Feb 27, 2011

Uvumilivu una mipaka yake!

`Mfanyakazi huyu anatafutwa na muajiri wake, kwa kushukiwa kutoroka na mamilioni ya hela, zawadi nono itatolewa kwa yoyote atakayetoa taarifa wapi alipo….’ Sikuweza kuendelea kusoma yale maelezo, kwani macho yangu yalivutika kuiangalia ile picha ya mtuhumiwa. Nilipikicha macho kuhakikisha kuwa kweli huyu ninayemuona kwenye picha ndio yeye kweli, yule jamaa ninayemfahamu au ni kufanana kwa sura, kwani dunia hii ni wawiliwawili. Na wakati nakodoa macho kuiangalia vyema ile picha, simu yangu ya kiganjani ikaita ‘Halloh, mkuu umeona gazeti la leo la habari, lina picha ya rafiki yako, anatafutwa na polisi…’ simu ikaendelea kuelezea, lakini mimi nikawa nimezama kwenye, na kukumbuka enzi wakati nasoma na huyu jamaa. Alikuwa mpole, alikuwa hapendi vurugu, alikuwa mtu ambaye kila mtu alimwamini kwa tabia na utendaji wake... Nakumbuka kuna kipindi kulitokea mgomo, jamaa huyu hakujihusisha kabisa, na alipewa zawadi ya nidhamu. Kipindi nipo nafanya kazi na yeye kabla fagio la walalahoi halijapitishwa na kunikumba mimi na wenzangu, ambao tunadau haki yetu mahakamani hadi leo tuliwahi kufanya mgomo, kushinikiza malipo bora ya wafanyakazi, jamaa huyu hakujiunga kweny emgomo huo, na ndicho kilichomfanya aendelee kuwepo kazini hadi tulipoona hili tangazo kuwa `anatafutwa na mwajiri wake, kwa kupitia polisi kwa kutoweka na mamilioni ya hela, tena za kigeni! ‘Bwana mimi nampa mkono wa hongera jamaa yetu huyu, najua wizi ni mbaya lakini kwake yeye kachukua haki yake aliyodhulumiwa..hajaiba, sisi tuliojifanya waumini tumepata nini zaidi ya kusota mitaani tukiwa mafupa, baada ya kuitumikia kampuni miaka kumi na zaidi, kwa bidii na uaminifu, wanakuja wengine wanakula kilaini…sisi tumepata nini kama sio kutupwa nje kwa dharau…’ akaendelea kuongea jamaa yangu kwenye simu. Nilimkumbuka sana jamaa yangu huyu siku za karibuni nilipokutana naye, nilimuulizia vipi maendeleo ya huko kazini kwao. Alisema kwa unyonge maneno haya; ‘mimi nimeamini kweli maneno matakatifu kuwa tajiri kuuona ufalme wa mbingu ni kama farasi kupita kwenye tundu la sindano’ Nikamuuliza vipi kulikoni, kwani siku zote ulikuwa mstari wa mbele kuwatetea matajiri kuwa wanafanya haki na wanaoharibu ni wafanyakazi kwa kuwa wavivu… ‘Ndugu yangu, hutaamini tangu muondoke, mshahara wangu ni ule ule haujawahi kuongezeka, licha ya kufanyakazi kwa bidii kwasababu tulibakia wachache, licha ya kuonyesha uaminifu wa hali ya juu, na…lakini hakuina cha nyiongeza wala ahadi za kuaminika,…fikiria hali za maisha sasa hivi, yanazidi kuwa magumu, kwa gharama za vitu kupanda bei, majukumu yameongezeka, kwani nimeoa, na nina watoto, na isitoshe dada yangu alipofariki kaniachia watoto, watoto yatima, hawana baba wala mama, mimi ndio baba yao, mimi ndio mama yao…siunakumbuka mume wa dada yangu alifariki kipindi kile mpo kazini, basi baadaye nikawachukua dada na watoto tukawa tunaishi nao, dada yangu akaanza kuumwa baadaye nikahangaika naye kwa matibabu huku na kule… ‘Hutaamini, nilikuwa naomba angalau mkopo ili nikamtibie dada yangu nilinyimwa, ili hali mimi nashika hela zao mamilioni kwa mamilioni, mimi ndiye mtunza pesa wao, naenda benki nachukua mamilioni yao kuwalipa, lakini hawakukubali kunipa mkopo wa kumtibia dada yangu, eti mshahara wangu ni mdogo, nimeshachukua mkopo mwingine haujaisha makato, kwahiyo sistahili kupata mkopo mwingine. ‘Ni sawa sheria hiyo ipo, lakini kuna dharura kama hiyo ya ugonjwa, hata hivyo kwanini wasiniongezee mshahara wakati wanaajiri wafanyakazi wapya ambao wanakuja hawajui kitu kabisa mimi ndio nawafundisha kazi, na kutokujua kwao kazi, bado wanalipwa mishahara mikubwa zaidi yangu, hebu fikiria, mimi nakisomo changu nalipwa