Aug 14, 2012

TAASISI ZA WAMA NA EOTF HAZITUMII RASILIMALI ZA SERIKALI

NA MAGRETH KINABO- DODOMA, MAELEZO
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Utawala Bora,Kapteni George Mkuchika amesema kuwa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo(WAMA) na Taasisi ya Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote(EOTF) zilianzishwa na kuandikishwa kwa mujibu wa sheria inayotawala taasisi hizo na wala hazitumii rasilimali za serikali.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuchika wakati akijibu swali Bungeni la Mbunge wa Viti Maalum(CHADEMA) , Naomi Kaihula ililoulizwa na Leticia Nyerere Viti Maalum (CHADEMA) kuwa kuwekuwepo na tabia ya wake wa marais hapa nchini kuunda NGO’S na kuzisajili kama taasisi zao binafsi wakati zinatumia rasilimali za serikali.
Je seriklai itaweka lini utaratibu wa kufanya taasisi hizo ziwe za kisheria ili hata wake wa marais wanapomaliza muda wao wapokezane vijiti kana urais unavyofanywa.
Waziri Muchika akifafanua kuhusu swali hilo alisema ni kweli zipo taasisi zinazoendeshwa wake za marais .Hivyo taasisi hizo hufanya shughuli zake kama zilivyo taasisi nyingine zisizo za kiserikali. Ipo taasisi ya WAMA iliyoanzishwa na Mke wa Rais wa Awamu ya Nne Mama Salma Kikwete na EOTF iliyoanzishwa na Mke wa Rais wa Awamu ya Tatu , Mama Anna Mkapa
Aliongeza kuwa kama zilivyo taasisi zingine za hiari na zisizo za kiserikali (NGO,S). Taasisi hizo ziliundwa kutegemea na jinsi Mke wa Rais navyopenda kujishughulisha na shughuli za kijamii.
Alisema inawezekana kabisa akatokea Mke au Mme wa Rais ambaye hana utashi au mapenzi ya kujishughulisha na shughuli za kijamii. Hivyo kutokana na mazingira hayo serikali haioni sababu za kuweka utaratibu wa kufanya taasisi hizo ziwe za kisheria ili wake / waume za marais wanapomaliza muda wao wapokezane vijiti.
Aliongeza kuwa kwa kufanya hivyo tutakuwa tunawalazimisha kufanya shughuli wasizo na utashi nazo.
Akijibu swali la nyongeza la Leticia liliouliza kuwa Watanzania wananufaikaje na taasisi hizo bila tofauti za kiitikadi. Waziri Mkuchika alisema hakuna anayefanya kazi kwa kubagua na alizipongeza taasisi hizo kwa kufanya kazi mijini na vijijini huku akiwataka Watanzania kuanzisha taasisi mijini na vijijini .
Alisema jumla ya wanafunzi 939 wamenufaika kielimu kupitia (WAMA). Pia WAMA imetoa msaada wa vitanda na magodoro katika wodi za wakina mama na imetoa kiasi cha fedha sh. milioni mbili kwa ajili ya ujenzi wa hospitali ya wanawake ya MEWATA, ambazo ni msaada kutoka Taasisi ya Nakayama, Japan.
Aidha alisema ina mpango wa kutoa vifaa vya hospitali vyenye thamani y a dola za Marekani milioni tatu kupitia msaada wa Project Care, Marekani vinavyotarajia kuingia nchini.
Alisema taasisi ya EOTF imetoa mafunzo kwa wajasiliamali mbalimbali.
Mwisho.