Jul 8, 2011

Duni Haji Atishia Kujiuzulu Uwaziri Zanzibar

WAZIRI wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Juma Duni Haji
--------------------
WAZIRI wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Juma Duni Haji amesema atajiuzulu wadhifa wake kama kitengo cha wagonjwa mahututi (ICU) kitashindikana kupatiwa vifaa vya kutoa huduma kwa wagonjwa katika bajeti ijayo.
Duni alisema hayo wakati akijibu hoja mbali mbali za wajumbe wa Baraza la Wakilishi waliochangia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara ya afya kwa mwaka 2011/2012 mjini hapa.
“Mheshimiwa Naibu Spika nitajiuzulu nafasi yangu ya uwaziri kama Serikali itashindwa kuifanyia ukarabati kitengo cha ICU kabla ya bajeti ya mwakani,” alisema Duni. Duni alitoa kauli hiyo kufuatia baadhi ya wajumbe wa baraza la wawakilishi kumbana ili kutaka kujua sababu za Serikali kushindwa kukifanyia ukarabati mkubwa kitengo cha ICU hadi sasa. Wajumbe wengi waliochangia makadirio ya bajeti ya wizara ya afya walisikitika na kitendo cha serikali kushindwa kukifanyia ukarabati kitengo hicho ambacho ni muhimu kwa afya za wananchi, wakati serikali ikitenga fedha nyingi kwa shughuli nyingine, ikiwemo kununua magari ya kifahari. “Mheshimwa naibu spika mimi bado sijaridhishwa na hali ya kitengo cha ICU katika hospitali ya Mnazi Mmoja mjini hapa.....kwa nini tusubiri fedha za wahisani wakati tunajua umuhimu wa afya ya jamii,” alisema Hamza Hassan Juma ambaye ni mwakilishi wa Jimbo la Kwamtipura kwa tiketi ya CCM.
"