Apr 1, 2011

MAGUFULI ATUA LOLIONDO KWA BABU NA KUMWAGA BILLIONI 1

Waziri wa ujenzi John Magufuli akinywa dawa kwa Mchungaji Ambilikile Masapila katika kijiji cha Samunge, Loliondo mkoani Arusha

WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli, jana aliingia katika Kijijini Samunge kwa mchungaji Ambilikile Masapila na kupata kikombe cha dawa, kisha kutangaza neema ya kujengwa kwa barabara kuu inayoingia kijijini hapo. Magufuli aliuambia umati wa watu uliokuwa ukisubiri zamu yao kunywa dawa kuwa, Serikali itatumia Sh1.05 bilioni kwa ajili kutengenenza barabara hiyo ili iweze kupitika wakati wote kwa lengo la kuwarahisishia usafiri wanaokwenda kunywa dawa kwa Babu Masapila. Barabara inayoingia katika kijiji hicho ambacho kimeshuhudia maelfu ya magari yakiingia kila siku tofauti na ilivyokuwa awali, ipo katika hali mbaya kiasi cha baadhi ya maneo kutoruhusu magari kupishana. Kwa mujibu wa Magufuli, Serikali ilikwishatoa Sh500/-milioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo kuanzia Mto wa Mbu eneo la Kigongoni, Ngaresero, Samunge hadi kuungana na barabara ya kutoka mkoani Mara. Dk Magufuli alisema jana ndio aliuagiza uongozi wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) Makao Makuu kutuma Sh500 milioni ili kuharakisha ujenzi huo. 'Tayari fedha hizo zimeshatumwa Tanroads mkoani Arusha na Meneja wa Mkoa, Kakoko (Deodatus), niko naye hapa hivyo kazi itakwenda haraka ili watu wanaokuja kwa mchungaji kunywa dawa wasiendelee kuteseka,' alisema Dk Magufuli huku akishangiliwa na mamia ya watu waliokuwa wakimsikiliza. Waziri pia huyo alisema kwa mamlaka aliyonayo, atawasiliana na uongozi wa Mfuko wa Barabara ili utume fedha za dharura kiasi cha Sh50 milioni kwa uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorogoro kwa ajili ya kufanya matenegenezo mengine ya barabara, wilayani humo. Alisema fedha zilizotengwa kwa ajilii ya barabara za nchi nzima kupitia mfuko huo zinafikia Sh286 bilioni katika bajeti ya mwaka 2010/11, na kwamba upo uwezekano mkubwa wa fedha za dharura kupatikana kwa ajili ya matenegenezo ya barabara ya Samunge.
"