Mar 1, 2011

HOTUBA YA MH RAIS KWA WANANCHI TAREHE 28/2/2011


HOTUBA YA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA
TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,
KWA WANANCHI, 28 FEBRUARI, 2011

Ndugu Wananchi

 Kama ilivyo ada naomba kuanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma kwa kutujaalia fursa nyingine ya kuzungumza kwa kutumia utaratibu tuliojiwekea wa kila mwisho wa mwezi. Leo nina mambo matano ambayo ningependa kuyazungumzia.
Milipuko ya Mabomu Gongolamboto
Ndugu Wananchi;
Jambo la kwanza ni lile tukio la usiku wa tarehe 17 Februari, 2011 la milipuko ya mabomu iliyotokea katika ghala kuu la Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania lililoko Gongolamboto, Dar es Salaam.  Pamoja na kuharibu majengo mengi yanayohifadhi zana na vifaa muhimu vya Jeshi letu, milipuko hiyo imesababisha vifo vya Watanzania wenzetu 25 na wengine 512 kujeruhiwa.  Aidha, mali na nyumba kadhaa za raia zimeharibiwa kwa viwango mbalimbali.  
Siku iliyofuata Baraza la Usalama la Taifa lilikutana kujadili tukio hilo na kuagiza hatua mbalimbali za kuchukuliwa kushughulikia athari za maafa hayo.  Mara baada ya kikao hicho nililitangazia taifa maamuzi tuliyofanya.  Napenda kutumia nafasi hii kutoa pongezi maalum kwa Ofisi ya Waziri Mkuu hususan Kitengo cha Maafa, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Madaktari na Wauguzi wa Hospitali za Amana, Temeke na Muhimbili na nyinginezo pamoja  na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwa kazi kubwa na nzuri ya kutekeleza maagizo ya Baraza la Usalama la Taifa.
Maiti wote 25 wameshazikwa kwa gharama ya Serikali kule ambako ndugu waliamua wakazikwe.  Kwa ajili hiyo maiti 10 wamezikwa Dar es Salaam na wengineo mikoani kama ifuatavyo:-, Mara – wanne, Pwani – watatu,  Tanga -  wawili, , Lindi – mmoja, Kagera -  mmoja, Kilimanjaro – mmoja, Mbeya – mmoja  na Mtwara – mmoja.  Majeruhi wameendelea kupatiwa matibabu na huduma stahili.  Mpaka sasa kuna majeruhi 36 ambao bado wamelazwa katika hospitali za Amana, Temeke na Muhimbili.  Watoto 857 waliopotezana na wazazi wao wameshaunganishwa na familia zao.  Hata hivyo, watoto 15 bado hawajatambuliwa na wazazi au walezi wao.  Kwa sasa watoto hao wamepelekwa kwenye kituo cha kulelea watoto cha Kurasini.  Napenda kuwakumbusha wazazi waliopotelewa na watoto kufika kituoni hapo kuwatambua watoto wao.  Ni jambo la kustaajabisha kwamba zaidi ya siku kumi sasa zimepita wazazi au walezi hawajajitokeza kutafuta watoto wao.
Ndugu Wananchi,
Ndugu zetu 539 katika kaya 115 hawana makazi kutokana na nyumba zao kuharibiwa na mabomu.  Wamepewa hifadhi ya mahema yaliyojengwa pembeni mwa makazi yao.  Aidha, wamepatiwa mavazi, magodoro, mashuka na mablanketi.  Kadhalika wanapatiwa huduma za chakula, maji na mengineyo.  Pamoja na mchango wa Serikali, wapo watu na mashirika mbalimbali yaliyotoa michango mbalimbali kusaidia waathirika hao.  Napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukrani nyingi sana kwa moyo wao wa upendo, ukarimu na huruma kwa ndugu zetu hao ambao kwa sasa wanaishi katika mazingira magumu yasiyotarajiwa.  Inshaalah Mola atawalipa maradufu kila mlichopunguza.  Narudia tena uamuzi na ahadi ya Serikali ya kuendelea kuwahudumia mpaka hapo watakapofidiwa kwa uharibifu wa nyumba zao na mali zao.