laki tatu, wao wanalipwa milioni tatu, …ni haki hiyo kweli. Wamenizidi nini mimi, eti kwasababu wanatoka nje, eti kwasababu ni watoto wa wakubwa, eti kwasababu ni ngozi nyeupe, eti…wanatoa sababu ambazo haziniingii akilini… ‘Sasa watoto wa dada wamfukuzwa shule, kwasababu ya ada, nashindwa nifanye nini, kwani wakati wazazi wao wapo walikuwa wakiwasomesha shule nzuri za binafsi, na nikaona niwatoe hapo niwapeleke shule ya gharama ndogo kidogo, lakini hata hiyo nimeshindwa kuwalipia…sasa hivi yupo mmoja anaumwa, kila mara , wakati mwingine anarudishwa nyumbani kutoka shuleni kwa sababu ya matatizo ambayo yanahitaji hela nyingi za matibabu, sina hizo hela, nimeomba kazini nimenyimwa… ‘Kumbuka mimi ni cashier pale ofisini, mimi ni mhasibu, mimi nafanya kazi hata za mauzo…wanajua wao kuwa mimi ni `kila kazi’ hapo kazini, hata chai za mabosi natengeneza…wananilipa nini hawa watu zaidi ya kunipa sifa za mdomoni, na ikifika muda wa maslahi wanakuwa hawanijui kabisa, eti kwasababu `sina title’ mtoto wa mlalahoi anayeishi `uswahilini’ kama wanavyopenda kuita wao wenyewe!...sasa nifanyeje, nimechanganyikiwa ndugu yangu, kama una chochote naomba uchangie matibabu ya mtoto huyu, anateseka sana, naomba muwe na Huruma, kwani akifa, nitasononokea sana, inafikia muda anasema `kama wazazi wake wangelikuwepo hai angeshapona…’ Alipofika hapo mzee mzima machozi yalimtoka Nilitaka kumwambia `unaomba jamvi msibani’ lakini nikatuliza kauli hiyo kwani akuombaye msada kwenye dhiki, usimkate kalima kwa kutoa matatizo yako pia, toa hata msaada wa ushauri, kuliko kuanza kuelezea na wewe una shida hii na ile, kuwa eti na mimi nadaiwa na mimi sina hela ya kula, na mimi…sio busara. Nilimpa nini, mungu ndiye mwenyewe anajua…! Leo nasoma tangazo hilo kuwa jamaa yangu huyu anatafutwa na polisi kwa kumuibia mwajiri wake. Sikuamini kabisaa, mpaka aliponipigia simu mtu ambaye alikuwa karibu naye! Na huyu aliyenipigia simu amemsifia ndugu yetu huyo kuwa kafanya jambo la maana saana, kwani hata kama angefanyakazi hapo hadi akongoloke, asingeweza kuzipata hizo hela, akaongezea kuwa `kachukua jasho lake ambalo alikuwa akinyonywa , miaka nenda rudi. Nchi yetu hii inapokwenda ni kubaya, kwani makampuni mengi yaliyopo hapa nchini hayana utawala bora, watawala waliopo wanawagawa wafanyakazi kimatabaka, wazungu na Wahindi toka nje wanalipwa zaidi ya huko kwao walipotoka, kila kitu analipiwa, na mshahara wake ni ule wenye sifuri sita kwenda mbele, nyumba analipiwa, watoto wanasomeshwa, analipiwa hadi karatasi ya chooni. ‘Mimi kama ningekuwa raisi ningesema tuwaajiri wazungu tu hapa nchini , kwani ni wachapa kazi,waaminifu….siunaona mwenyewe wanavyojituma…’ hii ni kauli ya meneja wetu wakati anafuatilia vibali vya kumuingiza bwana fedha toka India. Ni kweli wanachapa kazi, ni kweli ni waaminifu, lakini wanafanya hivyo kwa kuwa wao wana sababu na motisha! Niliwahi kuuliza swali kwa hawa `wakubwa’ kuhusiana na mslahi ya wafanyakazi kuwa je gari lililojazwa robo tanki linaweza kusafiri sawa na lile lilojazwa tanki zima. Bofya hapa! Safari ni moja wengine magari yao `fully tank with reserve’ kwasababu za rangi yao, dini yao, mmmh, mwenzetu nk ,wengine robo tanki na hakuna hata akiba, unategemea huyu mtu ajitume sawasawa na huyo wa fully tank? Jamani hivi kweli hii ni haki, nakumbuka usemi wa mkuu , kwenye blogi yake alisema `mnyonge mnyongeni lakini haki yake mpeni…itafika muda watu watadai haki yao, kwani `uvumilivu una mipaka yake, ikizidi sana,,,ndiyo hayo …migomo, maandamano…mwisho wa siku, hakukaliki tena! Wabunge Mpo?...mmh, najua hili haliwagusi sana, kwani nyie ni `matawi ya juu’ Ni mimi: emu-three
http://miram3.blogspot.com/feeds/posts/default?alt=rss

"