Jul 8, 2011

Mwingiliano TBS,TFDA kikwazo kwa wajasiriamali

MWINGILIANO wa utendaji kati ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) unachangia kukwamisha jitihada za wajasiriamali wadogo, katika kukuza uchumi wao na taifa kwa jumla. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro juzi, Mkuu wa Mradi wa usindikaji wa amatunda na mbogamboga kwa wajasiriamali wadogo wa Tanzania na Rwanda, Profesa Bendantunguka Tiisekwa,alisema mwingiliano huo ni tatizo katika maendeleo ya wajasiriamali. "Unaweza kukuta TBS inafanya ukaguzi katika viwanda na kutoa ushauri lakini baadaye wanakuja TFDA na kutia ushauri wao ambao wakati mwingine unakinzana na ule wa TBS,"alisema Profesa Tiisekwa. Alisema ni vema serikali ikatazama upya utendaji wa mashirika hayo ili kuondoa mwingiliano na hivyo kuwawezesha wajasiriamali wadogo kufanya shughuli zao kwa uhuru . Profesa Tiisekwa ambaye pia ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), alisema mbali na tatizo la mwingiliano wa mamlaka hizo mbili, pia kuna matatizo ya kisera na sheria zinazosimamia masuala ya chakula. Kuhusu mradi wa usindikaji matunda na mbogamboga kibiashara, mkuu huyo wa mradi alisema utasaidia kuinua vipato vya wajasiriamali. Alisema mradi huo unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwaka huu, una gharimu zaidi Sh 888 milioni na unalenga kuwafundisha wajasirimali wadogo namna ya kuendesha shughuli zao kwa ufanisi.
"