Nov 20, 2011

PROFESA CHRIS MAINA PETER ACHAGULIWA KUWA MJUMBE WA KAMISHENI YA SHERIA ZA KIMATAIFA ZA UMOJA WA MATAIFA

maafisa, kutoka kushoto, Bw. S. Shilla na Bw. Assah Mwambene kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, wakiwa na Kaimu Balozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Dr. Justin Seruhere wakipongezana baada ya Profesa Chris Maina Peter kutangazwa kuwa ni mmoja kati ya wagombea tisa kutoka kundi la Afrika walioshinda uchanguzi wa kuwania nafasi ya ujumbe wa Kamisheni ya Umoja wa mataifa inayoshughulikia sheria za kimataifa. katikati ni Bi Tully Mwaipopo akijaribu kumtafuta kwa simu Profesa Maina ili kumpatia habari njema za ushindi wake katika uchaguzi huo ambao kura zake zilipigwa kwa siri. Jumla ya wagombea 34 kati ya 49 wakiwakilisha mabara mbalimbali walishinda katika uchaguzi huo.
Afisa mshauri wa masuala ya sheria na uchaguzi katika Ubalozi wa Tanzania Umoja wa Mataifa, Bi, Tully Mwaipopo akiendelea na kampeni ya kugawa vipeperushi vyenye wasifu wa Profesa Chris Maina Peter aliyekuwa akigombea nafasi ya ujumbe katika Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayohusika na masuala ya sheria za Kimataifa, katika uchaguzi uliofanyika siku ya Alhamis katika ukumbi Mkuu wa Mikutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. New York
Na Mwandishi Maalum,New York
Profesa Chris Maina Peter, Muhadhiri Mwandamizi wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, amechaguliwa kuwa mjumbe wa Kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayoshughulikia masuala ya Sheria za Kimataifa ( International Law Commission).
Wajumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, katika mkutano wao uliofanyika siku ya Alhamis, hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, jijini New York. Walipiga kura ya siri kuwachagua wajumbe 34 kati ya 49 waliotakiwa kuingia katika Kamisheni hiyo.
Rais wa Baraza Kuu la 66 la Umoja wa Mataifa, Balozi Nassir Abdulaziz Al- Nasser alimtaganza Profesa Chris Maina Peter kutoka Tanzania, kuwa ni mmoja ya wagombea Tisa kati ya Kumi na Tatu kutoka Afrika ambao wameshinda na hivyo kuingia katika Kamisheni hiyo.
Profesa Chris Maina Peter ameshinda uchaguzi huo, uliokuwa na ushindani mkubwa akichuana na wagombea wengine 13 waliosheheni sifa na weledi wa hali ya juu katika nyaja ya sheria za kimataifa wakiwamo mabalozi na watu mashuhuri kama aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Kenya Bw. Amos S. Wako.
Wagombea wengine mbali ya wale tisa kutoka Afrika, walikuwa ni Nane kutoka kundi la nchi za Asia, Watatu kutoka kundi la Ulaya Mashariki, Sita kutoka kundi la Amerika ya Latini na Visiwa vya Caribbean na Wanane kutoka nchi za Ulaya ya Magharibi na nchi nyingine.
Profesa Chris Maina Peter, atakuwa mjumbe wa Kamisheni hiyo kwa kipindi cha miaka mitano kuanzia Januari 2012.
Katika kiny’anga’nyiro hicho, wagombea kutoka kundi A ambalo ni Afrika lilikuwa na wagombea 13 lakini waliotakiwa ni 9 tu hali iliyopelekea ushindani mkubwa na hasa ikizingatiwa kwamba, kati ya wagombea hao 13 , sita walikuwa wakiomba kurejea tena kwa mara ya pili.
Mbali ya Tanzania, wengine kutoka Kundi la Afrika walioshinda ni wagombea kutoka Afrika ya Kusini, Egypt, Msumbiji, Nigeria, Algeria, Kenya,Libya na Cameroon.
Ushindi wa Profesa Chris Maina Peter umetokana kwanza, uthubutu, wasifu,na weledi binafsi wa Profesa Maina, uratibu na ushirikiano mkubwa kati ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa ambako, maafisa wake wakiongozwa na Balozi wao Mhe. Ombeni Sefue, walifanya kazi kubwa na maandalizi mazuri ya kufanikisha uchaguzi huo.
Profesa Chris Maina Peter yeye binafsi, akiongozwa na Afisa wa Ubalozi wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa,anayehusika na Kamati ya Sita ya Masuala ya Sheria na Uchanguzi alifanya kampeni kwa takribani wiki zima akikutana na Mabalozi na Maafisa mbalimbali hapa Umoja wa Mataifa.
Akizungumza wa njia ya simu kutoka Addis Ababa Ethiopia, Profesa Chris Maina Peter amesema, ameyapokea matokea hayo kwa furaha kubwa huku akiwashukuru wale wote waliofanikisha uchaguzi huo.
Ushindi wa Profesa Peter unakuja ikiwa ni takribani wiki moja tangu Balaza Kuu la Umoja wa Mataifa kumthibitisha Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, (CAG) Bw. Ludovic Utouh kuwa mjumbe wa Bodi ya Ukaguzi wa Hesabu za Umoja wa Mataifa (UNBOA).
Tanzania kupitia Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania NAOT imeteuliwa kujaza nafasi itakayoachwa wazi mwakani na Afrika ya Kusini katika UNBOA. Bw. Ludovic Utouh atafanya kazi na wajumbe wengine wa bodi hiyo kutoka China na Uingereza.