Oct 25, 2011

DKT BILAL AKAGUA BANDA LA TANZANIA KATIKA MKUTANO WA MWASILIANO WA KIMATAIFA GENEVA

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Tanzania Youth Alliance (TAYOA), Peter Masika, wakati akitazama mashine ya mawasiliano (ICT Mobile Booth), iliyotengenezwa na vijana wa TAYOA, wakati akikagua banda la maonyesho la Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) uliofanyika Geneva, Switzerland Oktoba 24, 2011.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akiangalia mfumo wa kuwasiliana kwa masafa (tele-conference) katika Banda la HUWAWEI, wakati akitembelea mabanda mbalimbali yaliyopo katika maonyesho ya ITU, jijini Geneva, Switzerland Oktoba 24, 2011.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja wa Uhuru One, Mihayo Wilmore, kuhusu matumizi rahisi ya kompyuta ndogo na mpango wa kuzisambaza na kuwawezesha wanafunzi wa Tanzania kutumia kompyuta hizo, wakati wakati akikagua banda la maonyesho la Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) uliofanyika Geneva, Switzerland Oktoba 24, 2011.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa Naibu Mkurugenzi wa Kanda (TCRA), Victor Nkya, wakati akikagua banda la maonyesho la Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) uliofanyika Geneva, Switzerland Oktoba 24, 2011.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa kuhusu Teknolojia ya mawasiliano, wakati alipotembelea Banda la maonyesho Burundi,katika Mkutano wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) uliofanyika Geneva, Switzerland Oktoba 24, 2011.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akizungumza na Mkuu wa Mawasiliano wa Kampuni ya Qatar Assistive Technology Center, Ahmed Habib, ambaye ni mlemavu, wakati alipotembelea Banda la maonyesho la kampuni hiyo katika Mkutano wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) uliofanyika Geneva, Switzerland Oktoba 24, 2011.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa Meneja wa Tanzania Network Information Center, Eng. Abibu Ntahigaye, wakati akikagua banda la maonyesho la Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) uliofanyika Geneva, Switzerland Oktoba 24, 2011.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal, akisikiliza maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Tanzania Youth Alliance (TAYOA), Peter Masika, kuhusu namna ya kuwawezesha vijana kutumia teknolojia ya mawasiliano ya kompyuta, wakati akikagua banda la Tanzania katika Mkutano wa Kimataifa wa Mawasiliano (ITU) uliofanyika Geneva, Switzerland Oktoba 24, 2011. Picha na Muhidin Sufiani-OMR
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal ameiwakilisha Tanzania katika mkutano wa ITU (International Telecommunication Union) unaohusu wajibu nchi katika dhana ya mawasiliano unaofanyika jijini Geneva.
Makamu wa Rais ambaye ameambatana na wadau wa masuala ya mawasiliano kutoka Tanzania, sambamba na kushiriki kutoa mada katika mjadala unaohusu ‘Utandawazi na Dunia kuwa kijiji’ mjadala ambao pia umewashirikisha Balozi Philip Verveer wa Marekani, Waziri Mkuu wa Rwanda, David Kanamugire, Naibu Waziri Mkuu wa Bahrain, Shaikh Ali Bin Khalifa Al Khalifa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Senegal Alassane Dialy Ndiaye na kusimamiwa na Mtangazaji wa CNN, Becky Anderson, ametumia fursa hiyo kuuelezea ulimwengu juu ya fursa zinazotokana na Tanzania kuwekeza katika mkongo wa intaneti chini ya bahari ya Hindi ambao kwa kiwango kikubwa umetanua urahisi wa mawasiliano kati ya Tanzania na nchi za Afrika Mashariki na Kusini.
Kupitia mkongo huo, nchi jirani zitarahisisha mawasiliano yake ya Intaneti kupitia Tanzania na taifa litanufaika na gharama za malipo kutoka katika nchi hizo. Malawi ni moja ya nchi ambazo tayari zimeonyesha nia ya kutaka kuunganishwa haraka.
Makamu wa Rais pia amezungumzia ukuaji wa mtandao wa simu ambapo sasa Tanzania kuna kadi za simu milioni 12 ambazo zimesajiliwa na kufafanua kuwa licha ya kuwa idadi inaongezeka katika matumizi ya teknolojia, bado upo uwanda ambao haujatumika hivyo wawekezaji wanakaribishwa sana kuwekeza huku wakifahamu Tanzania ni nchi ya amani na yenye fursa nyingi sambamba na kuwa na watu walio wepesi wa kupokea mabadiliko.
Tanzania inalo banda la maonyesho hapa katika uwanja kunakofanyika mkutano huu wa ITU, banda ambalo linasimamiwa na TCRA, sambamba na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Afya ambao wanelezea namna Tanzania inavyoweza kutoa huduma za afya kwa kutumia teknolojia ya ICT, wahamasishaji vijana kuhusu ugonjwa wa Ukimwi TAYOA na UhuruOne ambao wanajihusisha na utoaji huduma za kielektroniki katika shule mbalimbali sambamba na usambazaji wa vifaa kama kompyuta.
Katika hatua nyingine, Tanzania inaonyesha namna inavyojiandaa kuondokana na mfumo wa urushaji matangazo sambamba na kutoa masafa kwa analojia kuelekea digitali, hali ambayo itaongeza uhuru mkubwa kwa watumiaji sambamba na kuwa na fursa nyingi za kupata matangazo kwa wananchi.
Mfumo huu unahamasishwa na ITU ambayo pia katika mkutano wa mwaka huu, inahamasisha kuhusu namna njema ya kutumia changamoto zinazotokana na magunduzi ya Brodabendi (Broadband) mfumo unaoongeza kasi ya matangazo ya sauti, data na video katika intaneti.
Mkutano huu wa ITU unafanyika huku Tanzania na dunia ikiwa katika mpango wa kumaliza kabisa mfumo wa analojia ifikapo mwaka 2015. Katika Afrika Mashariki, nchi ya Kenya inaonekana kuongoza kufuatia kuwa tayari na sera ya kuingiza mfumo wa kidigitali lakini hali nchini Tanzania kwa mujibu wa TCRA iko juu na inawezekana kabisa kuwa mfumo huo ukawa umefika maeneo yote nchini kabla ya kuzimwa rasmi na Bodi ya dunia.
Katika mkutano huu pia yupo Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Profesa Mbarawa Mnyaa ambaye amehudhuria mikutano kadhaa kwa ngazi ya mawaziri huku akinadi fursa zilizopo katika wizara yake kwa wawekezaji sambamba na kubadilishana uzoefu kuhusu makuzi ya ugunduzi katika sayansi, teknolojia namawasiliano.
Kwa upande wake Makamu wa Rais Dkt. Bilal pia amepata fursa ya kutembelea mabanda ya maonyesho ya nchi jirani kama Rwanda, Kenya, Malawi, Ghana, China, Uganda na Burundi.
Katika mabanda hayo Makamu wa Rais alijionea na kupata taarifa juu ya umuhimu wa mkongo wa Tanzania unaoziunganisha nchi za Afrika Mashariki na Kati katika kupata huduma za Intaneti kwa gharama nafuu na pia umuhimu wake katika kuingiza pato kwa Tanzania.