Nov 15, 2011

WAZEE-VURUGU ZA MBEYA ZIMEICHAFUA SERIKALI NA SISI KWA UJUMLA

MKUU WA MKOA WA MBEYA ABBAS KANDORO
MNARA WA MAKUMBUSHO YA MASHUJAA ULIOPO KATIKATI YA JIJI LA MBEYA.
*Vurugu za Mbeya zawaamsha,wadai hawana shida ya ajira.
*Wamkimngia kifua Kandoro kuwa hakuhusika kutoa amri.
Gordon Kalulunga na Jerome Nkulu, Mbeya
UMOJA wa wazee Jijini Mbeya (UWAJIMBE) umesema kuwa vurugu zilizojitokeza Jijini hapa hivi karibuni kati ya wafanyabiashara wadogo maarufu kama wamachinga zimechafua sifa ya amani na utulivu iliyozoeleka kuwepo Tanzania tangu ilipopata uhuru wake.
Wakizungumza na waandishi wa habari leo katika ukumbi wa mikutano wa Hoteli ya Mbeya Peack iliyopo Jijini Mbeya walisema kuwa vurugu hizo zimechafua sifa ya nchi na mkoa huo, watu wake na taifa kwa ujumla.
Akizungumza kwa niaba ya wazee hao waliokuwa wamekusanyika katika ukumbi huo, Mwenyekiti wa Umoja huo Isakwisa Mwambulukutu alisema kuwa vurugu hizo licha ya kuchafua sifa ya mkoa huo pia zimemchafua Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro ambaye ni mgeni na hakuhusika na maamuzi yoyote yaliyosababisha vurugu hizo.
‘’Taarifa yetu kwa umma kwanza ni kulaani vikali vurugu hizo zilizojitokeza kati ya Novemba 11-12, mwaka huu na kwamba zimetuchafua wakazi wa Mbeya na kumchafua Mkuu wa mkoa ambaye tunaamini si kiini cha vurugu hizo kwasababu yeye ni mgeni’’ alisema Mwambulukutu.
Alisema kuwa umoja huo haupendi zijitokeze tena vurugu za namna hiyo kwasababu zinavuruga sifa zilizozoeleka ndani ya nchi na nje kuwa Tanzania ni kisiwa cha Amani na utulivu.
Mwambulukutu alisema kuwa wazee hao wanalaani na kukemea vikali vurugu hizo kwani zimesababisha kuvunjika kwa mshikamano wa wananchi, zimedhoofisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na Serikali kwa ujumla na kwamba vurugu hizo zimempa taswira tofauti ya wananchi wa Mbeya Mkuu wa mkoa Abbas Kaondoro wakati si taswira halisi.
Sanjari na hayo wazee hao walitoa ushauri kwa Serikali na wananchi waliohusika katika vurugu hizo kuwa umefika wakati kwa Serikali na wafanyabiashara wanapokosa maelewano ni muhimu kuwashirikisha wazee hao ambao hawahitaji gharama zozote ili kuepusha vurugu kama zilizojitokeza hivi karibuni badala yake itumike busara zaidi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha waandishi wa habari mkoa wa Mbeya(MBPC), Christopher Nyenyembe alisema kuwa waandishi wa habari mkoa wa Mbeya wanaunga mkono taarifa ya wazee hao kwa sababu palipo na wazee hapakosi busara na hekima.
Alisema kuwa katika vurugu hizo kuna miundombinu iliyoumizwa bila sababu mfano barabara za lami zilizounguzwa na moto uliotokana na magurudumu kuchomwa jambo ambalo lingeepukika kama wataalam wa mipango miji waliopo Jijini hapa wangetumia vema taaluma zao.
Nyenyembe alisema kuwa ipo haja ya idara ya mipango miji kuangalia upya muundo wa jiji hilo kiramani kwa kuwa licha ya kukabiliana na hali hiyo bado kuna tatizo kubwa la kudhibiti uvamizi katika maeneo mengine hasa kwa miji inayokuwa kwa kasi ili kuepuka ujenzi holela uliojikita katika maeneo ya Mwanjelwa. kutoka kalulungablog