Mar 1, 2011

MSEKWA APONDA MAELEZO YA BUJIKU JUU YA MYUMBO WA CCM

Na Shadrack Sagati
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Pius Msekwa, amekiri kuwepo tatizo ndani ya chama hicho lakini amesema kuwa si kwwli kuwa CCM imepoteza mwelekeo.
Msekwa amesema, tatizo ndani ya chama hicho ni kamati za maadili za chama hicho kushindwa kutimiza wajibu wao.
Amesema, kamati hizo kuanzia tawi hadi Taifa zimelala wakati malalamiko ya wananchi juu ya vitendo vya rushwa ndani ya chama vikikithiri na kuonya kuwa hali hiyo imesababisha wananchi kupiga kura za hasira dhidi ya chama hicho katika uchaguzi uliopita.
Katika mahojiano na gazeti hili ofisini kwake jana, Msekwa pamoja na kukubaliana na kada wa CCM, Joseph Butiku, juu ya rushwa ndani ya CCM, lakini alimpinga akisema kuporomoka kwa maadili si chanzo cha CCM kupoteza dira wala mwelekeo.
Alisema, dira na mwelekeo wa CCM viko kwenye Ilani ya Uchaguzi, Katiba ya chama pamoja na sera ambazo zilinadiwa wakati wa uchaguzi na wananchi wakazikubali na kuamua kuichagua CCM. “Hivyo ni makosa kusema CCM haina mwelekeo, chama hakiwezi kukosa mwelekeo wala dira.”
Jana Butiku alinukuliwa na gazeti hili akisema CCM haina dira wala mwelekeo kutokana na viongozi wake kuzama kwenye vitendo vya rushwa. Katika kujibu hoja hiyo ya Butiku, Msekwa alisema: “Kuporomoka kwa maadili dhidi ya viongozi wetu si chama kukosa mwelekeo, hayo ni matatizo ya viongozi wetu lakini chama kina dira.”
Makamu Mwenyekiti huyo wa CCM, alisema kamati za maadili ndizo zenye jukumu la kuwachukulia hatua wanachama na viongozi ambao wanajihusisha na vitendo vya rushwa; lakini akakiri kuwa zimelala huku viongozi wetu waliopewa jukumu la kufanya kazi hizo hawatimizi wajibu wao.
“Unategemea nini kama kamati za maadili zimelala, hizi hazitimizi wajibu wake hivyo vitendo vya rushwa kuendelea kushamiri…ndio maana wananchi wamekuwa na hasira dhidi ya chama chetu,” alisema Msekwa.
Alipoulizwa chama kinachukua hatua gani dhidi ya kamati hizo za maadili ambazo zimelala, alisema, “hatuwezi kumshikia mtu rungu ili awajibike, cha msingi watambue wajibu wao na wajirekebishe ili wafanye kazi wanazotakiwa kuzifanya.”
Alionya kuwa bila vikao vya CCM vinavyowajibika kushughulikia matatizo ya rushwa kuwajibika, wananchi wataendelea kukasirika kama walivyofanya kwenye uchaguzi uliopita. “Ni lazima tuchukue hatua ili kurejesha imani ya wanachama na wapenzi kwa chama chetu.”
Akizungumzia lawama wanazotupiwa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM kuwa hawajakomaa kisiasa, Msekwa alisema chama hicho kimewapa fursa kubwa vijana kuanzia kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa na bungeni ili waweze kuiva kisiasa kwa manufaa ya baadaye.
Lakini akasema kama vijana hao wameshindwa kuzitumia fursa hizo kukomaa kisiasa chama hakiwezi kulaumiwa kwani tayari kimetimiza wajibu wake wa kuwashirikisha kwenye uongozi wa nchi.
“Sisi kazi yetu ni kuwapika lakini kama na wenyewe wamegawanyika kwenye makundi na kuingia kwenye mmomonyoko wa maadili chama kisilaumiwe bali walaumiwe wao maana tayari tumewapa nafasi,” alisema Msekwa.
Source:  Habarileo