanzania wanapata ajira katika kilimo, lakini tatizo limekuwa ni bei ndogo. 'Katika kilimo watu wetu wanajishughulisha kweli, lakini tatizo limekuwa ni bei ndogo, ukiulizia tatizo ni nini utakuta ni gharama za usafiri, tunahitaji kwenda kwa kasi...ndiyo maana nikasema masuala ya miundombinu ya uchukuzi ni muhimu. 'Kwa mfano hakuna haja ya soko kuwa Dar es Salaam tu, kila mkulima aje kupata soko hapa, mkulima aliyeko Rukwa anaweza kuuza nje ya nchi Zambia huko,' alisema Mzee Msuya. Akizungumzia juu ya mazingira ya uwekezaji nchini, alisema kuwa ni mazuri lakini kuna kila haja ya kujikita na kuweka kipaumbele katika miundombinu ya reli na bandari na upatikanaji wa umeme wa uhakika na rahisi, sambamba na mawasiliano ya elektroniki, ili kujiongezea uhakika na uwekezaji. Alisema hata jiografia ya Tanzania ni fursa ya kipekee inayoweza kutumiwa na nchi kunufaika kiuchumi kwani inazungukwa na nchi nane, ambazo nyingine hazina bahari wala ziwa, hivyo kutokuwa na bandari, hali ambayo inazifanya kutegemea nchi jirani kama Tanzania. 'Miaka 30 iliyopita Dubai haikuwa lolote, it was just a small..., lakini wameibadilisha kuwa moja ya miji mikubwa kama Singapore. Miaka 50 ijayo Tanzania inao uwezo kabisa wa kuwa nchi yenye uchumi wa kati, tunaweza kuweka malengo ya kuwa kama Korea Kusini, hata kama hatutawafikia kabisa, lakini tunaweza. Mjadala wa katiba mpya Katika suala la katiba mpya, Mzee Msuya alisema kuwa kuna kila haja ya vyombo vya utendaji kazi hasa vile vya kisheria kufanyiwa mabadiliko ili vifanye kazi inavyopaswa. Pia alisema ni wakati mwafaka katika mjadala wa katiba mpya, Watanzania waanze kufikiria iwapo kuna haja ya kuendelea kuwa na bunge moja, huku yeye akionea mfumo wa mabunge mawili, ndiyo unafaa kwa sasa nchini kutokana na wabunge kupatikana kutoka katika makundi mbalimbali ya kijamii nchini. 'Sasa hata wasomi wanakimbilia kwenye siasa...tunao wabunge wanatokana na NGO sijui wapi huko, hivyo ni vyema watu wakafikiria hilo. (Chanzo: Gazeti Majira)
"