Apr 24, 2011

DC aendesha ibada ya mazishi ya polisii!!

DC aendesha ibada ya mazishi ya polisii!!: "
IGP Mwema atema cheche Makamanda wa wilaya zote kufundwa Serikali za mitaa wakae `mkao wa kula` DC ajitosa kuendesha ibada ya mazishi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Said Mwema, akitoa heshima za mwisho mbele ya mwili wa ofisa wa Polisi, Joseph, wakati wa mazishi yake yaliyofanyika kijijini kwake wilayani Nkasi mkoani Rukwa jana. Siku chache baada ya wananchi wa kijiji cha Mwakashahala kata ya Puge wilayani Nzega, mkoani Tabora, kumuua askari polisi mwenye namba E6530 Joseph Millinga. Mkuu wa Jeshi la Polisi, Jenerali Said Mwema, ametema cheche na kusema kuwa makamanda wa polisi wa wilaya zote nchini wanakutana mjini Dodoma kuandaa mkakati wa kuimarisha ushirikiano baina yake na wananchi. Alisema lengo ni kujenga ushirikiano wa dhati baina ya jeshi hilo, serikali za mitaa na wananchi kwa ujumla ili kujenga uwanja mpana wa upatikanaji wa haki pindi wananchi wanapokwenda polisi. Akizungumza baada ya mazishi ya marehemu Millinga yaliyofanyika katika kisiwa cha Manda Kerenge kilichopo katika kata ya Kirando wilayani Nkasi mkoani Rukwa, IGP Mwema alisema hatua hiyo inakusudia pia kupunguza kasumba ya baadhi ya wananchi kujichukulia sheria mkononi. Aliongeza kwamba jeshi la polisi limeweka mikakati endelevu ya kulinda maisha ya wananchi na mali zao ikiwa ni pamoja na kupambana na vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na baadhi ya watu wanaojifanya kuwa na hasira kali na kuvunja sheria za nchi. Alisema kuwa “ni kifo cha kusikitisha kilichomkumba kijana wetu akiwa katika kulinda usalama wa wananchi kutokana na madhara makubwa yanayowapata wananchi wengi mara baada ya kutumia madawa hayo ya kulevya aina ya bangi sasa jeshi likitaka kuokoa maisha ya wananchi na wananchi wenyewe wanakatisha uhai wa askari wetu jamani tutafika wapi kwa hali hii?...juzi tu nimepata habari juu ya msiba mwingine uliotokea katika kijiji cha Miombo katika wilaya yenu ya Nkasi huku Tabora nako wakamuua askari wetu.” Alikumbusha kwamba “hakuna jambo lolote linaloshindikana katika sheria hivyo kama kuna mtu anaona hakufuata utaratibu basi jitahidini kufuata utaratibu wa kisheria kuanzia ngazi ya mtaa, kijiji kata wilaya mkoa na hata taifa na si kujichukulia sheria mikononi.” Hata hivyo, katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi, Joyce Mgana, amelazimika kuendesha ibada ya mazishi, baada ya Kanisa Katoliki kukataa kumzika marehemu huyo kwa maelezo kwamba hakuwa anatimiza masharti ya kikanisa wakati wa uhai wake. Mgana na mbunge wa jimbo la Nkasi Kaskazini, Ally Keisy nao walitoa hisia zao juu vitendo vya uhalifu vinavyoendelea kutokea katika maeneo mbalimbali nchini na hususani katika wilaya hiyo ya Nkasi, huku msemaji wa familia akiomba nafasi zaidi ya ajira kwa vijana waliobakia katika kisiwa hicho cha Manda Kerenge. Marehemu Milinga aliuawa Aprili 20, mwaka huu majira ya saa 4 asubuhi baada ya wananchi wa kijiji cha Mwakashanhala kata ya Puge wilayani Nzega mkoani Tabora, kuwashambulia askari waliokuwa wakifanya msako wa kuwakamata watu wanaolima bangi. Jeshi la polisi limetuma kikosi maalum cha Polisi wa Kutuliza Ghasia (FFU) zaidi ya 60 kinachoongozwa na Kamanda wa Polisi mkoa wa Tabora, Liberatus Barlow, kwenda kijijini hapo kuwasaka watu waliohusika katika mauaji hayo. Marehemu Millinga ameacha mjane na watoto watatu. http://www.ippmedia.com/
"