Apr 26, 2011

MAUAJI YA KISHIRIKINA YAFANYWA MYUNGA MBOZI

Na,Rashid Mkwinda, Tunduma.
MAUAJI ya kutisha yamedaiwa kutokea katika kijiji cha Lwasho kata ya Myunga wilayani Mbozi  baada ya watu wanaokadiriwa kufikia watano kuuawa kwa imani za kishirikina na kisha kutumbukizwa katika mto Momba baada ya kunyofolewa sehemu za siri,ulimi na meno.
Kwa mujibu wa maelezo kutoka kwa wananchi wa Kata hiyo ni kwamba mauaji hayo yanadaiwa kufanywa na mfanyabiashara mmoja (jina tunalo) mkazi wa kijiji hicho ambaye anadaiwa kutoa viungo vya ndani vya marehemu ikiwemo sehemu za siri,meno na ulimi kwa nia ya kufanyia vitendo vya ushirikina.
Akizungumzia mauaji hayo Diwani wa kata ya Myunga Bw.Richard Siyame alisema kuwa matukio hayo yameanza kutokea mwishoni mwa mwezi Disemba ambapo baadhi ya wapiti njia na wakazi wa kata hiyo wamekuwa wakipotea katika mazingira ya kutatanisha.
Alisema kuwa mauaji hayo yamebainika wazi April 21 baada ya kifo cha msichana mmoja ambaye hakufahamika jina lake ambaye mwili wake ulikutwa  kando yam to Momba huku ukiwa umeondolewa sehemu zake za siri,meno na titi moja la kushoto na kwamba wananchi waliwaambia maofisa wa polisi waliofika eneo la tukio kuwa wauaji wanafahamika.
Bw.Siyame alisema kuwa akiwa pamoja na Mwenyekiti wa kamati ya ulinzi shirikishi wa kijiji cha Lwasho kulikotokea mauaji hayo Bw.Mahesabu Siyame na Ofisa Mtendaji wa kijiji Bw.Edwin Sikapizye walijaribu kuwatuliza wananchi na kuliacha jeshi la polisi lifanye uchunguzi wake lakini ilishindikana baada ya wananchi kusema kuwa watachukua sheria mkononi.
Hata hivyo mara baada ya mzozano baina ya wananchi na askari polisi waliofika kuuchukua mwili wa marehemu kumalizika askari polisi waliondoka na mfanyabiashara anayetuhumiwa kuhusika na mauaji hayo(jina tunalo) hadi katika kituo cha polisi cha Tunduma.
Aidha Bw.Siyame alisema kuwa siku moja baada ya kuchukuliwa kwa mtuhumiwa huyo mtu mmoja aliyetambulika kwa jina la Leonard Simfukwe aliuawa na wananchi wenye hasira baada ya mabishano baina yake na wananchi hao akidai kuwa mtuhumiwa anayedaiwa kufanya mauaji hayo ameonewa.
Alisema kuwa wakiwa katika mzozano huo ndani ya gari wananchi hao walimtupa chini kisha wakasimamisha gari na kumpiga kwa mawe na marungu hadi alipofariki dunia.
Bw.Siyame alisema kuwa wakati marehemu akipata kipigo kutoka kwa wananchi hao alidai kuwa mbali na mwanamke aliyeuawa kuna watu watano waliouawa na kufungiwa mawe shingoni kisha kutumbukizwa mtoni ambao walipotea katika mazingira ya kutatanisha kijijini hapo.
Alisema kuwa siku hiyo hiyo wananchi hao walivamia nyumba ya mfanyabiashara anayedaiwa kuwa ni muuaji na kufanya uharibifu ambapo waliingia katika moja ya vyumba vya nyumba hiyo na kukuta nguo mbalimbali zenye damu ambazo zinadaiwa kuwa ni watu waliouawa na kutumbukizwa mtoni.
Kwa upande wake Ofisa mtendaji wa kijiji Bw.Sikapizye alisema kuwa matukio hayo yamejenga picha ya kuendelezwa kwa uhalifu na mauaji ya imani za ushirikina jambo ambalo linasababisha kurudisha nyuma maendeleo ya kata hiyo.
Bw.Sikapizye alisema kuwa ndani ya nyumba hiyo kulikutwa baadhi ya nguo ambazo zinadaiwa kuwa ni za watu waliotoweka katika mazingira ya kutatanisha ambapo pia kulikuwa na gari aina ya Landorover 110 inayodaiwa kuwa ilikuwa ni ya mtu mmoja aliyefika kupanga katika nyumba ya kulala wageni ya mfanyanyabiashara anayetuhumiwa kwa mauaji ambaye naye alitoweka katika mazingira ya kutatanisha.
Alisema gari hii ilikuwa nje ya nyumba ya mfanyabishara huyo kwa muda mrefu huku watu wakidhani kuwa ni mali ya mfanyabishara huyo ambapo baadaye ilielezwa kuwa ni gari ya askari mmoja ambaye hakufahamika jina lake aliyeomba kulihifadhi gari hilo eneo hilo.
Alibainisha kuwa hata hivyo taarifa zote zinazohusu mauaji hayo zimefikishwa katika kituo cha Polisi cha Tunduma ambako mtuhumiwa alikamatwa.
Alisema kuwa hata hivyo serikali ya kijiji inafanya jitihada za kuwatafuta watu wengine wanaodaiwa kuuawa na kutumbukizwa mtoni kwa imani za ushirikina.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Mbeya Bw.Advocate Nyombi hakuweza kupatikana kuelezea mauaji hayo kutokana na kuwa siku hiyo ilikuwa ni ya mapumziko ambapo pia namba zake zote za simu ya mkononi zilikuwa hazipatikani.