Aug 10, 2012

SEKRETARIETI YA AJIRA YATANGAZA RATIBA YA USAILI MWEZI HUU


Katibu wa Sekretarieti ya Ajira, Bw. Xavier Daudi akifafanua jambo kwa Waandishi wa habari (hawapo pichani) na kushoto kwake ni Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Ajira, Bw. Bakari Mahiza.

Sekretarieti ya Ajira imetangaza ratiba ya usaili kwa mwezi Agosti, 2012 kwa waombaji nafasi za kazi katika Taasisi za Umma kwa wale waliokidhi vigezo. Tangazo hilo limetolewa leo na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira, Bw. Xavier Daudi alipokuwa akiongea na Waandishi wa habari ofisi kwake.
Daudi amesema usaili huo utafanyika katika Mikoa sita ambayo ni Dodoma, Morogoro, Manyara, Arusha, Dar es Salaam na mkoa wa Pwani.
Amesema usaili umeanza tarehe 6 hadi 7 Agosti, mwaka huu kwa mkoa wa Manyara, wilaya ya Babati kwa nafasi za Mtendaji wa Kata, Kijiji na Madereva, ilihali kwa mkoa wa Dodoma umeanza tarehe 7-9 Agosti, 2012 katika Chuo cha Serikali za Mitaa, Hombolo kwa nafasi Wahadhiri wasaidizi, Afisa Utumishi, Afisa Tawala, Watunza kumbukumbu, Madereva na Wasaidizi wa Ofisi.
Aidha, usaili utafanyika pia katika Chuo cha Mipango Dodoma (IRDP) kuanzia tarehe 10-14 mwezi huu kwa kada za Afisa Ugavi, Afisa Utumishi, Mkutubi na Afisa Mitaala. Wakati katika Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Biashara (COASCO) utaanza tarehe 15-16 Agosti kwa kada za Wakaguzi wa hesabu wa ndani, Wakaguzi Wasaidizi wa hesabu wa ndani na nafasi ya Katibu Mahususi.
“Kwa mkoa wa Morogoro usaili utafanyika tarehe 15-16 mwezi huu katika Taasisi ya Tanzania Official Seed Certification Institute (TOSCI) kwa kada za Wakaguzi Wasaidizi wa hesabu wa ndani, Afisa Kilimo, na kwa Katibu Mahususi”. Alisema Daudi.
Ameongeza kuwa kwa mkoa wa Arusha usaili utafanyika tarehe 10-11 Agosti katika Tume ya Mionzi Tanzania (TAEC) kwa nafasi za Wataalamu wa Mionzi, Fizikia, Uhasibu, Ukatibu Mahususi, Msaidizi wa Ofisi na Ulinzi. Aidha, usaili utaendelea katika mkoa wa Pwani, wilaya ya Bagamoyo katika Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA) kwa nafasi ya Mkufunzi na Mkufunzi Msaidizi daraja la kwanza na la pili.
Katibu amesema usaili huo utamalizikia kwa mkoa wa Dar es Salaam ambao unatarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 23 hadi 31 Agosti kwa awamu hii ambao utakuwa kwa Vyuo vya elimu ya juu ikiwemo Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Chuo cha kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Chuo cha Biashara (CBE). Aidha, utafanyika pia katika Taasisi ya Utafiti wa Samaki Tanzania (TAFIRI) na Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) ambao utahusisha nafasi za Wakufunzi, Afisa Utumishi, Afisa Mitaala, Afisa Viwango, Madereva na Katibu Mahususi.
Katibu wa Sekretarieti ya Ajira amesema nia ya kufanya usaili katika mikoa husika kwanza ni kufikisha huduma karibu na wateja wetu na pia kuwapunguzia gharama za kusafiri mbali na eneo alilokuwa ameomba kazi husika. Aliongeza kuwa ili kupata maelezo zaidi juu ya usaili huo ni vyema wakatembelea tovuti ya Sekretarieti ya Ajira ambayo ni www.ajira.go.tz ili kupata ufafanuzi zaidi.