Apr 16, 2011

WANANWAKE WATAKIWA KUJIFUNGULIA KATIKA VITUO VYA AFYA




Mke wa Rais na Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) katikati , akikata utepe akiwa na watendaji wa shirika la EGPAF la Marekani lililowezesha  upatikanaji wa jengo hilo kwa kushirikiana na wizara ya afya nchini  kuashiria uzinduzi wa jengo la wodi ya wazazi la kituo cha Afya Mangaka wilayani Nanyumbu, Wa pili kutoka kulia ni mkurugenzi mkazi  wa shirika la EGPAF nchini Bw. Jeroen Van’t Bosch.


Na Anna Nkinda – Maelezo, Nanyumbu


Kina mama wajawazito wametakiwa kujenga mazoea ya kujifungulia katika vituo vya Afya ili kuweza kupata huduma stahili na endelevu katika kuzuia maambukizi ya Virusi Vya UKIMWI (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
Wito huo umetolewa jana na mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea na wakazi wa wilaya ya Nanyumbu mara baada ya kumaliza kufungua wodi ya wazazi na mradi wa kuzuia maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) katika kituo cha afya Mangaka kilichopo wilayani humo ambacho kimejengwa kwa ufadhili wa mfuko wa Elizabeth Glaser Paediatric AIDS Foundation (EGPAF) .

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliendelea kuwahimiza wanawake kwenda kupima katika kituo cha afya ili kujua kama wamepata maambukizi ya VVU au la na kama watakuwa wamepata maambukizi wasione aibu kujiunga na huduma zinazotolewa kwani zitawasaidia kujifungua mtoto asiye na maambukizi ya ugonjwa huo.

“Msione aibu kujiunga na huduma ya kudhibiti maambukizi ya VVU kutoka kwa Mama kwenda kwa Mtoto (PMTCT) kwani kupata maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI si suala la mtu kuwa tabia za kihuni bali mtu anaweza kupata kwa njia tofauti. Leo hii kama utaamua kuzaa mtoto ambaye hana maambukizi ya ugonjwa huo inawezekana kabisa kwani ni wengi wamepata huduma hii na kujifungua watoto ambao ni salama”, alisema Mama Kikwete.

Aliendelea kusema kuwa kutokana na takwimu za utafiti wa hali za Kiafya kulingana na idadi ya watu , Tanzania Demographic Health Survey (TDHS) za mwaka 2009/2010 zinaonyesha kuwa zaidi ya wanawake 20 hupoteza maisha kila siku pia watoto wachanga 29 katika kila 1000 wanaozaliwa hufa kutokana na tatizo la uzazi.

Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema, “Sababu kubwa inayosababisha vifo hivi ni uhaba wa huduma bora za afya, ikiwemo miundo mbinu haba katika wodi za wazazi, vifaa vya kutolea huduma, upungufu wa watoa huduma, umbali kutoka sehemu anapoishi mama mpaka zahanati au kituo cha afya na nyingine nyingi. Hii hupelekea akina mama wengi kujifungulia kwa wakunga wa jadi”.

“Haina maana kuwa wakunga wa jadi hawana msaada, la! bali hupelekea matatizo hasa pale mgonjwa anapopata matatizo makubwa kama upasuaji (operation), shinikizo la damu ( BP) na kadhalika, kwani mkunga wa jadi hawezi kukabiliana na changamoto kama hizo”.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa EGPAF Dk. Jeroen Van’t Pad Bosch alisema kuwa shirika hilo limedhamiria kupunguza na hatimaye kuondoa kabisa maambukizi ya VVU kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto kupitia utafiti, uhamasishaji na uhabarisi pamoja na tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na VVU.

Alisema kuwa Shirika hilo linafanya shughuli zake kwa kushirikiana na Halmashauri za wilaya katika mikoa sita hapa nchini ambayo ni Arusha, Kilimanjaro, Tabora, Shinyanga, Lindi na Mtwara.

Katika mkoa wa Mtwara kuna vituo 167 vya kupima kina mama wajawazito na kutoa dawa za kuwakinga watoto wachanga wasipate maambukizi. Vituo hivyo vimewezeshwa kutoa huduma na wakina mama 148719 wamepata ushauri nasaha na kati ya hao 138252 wamepima kwa hiari , 4824 wamegundulika kuwa na maambukizi ya VVU. Kati ya hao 3930 wamepata huduma za PMTCT huku watoto wanaopata huduma hiyo wakiwa 2443.

“Sisi tunaamini kuwa maambukizi ya VVU kwa mtoto yanaweza kuzuilika ikiwa mama atahudhuria kliniki mapema wakati wa ujauzito, kujifungulia katika kituo cha afya na pia kama atatumia huduma kwa uthabiti hivyo basi tunawaomba kina mama wa Nanyumbu wakitumie kituo hiki cha Afya ili waweze kujifungua salama na kupunguza vifo vyao na vya watoto wachanga”, alisema Dk. Bosch.

Akisoma taarifa ya kituo hicho daktari wa wilaya hiyo Dk. Joseph Mkapa alisema kuwa kutokana na ufadhili wa EGPAF kati ya mwaka 2008 hadi 2010 wilaya hiyo imefanikiwa kupima kina mama wajawazito 15,094 kati ya kina mama wajawazito 16,915 waliohudhuria kliniki kati ya hao wajawazito 360 walionekana kuwa na maambukizi ya VVU.

“Kati ya kina mama wajawazito walioonekana kuwa na maambukizi ya VVU ni 179 pekee waliopata dawa za kinga, hii inatokana na akina mama wengi wajawazito kuendelea kujifungulia majumbani na kwa wakunga wa jadi”, alisema.

Dk. Mkapa alizitaja changamoto wanazokabiliana nazo kuwa ni pamoja na baadhi ya kina mama wajawazito kujifungulia majumbanni na kwa wakunga wa jadi, ufinyu wa maji safi na salama ya kutosha, vifaa vya upasuaji, upungufu wa majengo, usafiri pamoja na upungufu wa wafanyakazi.