May 27, 2011

MKE WA WAZIRI MKUU WA INDIA ATOA MSAADA WA MILION 15 KWA WAMA

Na Anna Nkinda – Maelezo
27/5/2011 Dar es Salaam Mke wa waziri Mkuu wa India Mama Gursharan Kaur ametoa msaada wa shilingi milioni 15 kwa Taasisi ya Wanawake na Maendeleoo (WAMA) fedha ambazo zitatumika katika shughuli mbalimbali za kuwasaidia watanzania zinazofanywa na taasisi hiyo.
Msaada huo umetolewa leo katika ofisi za WAMA zilizopo jijini Dar es Salaam wakati mama Kaur alipoitembelea taasisi hiyo inayoongozwa na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete kwa ajili ya kufahamu shughuli zinazofanywa na WAMA.
Akikabidhi msaada huo Mama Kaur alisema kuwa ameguswa na kazi zinazofanywa na WAMA za kuisaidia jamii ya kitanzania, hivyo msaada huo utasaidia kutekeleza majukumu mbalimbali wanayoyafanya.
Kwa upande wake Mama Kikwete alishukuru kwa msaada huo na kusema kuwa fedha hizo zitasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua matatizo yanayoikabili jamii ya kitanzania.
Alisema kuwa taasisi ya WAMA imekuwa ikipokea misaada mbalimbali kutoka kwa wadau wa maendeleo wa ndani na wa nje ya nchi hivyo aliwaomba wananchi wenye moyo wa kusaidia wasisite kufanya hivyo bila ya kuangalia kama msaada watakaoutoa ni mdogo au mkubwa.
Mama Kikwete alisema kuwa Taasisi ya WAMA imekuwa ikifanya kazi mbalimbali za kuhakikisha kuwa inawasaidia wanawake kuinua maisha yao, kuisaidia jamii ya watanzania kuwa na afya bora, kupambana na maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI kwa vijana na kada tofauti, kushughulikia uzazi salama na kuwawezesha watoto wa kike ambao ni yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu kupata elimu.
Mama Kaur ameambatana na mumewe waziri Mkuu wa India Dr. Manmohan Singh aliyeko nchini katika ziara ya kikazi ya siku tatu.
Mwisho.