Apr 4, 2011

uzinduzi wa mfumo wa uombaji mikopo kupitia mtandaoni

Profesa Anselm Lwoga akiongea wakati wa uzinduzi wa Mfumo wa Uombaji Mikopo kwa njia ya Mtandao (OLAS) ambao umeshaanza kutumika kwa mafanikio makubwa. Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji, Bw. George Nyatega akifuatiwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano Bw. Cosmas Mwaisobwa.

Profesa Anselm Lwoga,(katikati) akibonyeza kompyuta kuashiria Uzinduzi wa Mfumo wa Uombaji Mikopo kwa njia ya Mtandao (OLAS) akishuhudiwa na Mkurugenzi Mtendaji, Bw. George Nyatega na Mkurugenzi wa Mipango,Utafiti na Teknohama, Bw. Asangye Bangu.

Mkurugenzi Mtendaj Bw. George Nyatega akiongea wakati wa hafla hii Tovuti ya Bodi ya Mikopo www.heslb.go.tz HOTUBA FUPI YA MWENYEKITI WA BODI KWENYE UZINDUZI WA MFUMO WA UOMBAJI MIKOPO KWA NJIA YA MTANDAO (OLAS) Ninayo furaha kujumuika nanyi katika hafla hii fupi ya kuzindua rasmi utaratibu mpya wa uombaji wa mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kwa njia ya mtandao yaani “Online Loan Application System (OLAS)”. Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu imeanzisha utaratibu huu mpya ambao utaanza kutumiwa kwa mara ya kwanza na waombaji wapya na wale Wanafunzi wanaoendelea na masomo katika Vyuo vya Elimu ya Juu mbalimbali kwa mwaka wa masomo 2011/2012. Mabibi na Mabwana, Tangu Bodi ya Mikopo ilipoanza rasmi shughuli zake kiutendaji mwezi Julai 2005, hadi mwaka wa masomo wa 2010/2011 wanafunzi wa elimu ya juu ambao wanatimiza vigezo vya kukopeshwa, wamekuwa wakiomba mikopo, kwa kutumia fomu maalum na kisha kuziwasilisha Bodi. Utaratibu huu ulitumika vizuri na kuwezesha utoaji mikopo kwa ufanisi, ingawa ulikuwa na changamoto katika utekelezaji wake, kama vile kutumia muda mrefu zaidi kuwasilisha fomu za waombaji mikopo, kuchungua na kuhamishia taarifa za waombaji katika mfumo wa kompyuta (Loan Management System) kabla ya kuanza zoezi la kupanga mikopo. Kutokana na kuongezeka kwa idadi ya waombaji na pia maendeleo ya kiteknolojia, Bodi imelazimika kuboresha utendaji wake kwa kuanzisha utaratibu huu mpya, ili kuongeza ufanisi katika zoezi zima la utoaji mikopo. Mabibi na Mabwana, Uombaji mikopo kwa njia ya mtandao umeanzishwa kwa lengo la kuboresha utoaji mikopo na vilevile kuimarisha utunzaji wa kumbukumbu za wanufaika wa mikopo. Hivyo, Bodi ya Mikopo, inatarajia kwamba kwa kupitia OLAS, waombaji wataweza kuingiza taarifa zao binafsi na kuziwasilisha Bodi kwa urahisi na usahihi zaidi. Hii ikiwa na maana kwamba mwombaji atawasilisha yeye mwenyewe taarifa zake na maelezo mengine muhimu na taarifa hizo zitapokelewa moja kwa moja katika mfumo wa uombaji mikopo. Mabibi na Mabwana, Ni matarajio ya Bodi kwamba, wanafunzi wote wanaotarajia kujiunga na Vyuo vya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo 2011/2012 watasoma kwa umakini mwongozo wa uombaji mikopo ambao umetolewa na Bodi kupitia vyombo vya habari, vipeperushi na kwenye tovuti ya Bodi ili kupata ufahamu wa kutosha wa zoezi hili. Vilevile Bodi inasisitiza juu ya umuhimu wa waombaji kuzingatia maelekezo ya jinsi ya kuwasilisha maombi ya mikopo, ndani ya muda uliopangwa na kuhakikisha wanawasilisha taarifa sahihi na za kweli zitakazowezesha upangaji wa madaraja ya mikopo kwa waombaji wanaostahili. Kwa hayo machache, natamka rasmi kuwa utaratibu mpya wa kuomba mikopo ya Wanafunzi wa elimu ya juu kwa njia ya mtandao yaani “Online Loan Application System (OLAS)” sasa umezinduliwa rasmi tayari kwa zoezi la uombaji wa mikopo litakaloanza rasmi Aprili 1, 2011. Ukitaka mwandani wa namna ya kuomba mkopo BOFYA HAPA
"