Ndugu Wananchi;
Utekelezaji wa agizo la  kutambua na kufanya tathmini ya nyumba zilizoharibiwa unaendelea kufanywa kwa nia ya kuwafidia ipasavyo.  Kwa upande wa fidia tumeamua kuwa Serikali ibebe jukumu la kujenga upya nyumba hizo kwa mujibu wa kiwango cha uharibifu.  Nimeagiza Jeshi la Kujenga Taifa lifanye kazi hiyo kupitia Shirika lake la Uchumi.  Nimeamua hivyo ili kuhakikisha kuwa maisha ya ndugu zetu waliokumbwa na maafa haya yanarejea kuwa ya kawaida mapema iwezekanavyo.  Aidha, nimeagiza Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ishirikiane na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Kitengo cha Taifa cha Maafa kuhakikisha kuwa utekelezaji unaanza mapema iwezekanavyo.
Ndugu Wananchi,
Jeshi la Ulinzi la Wananchi lilipewa kazi kubwa tatu.  Kwanza, madaktari na wauguzi wa Jeshi washiriki katika kusaidia kutoa huduma kwa wananchi waliojeruhiwa.  Nafurahi na kupongeza kwamba jambo hili limetekelezwa vizuri.  Pili, kuokota na kukusanya mabomu ambayo hayakulipuka na vipande vipande vya mabomu yaliyolipuka kutoka maeneo wanayoishi raia.  Kazi hiyo nayo imefanyika na inaendelea kufanyika.  Mpaka tarehe 25 Februari, 2011, Wanajeshi wamekusanya zaidi ya mabomu na vipande 3,013.  Yapo maombi ya wananchi kuwa kasi ya ukusanyaji iongezwe, ujumbe huo umeshafikishwa kwa viongozi wa Jeshi.
Ndugu Wananchi;
Jukumu la tatu ambalo ni wajibu wao kufanya, ni kuhakikisha kuwa uchunguzi wa kina unafanywa kuhusu chanzo cha milipuko hiyo.  Nimearifiwa na Mkuu wa Majeshi kuwa Bodi ya Uchunguzi imekwishaundwa.  Wakati huo huo lile agizo la Baraza la Usalama kuwa wataalamu wa nchi za nje nao washirikiswe katika uchunguzi limetekelezwa.  Serikali ya Marekani imetoa wataalamu kutoka Jeshi lake kusaidia katika uchunguzi.  Ni imani yangu kuwa uchunguzi wa makundi haya mawili kila moja kwa wakati wake huenda utasaidia kupata ukweli.  Napenda kutumia nafasi hii kuwasihi Watanzania wenzangu kuwa na subira na kuacha tabia za kueneza uvumi kwenye vijiwe vya kahawa na kwenye vikao vya kinywaji  kuhusu chanzo cha milipuko hiyo.  Wakati mwingine watu wanageuza dhana zao kuwa ndiyo ukweli na kupotosha au hata kuwatia watu hofu.  Wataalamu wamekwishafika, ukweli wenyewe utajulikana baada ya muda si mrefu.
Hali ya Chakula Nchini
Ndugu wananchi;
Jambo la pili ninalotaka kulisemea ni hali ya chakula nchini.  Kwa ujumla hali ya upatikanaji wa chakula nchini katika maeneo mengi ni ya kuridhisha isipokuwa katika maeneo machache.  Taarifa ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika inaonyesha kwamba kuna akiba ya kutosha ya chakula katika maghala ya Serikali, ya wafanyabiashara wakubwa na katika maghala ya wakulima mashambani.  Maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula yana tani 216,012 za mahindi na mpunga, nafaka ambazo zinatuhakikishia kuwa upungufu wowote wa chakula tutaukabili bila matatizo.  Kiasi hicho ndicho kikubwa kuliko chote kilichowahi kuhifadhiwa tangu hifadhi hiyo kuanzishwa na shabaha yetu ni kufikia tani 400,000 ifikapo mwaka 2015.
Ndugu wananchi;
Katika baadhi ya maeneo nchini kumeanza kujitokeza matatizo ya upungufu wa chakula kuanzia mwezi Januari 2011. Mengi ya maeneo hayo ni yale yanayopata mvua za vuli ambazo bahati mbaya hazikuwa nzuri.  Imetambuliwa kuwa katika Halmashauri 36 za mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Morogoro, Mwanza, Shinyanga, Mara, Tabora, Singida, Dodoma, Lindi, Mtwara na Iringa ndiko kwenye maeneo mengi yenye upungufu mkubwa.
