Jun 23, 2011

WILAYA YA MBOZI YATANGAZA VITA NA KAMPUNI YA LIMA INAYONUNUA KAHAWA MBICHI

Na Danny Tweve
Uongozi wa wilaya ya Mbozi pamoja na baraza la Madiwani la halmaashauri ya wilaya hiyo kwa kauli moja wametangaza vita dhidi ya kampuni yoyote itakayobainika kununua kahawa Mbichi maarufu kama kahawa cheri.

Msimamo huo umetangazwa kwenye kikao cha baraza la madiwani kilichoketi leo katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya, ambapo imeelezwa kuwa tayari watendaji wa vijiji, kata pamoja na jeshi la polisi wameshapewa maelekezo kutekeleza agizo hilo.

Akichokoza maelekezo hayo Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Elick Ambakisye amesema, kwa muda mrefu kampuni na wafanyabiashara wametumia uelewa mdogo wa baadhi ya wakulima katika kujinufaisha kwa kununua kahawa cheri ambayo bei zake ni sawa na kuwaibia wakulima wakati bei ya sasa ya kahawa kavu ni mara 100 ya bei wanayouza kahawa cheri.
Alisema hali hiyo imefikia hatua kuwafanya wananchi kurejea kwenye ukoloni wa kipato ambacho wamekuwa waklizalisha kwa jasho kubwa lakini wachache wanajinufaisha, na kwamba kampuni itakayokutwa ikifanya manunuzi hayo mwaka huu ni kuwakamata watendaji wake.
Akichangia kwa upande wa serikali kuu katibu tawala wilaya ya Mbozi Magacha akkizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya alisema msimamo huo utatoa mfano mwaka huu kwakuwa kampuni ya Lima baada ya kuona imebanwa wilayani ikapita njia zake za vichochoroni na kufanikiwa kupata leseni ya kununua kahawa, wakati ambapo haikubaliki katika eneo ambalo wanataka kununua.
Alisema ili kuonyesha hasira za wananchi, kampuni hiyo ikituma watendaji wake vijijini wakamatwe na kuchukuliwa hatua papo hapo na kwamba maelekezo yameshatolewa kwa mamlaka za dola wilayani humo.

Mwaka jana wilaya ya Mbozi imejiingizia zaidi ya Bilion 100 kutokana na mauzo ya kahawa yake kupitia vikundi vya wakulima katika mnada wa moshi ambapo halmashauri ya wilaya iliweza kukusanya zaidi ya shilinmgi 1.5 Bilion ikiwa ni ushuru wa zao hilo.
Kampeni za kumlinda mkulima zilianza kutekelezwa mwaka jana ambapo watendaji wa kampuni ya Lima walikamatwa wakati fulani wakinunua kahawa cheri vijijini na baadaye kuachiwa, lakini msimamo wa mwaka huu unalenga kuhakikisha kahawa hiyo haiuzwi  ikiwa mbichi kutokana na bei yake kupanda mara dufu hadi kufikia 20,000 kwa kilo vijijini kwa kahawa kavu.

Wakati tamko hilo likitolewa kuna taarifa kuwa kuna watu wanazunguka vijjini kununua kahawa cheri kwa bei ya shilingi 50,000/ kwa ndoo ya plastiki ya lita 20 hali ambayo inawarusha roho wakulima na kushindwa kuvumilia kuuza kwenye soko rasmi na badala yake kuuza kwenye soko la kahawa cheri ili washike haraka hiyo pesa ya fasta fasta.
Ikiwa msimamo wa wilaya hiyo utasimamiwa vyema kuna kila dalili za ushindi wa mkulima wa wilaya ya Mbozi kuendelea kufanywa kichwa cha mwendawazimu cha kujifunzia kunyoa.
Wakati hayo yakiendelea tuhuma za aliyetoa leseni hiyo zinaelekezwa kwa waziri mwenye dhamana na kilimo kutokana na bodi ya Kahawa kukataa tangu mwaka jana mchezo wa kuuza kahawa cheri. Inaelezwa kuwa kampuni ya Lima ilienda kumwona mh waziri wa Kilimo ili kuiruhusu kununua kahawa hatua ambayo iliwezesha leseni hiyo kuagizwa kutolewa na mh waziri.

Pamoja na hatua hiyo, kuna tishio kuwa kuna uwezekano wa kusababisha uharibifu wa mali na hata kusababisha maafa vijijini wakati kampuni hiyo itakavyojihusisha na ununuzi huo ikiwa  maelekezo yaliyotolewa yatatekelezwa kwakuwa imeelezwa wazi kuwa magari ya kampuni hiyo yakikutwa yakinunua kahawa cheri hatua za ndani ya vijiji na zile za kidola zichukuliwe.

Tangazo hilio pia limeelezwa kusimamiwa na waheshimiwa madiwani.