Jun 12, 2011

Wapanda Mianzi kuhifadhi mazingira Mbeya

Erasto Njavike akitoa maelezo mafupi baada ya zoezi hilo la kupanda mianzi eneo hilo la Mwansenga kuhifadhi mazingira.
ASASI isiyokuwa ya kiserikali ya Roots & Shoots, imepanda miti aina ya mianzi eneo la Mwansenga Jijini Mbeya kwa ajili ya kuhifadhi mazingira katika maeneo ya vyanzo vya Maji. Zoezi hilo lilifanyika mwishoni mwa wiki kwa kushirikisha vijana 300 kutoka katika kada mbalimbali wakiwemo wanafunzi wa shule za Sekondari na Msingi na vikundi vya Scout. Akizungumza katika eneo hilo baada ya kupanda mianzi hiyo, Mratibu wa asasi hiyo Erasto Njavike alisema kuwa asasi yake inajishughulisha na shughuli mbalimbali zikiwemo za kuhifadhi Wanyama, Mazingira na jamii kwa kushirikisha vijana wanaoweza kujitolea. Njavike alisema kuwa katika eneo hilo wamefanikiwa kupanda mianzi 265 kwa kushirikiana na Serikali ya Jiji la Mbeya na wanamazingira wengine ikiwemo asasi ya kuhifadhi Mazingira mkoa wa Mbeya MRECA. Kwa upande wake Afisa Mazingira wa Jiji la Mbeya January Kazoba alisema kuwa wamefurahishwa na asasi hiyo kusjitolea kupanda mianzi hiyo kwa kushirikisha vijana na asasi zingine na kwamba Serikali ya Jiji hilo imejipanga vema kutoa elimu ya utunzaji wa Mazingira na kukabiliana na wahalibifu wa mazingira wakiwemo wanaolima karibu na vyanzo vya maji. Kwa upande wake Mwanafuzni wa kidato cha Sita katika shule ya Sekondari ya wasichana ya Loleza iliyopo mkoani Mbeya Pendo Mboya alisema anatoa wito kwa vijana kote nchini kujitokeza katika shughuli za kujitolea nguvu kazi kwa manufaa ya Taifa. Naye Mkurugenzi wa asasi ya MRECA Mchungaji William Mwamalanga alisema asasi ya Roots & Shoots imeonesha mwanga wa jamii kuhusu kujitolea katika kuhifadhi mazingira na aliziomba asasi zingine kutimiza majukumu yake ipasavyo kama ilivyofanya asasi hiyo. KUTOKA www.kalulunga.blogspot.com
"