Jul 6, 2011

MUNGU IBARIKI TANZANIA (TWIGA STARs) KESHO

DUA za watanzania zimeelekezwa kwa timu ya wanawake Tanzania 'Twiga Stars' ambayo inataraji kushambulia uwanjani kesho (Julai 7) kuwakabili wenyeji Zimbabwe 'Mighty Warriors' katika mechi ya pili ya nusu fainali ya michuano ya Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Kusini mwa Afrika (COSAFA) itakayochezwa Uwanja wa Rufaro, jijini hapa. Mechi ya Twiga Stars itachezwa saa 9.15 kwa saa za hapa (saa 10.15 kwa saa za Tanzania), wakati nusu fainali ya kwanza kati ya Afrika Kusini 'Banyana Banyana' dhidi ya Malawi itaanza saa 6.30 mchana kwa saa za hapa. Twiga Stars inayoongozwa na nahodha wake Sophia Mwasikili imefanya mazoezi mepesi leo asubuhi kwenye Uwanja wa Rufaro kujiweka tayari kwa ajili ya pambano hilo ambalo tayari limekuwa gumzo kwa mashabiki wa hapa. Akizungumza baada ya mazoezi , Kocha Mkuu wa Twiga, Charles Mkwasa amesema Zimbabwe ni timu nzuri lakini amekiandaa kikosi chake kwa ajili ya kuibuka na ushindi ili kiweze kucheza nusu fainali na hatimaye kunyakua kombe hilo. 'Zimbabwe watakuwa na faida ya kucheza mbele ya mashabiki wao. Kwa kawaida wanamtegemea yule mshambuliaji wao mrefu wa kati (Rufaro Mutyavaviri) huku wakitumia sana wingi ya kulia. Nimewaandaa wachezaji wangu kwa hilo. 'Kikosi hakitakuwa na mabadiliko ambapo Ettoe Mlenzi aliyekuwa na kadi mbili za njano atarejea uwanjani. Mabadiliko yatakuwa kwa beki wa kushoto ambapo kwenye mechi ya Zimbabwe ataanza Fatuma Khatibu,' amesema Mkwasa ambaye timu yake imeingia katika michuano hiyo ikiwa mwalikwa kwa vile si mwanachama wa COSAFA. Mutyavaviri ndiye anayeongoza katika ufungaji katika michuano hiyo ambapo kwenye mechi kati ya timu yake na Malawi alifunga mabao matano. Mighty Warriors ilishinda mabao 8-2 na mshambuliaji huyo amekuwa akifunga katika kila mechi. Twiga Stars ni miongoni mwa timu ambazo tangu awali zilikuwa zikipewa nafasi ya kutwaa ubingwa kutokana na kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika zilizofanyika mwishoni mwa mwaka jana nchini Afrika Kusini. Nyingine ni wenyeji Mighty Warriors na Banyana Banyana ambazo zote zimefuzu kwa hatua ya nusu fainali. Wachezaji watakaonza kwa Twiga Stars katika mechi ya kesho ni Fatuma Omary, Fatuma Makusanya, Fatuma Khatibu, Sophia Mwasikili, Mwanaidi Tamba, Mwajuma Abdallah, Mwanahamisi Omary, Ettoe Mlenzi, Fatuma Mustafa, Asha Rashid na Fadhila Kigalawa. Twiga Stars imekuwa ikishangiliwa kwa nguvu na Watanzania wanaoishi hapa wakiongozwa na Balozi Adadi Rajab ambaye ameshuhudia mechi zote za timu hiyo. Mechi kati ya Twiga Stars na Mighty Warriors itaoneshwa moja kwa moja (live) kupitia SuperSport 4 na Shirika la Utanganzaji la Zimbabwe (ZBC). Fainali na mechi ya kutafuta mshindi wa tatu (classification) zitachezwa Julai 9 mwaka huu kwenye Uwanja wa Rufaro. Timu ambazo zimeaga mashindano baada ya kushindwa kufuzu kwa hatua ya nusu fainali jana ni Botswana, Zambia, Lesotho na Msumbiji. Boniface Wambura Ofisa Habari TFF Harare
"