Tayari Serikali imeidhinisha kutolewa kwa jumla ya tani 13,760 za chakula kutoka Akiba ya Taifa ya Chakula (NFRA) kwa ajili ya kuhudumia watu 423,530 walioathiriwa na upungufu wa chakula katika maeneo hayo. Kazi ya usambazaji inaendelea.  Hadi sasa jumla ya tani 4,822 za chakula cha msaada kimekwishatolewa katika mikoa ya Arusha, Iringa, Morogoro na Lindi.  Napenda kuwathibitishia kuwa tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa hakuna Mtanzania atakayekufa kwa njaa. Tutawahudumia ipasavyo hawa waliokwishatambulika na wengineo watakaojitokeza siku za usoni.   
Ndugu Wananchi;
Kwa sababu ya kukosekana kwa mvua za vuli na mvua kuwa pungufu katika maeneo mengine, mwelekeo wa hali ya upatikanaji wa chakula siyo mzuri sana.  Tayari kiasi cha chakula kinachoingia kwenye masoko ya mijini si kingi kama ilivyokuwa siku za nyuma.  Hii imekuwa kiini cha bei za vyakula kupanda katika masoko ya mijini.  Hivi sasa matumaini yetu yapo kwa Mwenyezi Mungu kujaalia mvua za masika ziwe nzuri.  Kama hilo halitatokea nchi yetu itakumbwa na tatizo kubwa la upungufu wa chakula na bei za vyakula kuwa kubwa zaidi.  Tutajipanga ipasavyo kukabiliana na hali hiyo ili kunusuru maisha ya Watanzania.  Ili kupunguza makali ya bei ya vyakula nimeagiza akiba ya taifa itumike kwa kuwauzia wafanyabiashara ya chakula mijini.
Ongezeko la Bei ya Sukari
Ndugu Wananchi;
  Jambo la tatu ni bei ya Sukari.  Hivi karibuni bei ya sukari nchini imekuwa ikipanda kwa kasi kubwa na katika baadhi ya maeneo nchini bei ya sukari ilifika zaidi ya shilingi 2,200 kwa kilo.  Nilimuomba Waziri Mkuu kufuatilia kwa karibu tatizo hilo na amefanya hivyo.  Alikutana na wadau wote wakiwemo wazalishaji na wasambazaji wa sukari nchini.  Kilichobainika ni kuwa bei ya sukari ilipanda sana kwa sababu ya kuwepo upungufu wa sukari katika soko.  Upungufu wa sukari katika soko ulikuwa umesababishwa na sukari iliyokuwepo katika maghala ya viwanda vya sukari na ya wafanyabiashara wakubwa wa sukari kutofikishwa kwa wingi madukani kwa hofu ambazo hazikuwa na msingi.  Aidha, mahusiano mabaya kati ya wazalishaji na wafanyabiashara wakubwa wa sukari ilikuwa sababu kubwa.  Wenye viwanda wakawa wanatoa kiasi kidogo kuliko wafanyabiashara walichokuwa wanaagiza.  Kwa upande wao wafanyabiashara wakubwa nao wakawa wanasambaza kiasi kidogo kidogo kwa madai kuwa wasijekuishiwa kabisa na bidhaa hiyo.
 Katika mazungumzo hayo ilibainika kuwa viwanda na wafanyabiashara wakubwa wanayo sukari ya kutosheleza mahitaji mpaka mwezi Mei, 2011.  Kutakuwa na uhaba katika miezi ya Mei na Juni kutokana na ukweli kwamba viwanda vya sukari nchini husimamisha uzalishaji kuanzia mwezi Februari hadi Mei kila mwaka.  Hiki ni kipindi cha mvua nyingi, miwa hunyonya maji mengi hivyo huwa haitoi sukari nyingi.  Wenye viwanda hutumia muda huo kusimamisha uzalishaji na kufanya matengenezo ya mitambo.
Ndugu Wananchi;
Waziri Mkuu aliagiza sukari yote iliyoko katika maghala itoke mara moja na kufikishwa katika soko ili watu waipate tena kwa bei nafuu.  Katika mazungumzo ya pamoja na wadau, ilikubalika kabisa kuwa hata kwa maeneo yaliyo mbali na viwanda vya sukari bei haiwezi kuzidi shilingi 1,700/= kwa kilo.  Atakayeuza kwa bei kubwa zaidi ya hiyo anadhulumu, taarifa zitolewe ili hatua za kinidhamu na kisheria zichukuliwe, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa kufutiwa leseni ya biashara. 
