Nov 1, 2011

KAMPUNI YA LIMA MBEYA YAPEWA KIBALI CHA KUNUNUA KAHAWA MBICHI

KULIA NI MENEJA WA KAMPUNI YA LIMA MR.NZUNDA AKIWA ANATOA MAELEKEZO KWA NAIBU WA WIZARA YA KILIMO CHAKULA NA USHIRIKA INJINIA CHRISTOPHER CHIZA HIVI KARIBUNI. (Picha na maktaba ya www.kalulunga.blogspot.com)
KITENDAWILI kilichokuwepo kati ya Halmashauri ya wilaya ya Mbozi mkoani Mbeya, kampuni ya lima na kikundi cha wakulima wanaojishughulisha na ununuzi wa kahawa mbichi wilayani, kimeteguliwa na Wizara ya kilimo, chakula na ushirika.
Wizara hiyo imetegua Kitendawili hicho kwa kuipa leseni ya kununua kahawa kavu na mbichi kampuni ya Lima tofauti na matarajio ya kikundi cha Mviwata kilichokuwa kikionekana kutetea maslahi ya wakulima wilayani Mbozi na kutetewa na Halmashauri hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Meneja wa kampuni hiyo ya Lima Tingson Nzunda, huku akionesha leseni hiyo, amesema kuwa kampuni yake imeamua kuweka wazi leseni hiyo ili kuwaondoa hofu wananchi waliokuwa wakitishwa na Halmashauri ya Mbozi kuwa hawapaswi kuuza kahawa mbichi kwa kampuni hiyo.
Nzunda amesema kumetokea wizi wa mapato ya Serikali unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara kupitia kwa kile wanachokiita kuunda vikundi ambavyo hapo awali vilikubalika na Serikali ili kuwarahisishia wakulima kukusanya mazao yao na kupeleka kwenye makampuni ya ununuzi.
Amesema wajanja hao wametumia mwanya huo kuiibia Serikali kwa kuanza kununua kahawa mbichi kwa wakulima kisha kuiuza katika masoko ya ndani na nje ya nchi tofauti na Msingi halali wa uanzishwaji wa vikundi hivyo.
Aidha amesema kuwa umefika wakati kwa Serikali ili kutoendelea kupoteza mapato yake kutokana na ununuzi wa kahawa mkoani Mbeya unaofanywa na vikundi hivyo, ni muhimu vikundi hivyo vikasajiliwa kama kampuni ili vilipe kodi kwasababu havikusanyi kahawa hiyo kwa wakulima bali hununua kama makampuni yaliyosajiliwa na kulipa kodi ikiwemo kampuni ya Lima.
Kampuni hiyo ya Lima inajishughulisha na ununuzi wa Kahawa mbichi, kukoboa na kusindika kisha kuuza katika soko la ndani ya nchi ambalo lipo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro na nje ya nchi. Hata hivyo msimamo wa halmashauri ya wilaya ya MBOZI upo pale pale kwamba hakuna mtu atakayenunua kahawa mbichi licha ya leseni hiyo kutolewa katika mazingira yenye utata. Halmashauri imesisitiza katika kikao chake cha mwishoni mwa mwezi September kuwa hakuna mtu atakayenunua kahawa cheri kwalengo la kulinda maslahi ya wananchi na pia kusimamia mapato ya halmashauri ambayo yamekuwa yakivuja kupitia mfumo wa kuuza kahawa cheri. Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Ambakisye alieleza katika kikao hicho kuwa wanaruhu wananchi kuchukua hatua zozote ikiwa makampuni yatakaidi hatua hiyo na kwamba hatua ya kununua kahawa cheri inalenga kudidimiza uzalishaji wa kahawa wilayani humo kwakuwa bei ambao wakulima wanalipwa ni ya unyonyaji.