Jun 10, 2011

Wamarekani waja juu kuhusu Clinton kuwania ubosi WB

Mamlaka za juu nchini Marekani zimekuja juu na kukanusha vikali juu ya tetesi zilizozagaa kuwa Waziri wake wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa kimataifa, Hillary Clinton, amekuwa akiwania kuwa kiongozi katika Benki ya Dunia

“Kwa asilimia 100 nakanusha kuhusu habari hizi” amesema Philippe Reines, ambaye ni mshauri wa karibu wa Clinton, wakati alipokuwa akikanusha taarifa zilizoandikwa na shirika la habari la Reuters.

Reines, aliyekuwa akihojiwa na shirika jingine la habari la AFP, aliongeza kuwa shirika hilo la habari la Uingereza limetoa taarifa hizo bila kufanya uchunguzi wala kuwasiliana na mamlaka zozote za Marekani na kwamba yeye pamoja na Wamarekani kwa ujumla wamesikitishwa na uzushi huo.

“Kama nitakuwa muwazi kabisa, bibi Clinton hajawahi kuwa na maongezi ya namna yoyote ile na rais wa Marekani, Ikulu ya Marekani au na mtu mwingine yeyote kuhusiana na wazo la kuwania kuwa mtendaji mkuu katika Benki ya Dunia. Hajawahi kuonyesha dhamira ya namna hiyo na kwa hakika hata akipewa nafasi hiyo hawezi kuikubali” aliongeza bwana Reines.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Jay Carney, naye akaungana naye kwa kusema kuwa “Taarifa hizo ni za uongo, zisizo na ukweli wowote” .

Alhamisi ya wiki hii, shirika la Reuters, lilitoa habari iliyodai kuwa mke huyo wa rais wa zamani wa Marekani, alikuwa katika maongezi na Ikulu ya Marekani, juu ya azma yake ya kuwania nafazi ya uongozi katika taasisi hiyo kubwa ya fedha duniani.

Reuters, lilidai kuwa bibi Clinton alikuwa amewasilisha ombi la kuachia ngazi kama Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, ifikapo mwakani ili aweze kufanikisha azma yake ya kuingia katika utawala kwenye Benki ya Dunia.

"