Ndugu Wananchi;
Kwa ajili ya kuziba pengo la miezi ya Mei na Juni kibali kimetolewa cha kuagiza tani 50,000 za sukari kutoka nje ya nchi.  Tunatarajia kupata tani 12,500 kutoka nchi za Afrika Mashariki na tani 37,500 zitatoka nje ya Afrika ya Mashariki.  Bahati mbaya sana kuna upungufu mkubwa sana wa sukari duniani, hivyo bei imepanda kuliko wakati wowote katika miaka ya hivi karibuni.  Tani moja ya sukari inauzwa kwa dola za Marekani 900 ikilinganshwa na dola za Marekani 500 mwaka 2009.  Hivyo, sukari itakayoingizwa wakati huo itakuwa na bei kubwa.  Kwa nia ya kuzifanya bei ziwe chini na kuwapa watumiaji nafuu, sukari hiyo haitatozwa ushuru wa forodha.  Tutafanya hivyo pia kwa vyakula vyote muhimu tutakavyolazimika kuagiza kutoka nje kwa sababu ya uhaba wa mvua uliokumba maeneo mengi hapa nchini.
Hali ya Umeme
Ndugu wananchi,
Jambo la nne ni hali ya umeme.  Kama mnavyofahamu, hali ya upatikanaji wa umeme nchini ni mbaya.  Chanzo cha matatizo ni kupungua sana kwa maji katika Bwawa kubwa la Mtera.    Hadi jana kina cha Bwawa hilo kimeshuka hadi kufikia mita 691.25 ambacho ni pungufu kwa mita 7.  Kwa sasa zimebaki  mita 1.25 tu juu ya kiwango cha chini kinachoruhusiwa kuendesha mitambo ya kuzalisha umeme.
 Tarehe 15 Februari, 2011, Baraza la Mawaziri lilijadili na kuidhinisha mpango wa dharura wa TANESCO wa kukodi mitambo ya kuzalisha MW 260 za umeme.  Baraza limeitaka Bodi na Menejimenti ya TANESCO kuhakikisha kuwa mchakato huo unakamilika mapema iwezekanavyo ili kupunguza makali na athari za ukosefu mkubwa wa umeme kwa jamii na uchumi wa nchi.  Aidha, imesisitizwa kuwa pamoja na udharura uliokuwepo sheria na taratibu za manunuzi ya umma vizingatiwe.  Pia, wahakikishe kuwa mkataba wataoingia uwe ni wenye maslahi kwa taifa.   Vile vile, watoa huduma wawe ni makampuni yanayofahamika na yenye sifa stahiki na kuaminika.
Natambua kuwa Bodi na Mejemienti ya Shirika la Umeme, wanaendelea na mchakato wa kupata umeme huo wa dharura kati ya sasa na Julai, 2011.
Ndugu Wananchi;
Tulipopata tatizo kama hili mwaka 2006/2007 tuliamua kuwa tuanze safari ya kupunguza kutegemea mno umeme wa nguvu ya maji kwa kuongeza matumizi ya vyanzo vingine vya nishati.  Mpango umetengenezwa na utekelezaji wake unaendelea.  Tayari umeme wa MW 145 wa kutokana na gesi asilia umeongezwa kwa kugharamiwa na Serikali. Aidha, mwisho wa mwaka huu MW 160 zitaongezeka yaani MW 100 Dar es Salaam na MW 60 Mwanza kwa gharama za Serikali.
 Bahati mbaya kutokana na matatizo ya fedha ya kimataifa, wawekezaji wa sekta binafsi wa kuzalisha MW 300 za umeme wa gesi asilia pale Mtwara walijiondoa.  Umeme huo ungekuwa tayari umeshaingizwa katika gridi ya taifa hivi sasa na kuondoa tatizo la sasa.  Wawekezaji wengine wamepatikana na mazungumzo yanaendelea vizuri.  Mradi wa Kiwira umecheleweshwa na mchakato wa kubadili milki na kupata mkopo wa dola za Marekani 400 milioni za kuwezesha ujenzi wa kituo cha kuzalisha MW 200.  Suala la kubadili milki limefikia ukingoni na mchakato wa kupata mkopo unaendelea kwa matumaini.
