Nov 16, 2011

MITAMBO YA UMEME ILIVYOLIPUKA UBUNGO

MOTO mkubwa umezuka jana kwenye Makao Makuu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na kuunguza kifaa kiitwacho ‘reactor’ kinachotumika kudhibiti mfumo wa usambazaji umeme katika jiji la Dar es Salaam hali iliyosababisha jiji hilo kukosa umeme. Tukio hilo lililotokea saa 10:45 jioni, lilisababisha kukatika kwa umeme katika jiji hilo na viunga vyake huku uongozi wa ukisema haijajulikana tatizo hilo lingechukua muda gani kutatuliwa. Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Sophia Mgonja aliwaambia waandishi wa habari kwamba: “Hadi sasa hatujui chanzo na wala athari zake. Umeme umekatika jiji zima na hatuwezi kurudisha hadi tutakapofanya uchunguzi kuona kiwango cha uharibifu.” Alisema kifaa hicho kilichoungua kinachokadiriwa kuwa na thamani ya Dola za Marekani 500,000 (takriban Sh 900milioni) hakitengenezeki na badala yake kinatakiwa kuagizwa kingine. Mgonja alisema mbali ya kifaa hicho vingine kama ‘Control Cable’ pamoja na vikombe vya kwenye nguzo ambavyo vilikuwa havionekani kutokana na kufunikwa kwa moshi huenda navyo vimeteketea.“Kuanzia sasa mafundi wanaanza kazi ya kuchunguza chanzo cha tukio hilo lakini pia kuona namna tunavyoweza kurudisha umeme kwa wakazi wa jiji la Dar es Salaam”. Mkuu wa zamu wa Kikosi wa Kikosi cha Zimamoto wa Jiji la Dar es Salaam, Seleman Said alisema kikosi hicho kiliwasili katika eneo hilo saa 11:03 baada ya kupata taarifa saa 10:45 jioni. Alisema baada ya kuwasili, walielezwa kuwa kifaa hicho kina mafuta hivyo kulazimika kuchanganya maji na dawa ili kuwezesha kazi hiyo kufanywa kwa ufanisi.“Kazi tuliifanya kwa muda wa dakika saba na katika muda wa dakika 20 tulikuwa tunamalizia kuhakikisha moto huo haulipuki tena,” alisema Said.