Oct 14, 2011

Iran yaipa Tanzania trekta 100

IRAN imetoa trekta ndogo aina ya Power tiller 100 kwa Serikali ya Muungano wa Tanzania katika kusaidia kuinua na kuimarisha kilimo nchini na hasa kuunga mkono malengo ya Mpango wa Kilimo Kwanza. Mchango huo mkubwa wa kusaidia kuinua na kuboresha kilimo cha Tanzania, umeelezwa na Balozi wa Iran nchini, Mohsen Movahhedi Ghumi kwa Rais Jakaya Kikwete wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi huyo. Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika, Ikulu, Dar es Salaam, Balozi huyo alimweleza Rais Kikwete kuwa trekta hizo ndogo zenye thamani ya dola za Marekani 600,000 zimenunuliwa kutokana na sehemu ya msaada wa maendeleo wa Iran kwa Tanzania. Mwaka jana, Tanzania na Iran zilitiliana saini makubaliano ambako Iran iliahidi kuipatia Tanzania msaada wa maendeleo wa dola za Marekani milioni 1.2. Sehemu ya msaada huo ndiyo imetumika kununulia trekta hizo na kiasi kinachobakia cha dola za Marekani 600,000 kitatumika kujenga kliniki ya kisasa mjini Dar es Salaam kwa ajili ya kuongeza huduma za afya kwa wakazi wa jiji hilo. Pia Iran itatoa msaada wa dola za Marekani milioni moja kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.