Ndugu Wananchi;
          Waswahili wana msemo usemao “jitihada za mwanadamu hazishindi kudra ya Mwenyezi Mungu”.  Bahati mbaya sana tatizo la ukame limetukuta tena wakati mipango hiyo haijakamilika.  Miaka miwili ijayo hali itakuwa tofauti sana kwani miradi hii na mingine kadhaa itakuwa imekamilika na kulihakikishia taifa uhakika wa umeme.
Naomba ndugu zangu muelewe kuwa miradi hii huchukua muda kukamilika.  Mitambo huchukua muda kutengenezwa na ujenzi wa kituo nao pia.  Ingekuwa ni mitambo ya kununua tu dukani tungefanya hivyo na kulimaliza mara moja tatizo hili.  Tena lingeisha zamani na wala sisi tusingelikuta.  Subira yavuta heri.
Hali ya Usalama Nchini
Ndugu Wananchi;
          Hivi karibuni wananchi wengi wameingiwa na hofu kubwa kuhusu usalama wa nchi yetu.  Ni mara ya kwanza Watanzania wamekuwa hivyo.  Hofu hiyo inatokana na kauli na vitendo vya wenzetu wa CHADEMA vyenye dhamira ya kutaka kuleta machafuko makubwa na uvunjifu wa amani nchini.  Kufanya maandamano na mikutano ni haki ya msingi ya vyama vya siasa na raia.  Lakini, kuigeuza fursa hiyo kuwa ni jukwaa la kuchochea ghasia na kwa nia ya kuiondoa Serikali iliyoko madarakani kwa mabavu ni matumizi mabaya ya fursa hiyo.
          Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila miaka mitano tunafanya uchaguzi wa kuchagua viongozi wetu.  Uchaguzi wa mwisho tumefanya tarehe 31 Oktoba, 2010.  Kabla ya hapo tulikuwa na kampeni zilizochukua karibu miezi mwili na nusu.  Kila chama kilielezea jinsi kitakavyokabiliana na matatizo yanayowakabili wananchi wa nchi yetu ikiwa ni pamoja na haya wanayoyazungumza sasa.  Hatimaye siku ya uchaguzi wananchi walifanya uamuzi wa kuchagua chama walichokiamini, nacho ni Chama cha Mapinduzi.  Iweje leo, miezi mitatu baadae kwa mtu au chama cha siasa kufanya maandamano kwa masuala yale yale waliyoyasema kwenye kampeni.  Siyo sawa hata kidogo.  Kuchochea ghasia ati kwa nia ya kuiondoa Serikali madarakani ni kinyume cha Katiba na ni kuiingiza nchi katika mgogoro usiokuwa wa lazima.  Tutasababisha umwagaji wa damu, watu kupoteza maisha na mali zao kuharibiwa bila sababu yoyote ya msingi.
Ndugu Wananchi;
          Katika nchi ya kidemokrasia na kwa wanademokrasia wa kweli, mnapomaliza uchaguzi mmoja, mnajiandaa kwa uchaguzi mwingine.  Mnajenga upya chama chenu, mnaongeza wanachama, mnaboresha sera na hoja zenu pamoja na namna ya kuziwasilisha ili watu wawakubali nyinyi na kuwakataa wenzenu.  Na, uwanja muhimu wa kufanya sehemu kubwa ya hayo ni katika Bunge na Halmashauri za wilaya kupitia Wabunge na Madiwani wenu.
          Kuacha kufanya hivyo na badala yake kuamua kuzunguka nchi nzima na kuchochea ghasia kwa lengo la kuwaondoa walioshinda ili muingie nyie ni kinyume kabisa na misingi ya demokrasia.  Tutajenga misingi ya hovyo na nchi yetu itakosa amani na utulivu daima.  Hebu fikirieni, kama kila atakayeshindwa uchaguzi anafanya hivyo tutakuwa nchi ya namna gani?  Tanzania yetu hii yenye sifa na heshima ya kuwa nchi ya amani na utulivu itapoteza kabisa sifa hiyo na badala yake umwagaji wa damu na mateso kwa watu wasiokuwa na hatia vitageuka kuwa maisha ya kawaida.  Hatuitendei haki nchi yetu na hatuwatendei hai wananchi tunaodai tunawapenda na kuwatetea.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
Ndugu zetu wa CHADEMA wanayajua yote haya, lakini wanalo lao jambo.  Wanataka kuipeleka nchi yetu pabaya kwa kukidhi uchu wao wa madaraka.  Kwao sasa demokrasia haina maana, inaweza kusubiri.  Wanataka kutumia mabavu.  Naomba  tuyakatae mambo yao.  Tusiwafuate.  Waambieni mchezo wao ni hatari na ni mauti yetu.  Sisi katika Serikali tutajitahidi kutimiza wajibu wetu wa kulinda usalama wa nchi yetu, watu wake na mali zao.
