Oct 12, 2011

Mwinyi-Viongozi wa dini mnanuka



I
Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, amesema viongozi wa dini kutoka Tanzania wanatia aibu na kuchangia Watanzania kunuka nje ya nchi kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya.

Mzee Mwinyi alitoa kauli hiyo jana mbele ya viongozi hao na kusimulia mkasa uliomkuta yeye binafsi wa kupekuliwa kupita kiasi katika kiwanja cha ndege nje ya nchi, akishukiwa kuwa kiongozi wa dini kutoka Tanzania anayesafirisha dawa za kulevya.

Alikuwa akizindua Baraza la Viongozi wa Dini la Kupambana na Athari za Dawa za Kulevya jana Dar es Salaam katika hafla iliyoandaliwa na asasi ya kiraia ya American International Health Alliance (AIHA).

“Ninachokisema kuna maneno mengi ya aibu yanasemwa kuhusu Watanzania, aibu zaidi hata kwa wacha Mungu wa Tanzania sasa hawaaminiki, wanatumia fursa walizonazo kuficha na kusafirisha dawa za kulevya.

“Nilikuwa naenda Ujerumani hivyo nililazimika kubadili ndege katika moja ya nchi huko ughaibuni, wakati wa kupanda ndege ya pili tukaanza kukaguliwa. Ilipofika zamu yangu, nilikaguliwa sana, lakini hawakutosheka, nikaingizwa kwenye chumba cha pembeni, nikavuliwa viatu na koti wakanikagua kwa mashine na mwisho wakanipapasa mwili mzima,” alisema Mzee Mwinyi.

Alisema alikumbana na kadhia hiyo pamoja na hadhi yake ya kidiplomasia kwa vile tu alikuwa ameshikilia tasbihi (rozari) mkononi, jambo lililofanya ahisiwe kuwa ni kiongozi wa dini anayesafirisha dawa za kulevya.

“Yule aliyenikagua alikuwa akifanya kazi yake, amenifundisha, lakini nataka mjue Watanzania wenzangu kuwa tunanuka huko nje,” alisema Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa wakati wa utawala wake.



Mzee Mwinyi alilazimika kutoa mkasa huo uliompata miaka mingi iliyopita bila kutaja mwaka wala uwanja husika mbele ya viongozi hao wa dini mbalimbali ili kufikisha ujumbe kwao kuwa Tanzania inanuka kwa kuhusishwa na dawa za kulevya.



Alisema mmoja wa wasaidizi wake alijaribu kumnusuru katika hali hiyo kwa kumtahadharisha ofisa wa uwanja huo wa ndege kuwa huyo anayemkagua ni mwanadiplomasia.



“Lakini bwana yule alimjibu tena kwa ukali ‘I don’t care’ (sijali), wakaendelea kunikagua wanavyotaka baadaye nikajiuliza kwani imekuaje wakanikagua vile, nikagundua kuwa ni kwa vile nimebeba tasbihi,” alisimulia Mzee Mwinyi.


Alisema alionekana kama mwanadini anayetumia alama ya tasbihi ili apitishe dawa za kulevya kirahisi, jambo ambalo lilimsikitisha na wakati anaondoka uwanjani hapo, alilazimika kumkabidhi yule ofisa aliyemkagua tasbihi yake kama zawadi.



Kauli hiyo ya Mzee Mwinyi, imetolewa baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwataka viongozi wa dini kukemea uhalifu huo na kutahadharisha kuwa sasa biashara hiyo imeaanza kuvutia viongozi wa dini.



Rais Kikwete alitoa kauli hiyo alipokuwa akiwahutubia waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo la Mbinga, kwenye ibada maalumu ya kupewa kuwekwa wakfu Mhashamu Askofu John Ndimbo wa Jimbo hilo.



Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema Serikali imejipanga kuhakikisha kunakuwa na sheria moja yenye nguvu itakayoziba mianya yote inayojitokeza katika sheria za dawa za kulevya.



Alisema kwa sasa sheria zilizopo zina mianya mikubwa ambayo inasababisha mapapa wa biashara hiyo na vipapa vidogo vinavyokamatwa kuishia kulipishwa faini ya Sh. milioni moja na kutoka.



“Sheria inasema wazi ukikamatwa na dawa za kulevya unalipishwa mara tatu ya gharama ya mzigo wa dawa hizo, kifungo cha miaka 30 au maisha lakini hivi kweli mmeshawaona watu wakifungwa kwa kosa hilo, lazima kuwe na marekebisho katika sheria hizi,” alisema



Kamishna wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya, Christopher Shekiondo, alisema kikosi kazi maalumu kilichopo chini ya Tume hiyo kimekamata watu wengi wanaotuhumiwa kufanya biashara hiyo.



Takwimu zinaonesha mwaka 2008 hadi mwaka huu, watuhumiwa 22,814 walikamatwa nchini na 67 nje ya nchi huku idadi ya dawa zilizokamatwa ikiongezeka.



Kwa mujibu wa Shekiondo, dawa zilizokamatwa zimeongezeka kutoka heroine kilo 100 kutoka mwaka 2000 hadi 2009 hadi kilo 154 mwaka jana na mwaka huu; na cocaine kilo 57 mwaka 2000 hadi 2009 hadi kufikia kilo 191 mwaka 2010 hadi mwaka huu.



Baraza hilo la Viongozi wa Dini kazi yake ni kuhamasisha vijana kuepuka biashara na matumizi ya dawa za kulevya na linaongozwa na Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Salum.