Nov 11, 2011

China Kukuza Sekta Ya Utalii -Tanzania

China Kukuza Sekta Ya Utalii -Tanzania:
|
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Maimuna Tarishi (mwenye miwani) akimkaribisha Makamu Gavana wa Jimbo la Jiangxi la China, Bw. Zhu Hong Makao Makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii, Mpingo House tayali kwa majadiliano ya kusaini makubaliano ya mashirikiano ya kukuza sekta ya utalii nchini, leo asubuhi. Kushoto ni Afisa Mkuu wa Utalii, Bi. Lilian Nyaki.
Makamu Gavana wa Jimbo la Jiangxi la China, Bw. Zhu Hong (kushoto) akimkabidhi kitabu kinachoelezea vivutio vya utalii vya jimbo hilo Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Maimuna Tarishi.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii akimkabidhi Makamu Gavana wa Jimbo la Jiangxi la China, Bw. Zhu Hong kitabu kinachoelezea vivutio vya vilivyopo nchini kulia ni Afisa Mkuu wa Utalii, Lilian Nyaki akijiandaa kumpa CD ya vivutio vya nchini.
Makamu Gavana wa Jimbo la Jiangxi la China akimkabidhi kitabu kinachoelezea vivutio vilivyopo jimboni mwake Mkurugenzi wa Idara ya Utalii, Bw. Ibrahim Mussa (wapili kulia) huku akishuhudiwa na Afisa Mkuu wa Utalii na katibu mkuu.
Ujumbe kutoka Jimbo la Jiangxi la China ukiwa katika picha ya pamoja na ujumbe wa Tanzania mara baada ya kumaliza majadiliano ya jinsi pande hizo mbili zitakavyosaidia kukuza sekta ya utalii.
Wizara ya Maliasili na Utalii hivi leo imepokea ujumbe kutoka Jimbo la Jiangxi nchini China uliongozwa na Makamu Gavana, Bw. Zhu Hong kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kusaini Mkataba wa Mashirikiano (MoU) katika kukuza Sekta ya Utalii baina ya pande hizo mbili.
Ujumbe huo ulioongozwa na Makamu Gavana, Bw. Zhu Hong uliambatana na wakurugenzi mbalimbali wa masuala ya maendeleo pamoja na wajumbe kutoka Ubarozi wa China nchini umelenga kuangalia uwezekana wa kushirikiana na Tanzania katika kuboresha shughuli za utalii kwa kubadirishana taarifa, kuimarisha miundombinu, kutangaza vivutio vya utalii n.k.
Akiupokea ujumbe huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Bi. Maimuna Tarishi mapema hivi leo, alisema ujio wa ujumbe huo unaweza kuleta tija katika sekta ya utalii nchini kwa kuwekeza katika tafiti mbalimbali na kuendeleza rasilimali watu.
“Hapa nchini hivi sasa utalii uliopo ni wawanyamapori lakini tukiwekeza katika miji mikubwa kama Jiji la Dar es Salaam na fukwe zake kama ilivyo kwa wenzetu Zanzibar watalii wengi watavutiwa kutalii mjini kabla ya kwenda mbugani, ushirikano wetu ukilitazama hili tutainua uchumi wan chi yetu,” alisema Bi. Tarishi.
Lakini Jimbo la Jiangxi kwa upande wao, wamesema kwamba jimbo hilo lenye wakazi wengi zaidi ya idadi ya Watanzania licha ya kusheheni vivutio vingi vya utalii hutembelewa zaidi na wazawa na idadi ndogo ya Waafrika.
Makamu Gavana, Bw. Zhu Hong alisema wameamua kuja nchini kuangalia fursa za kuwekeza katika sekta ya utalii kwa sababu ushirikiano kati ya China na Tanzania unaimarika siku hadi siku katika mambo ya uchumi na biashara.
Gavana huyo aliongeza kuwa anaima muafaka baina ya pande hizo mbili utafikiwa na katika kuhakikisha hilo ataualika ujumbe wa Tanzania jimboni mwake kujionea vivutio viliyopo kwa kuwa anaamini usemi usemao ‘seeing is believing’.
Picha na Habari kwa Hisani ya Afisa Habari wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Bw. Tulizo Kilaga