Ndugu Zangu, Watanzania Wenzangu;
          Ni kweli kuna hali ngumu ya maisha, na kukabiliana nayo ndiyo kazi tunayoendelea nayo kufanya kila siku.  Tumeelekeza nguvu zetu na rasilimali zetu huko na mafanikio yanaonekana katika nyanja mbalimbali na maeneo mbalimbali.  Kikwazo siyo upungufu wa sera wala dhamira, kikwazo kikubwa ni kiwango cha maendeleo madogo ya uchumi wetu na hivyo uwezo wetu siyo mkubwa wa kuyakabili na kuyamaliza matatizo yote haraka kama ambavyo tunapenda iwe.
Ndugu Zangu;
 Hayo si matatizo ya kumalizika ndani ya siku tisa. Mzee Nyerere aliongoza kwa miaka 23 na hakuyamaliza matatizo ya maendeleo ya nchi hii.  Na wale wa umri wangu au kunizidi wanakumbuka hali ilivyokuwa wakati anang’atuka. Hakuacha nchi ikiwa tajiri.  Mzee Mwinyi kakaa miaka 10 hakuyamaliza, Mzee Mkapa nae kakaa miaka 10 hakuyamaliza.  Mie nimekaa miaka mitano hayakwisha na nitamaliza mitano hayataisha yote.  Lililo muhimu kuliko yote ni kuwa katika kila awamu nchi yetu imekuwa inapiga hatua ya kusonga mbele katika kujiletea maendeleo.  Hali iliyokuwa wakati ule sivyo ilivyokuwa mwaka 1985, wala 1995 au 2005 na ilivyo sasa.  Katika miaka mitano hii kuna maendeleo yanayoonekana wazi, pamoja na changamoto nyingi tumefanya juhudi kubwa na mafanikio yanaonekana katika nyanja zote za maisha ya Watanzania. Mwenye macho haambiwi tazama.
          Lakini, pia ni muhimu watu kutambua ukweli kwamba uchumi kama wetu ambao haujajenga uwezo wake wa ndani wa kujitosheleza kwa mahitaji yake, huathirika sana nay ale yanayotokea katika uchumi wa dunia.  Unapoyumba na sisi tunayumba.  Bei za mafuta katika soko la dunia zikipanda na kwetu kupitia gharama za uchukuzi na uzalishaji huongezeka na kusababisha bei za bidhaa kupanda.  Mfumuko wa bei ukipanda China, nguo na bidhaa tunazonunua kutoka China hupanda bei.  Hivi sasa mataifa yote makubwa tunakonunua bidhaa mfumuko wa bei umepanda na sisi tunaathirika.  Mvua ikikosekana kunakuwa na uhaba wa chakula, bei za vyakula hupanda na watu wengine hukosa chakula.  Lawama kwa Serikali au Rais Kikwete inaanzia wapi?  Hata kwa matatizo yote hayo na mengine tumekuwa tunatafuta nafuu kwa kiwango tunachoweza.  Aghalabu, hutoa nafuu ya kodi kama tulivyofanya kwa sukari na tulivyowahi kufanya kwa saruji na kadhalika.   Tutaendelea kufanya hivyo inapobidi.
Mwisho
Ndugu Wananchi,
Naomba nimalizie kwa kuwashukuru wananchi kwa kuwa wavumilivu kwa kipindi chote hiki, nawaomba muendelee kuiunga mkono Serikali yenu. Tuendelee kuchapa kazi kwa bidii kuijenga na kuiendeleza nchi yetu na vile vile tuendelee kuithamini na kuitunza amani ya nchi yetu.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni sana kwa kunisikiliza!