Feb 23, 2013

TANZANIA NA MALAWI ZAJA NA MPANGO WA KUTAJIRISHA WILAYA SITA ZA MPAKANI





Na Danny Tweve wa Indabaafrica blog

Wilaya  nne  za Tanzania na Mbili za nchini Malawi zitanufaika na miradi mikubwa inayokusudiwa kuanzishwa kupitia mto songwe itakayogharimu Euro 400 Milion (zaidi ya Trilion moja za Kitanzania) katika  kipindi cha miaka kumi kuanzia mwezi march mwaka huu.

Miradi hiyo imeibuliwa ikiwa ni sehemu ya suluhisho lakudumu la maafa ya kuhama hama kwa mto songwe na kusababisha upotevu wa mali, uhai wa watu na pia mipaka baina ya Tanzania na Malawi kuhama hama kila msimu wa mafuriko ya mto huo

Akitambulisha hatua za utekelezaji wa Program ya Maendeleo ya Bonde la Mto Songwe , mratibu wa  program hiyo upande wa Tanzania Mhandisi Gabriel Kalinga ambaye pia aliongozana na afisa wa upande wa Malawi  pamoja na Meneja wa Program hiyo  kwa ujumla faida za awali ya miradi hiyo mikubwa ni pamoja na ujenzi wa mabwawa matatu kwa upande wa Tanzania yatakayozalisha umeme Megawati 430

Vivyo hivyo kwa upande wa Malawi wilaya za Chitipa na Kalonga zitanufaika na miradi hiyo ambapo pia jumla ya mabwawa matatu yatajengwa na kuzalisha umeme pamoja na fulsa nyingine za kiuchumi ikiwemo kilimo cha umwagiliaji.

Kulingana na matakwa ya mpango huo miongoni mwa hatua muhimu za utekelezaji wa hatua ya pili ya program huyo ni pamoja na kubaini wadau wa Bonde husika na hatimaye kutambulisha nia ya utekelezaji wa mradi huo ili waweze kutoa maoni yao, hatua ambayo ujumbe huo umeendelea kufanya kwa wilaya za Kyela, Rungwe, Mbozi na Ileje.

Mhandisi Kalinga alisema tayari wameshateua makampuni mawili  ya Ushauri wa hatua ya kufanya usanifu na maandalizi ya uwekezaji ambapo kampuni ya Lahmeyer International GmbH ya Ujerumani na Arab Consulting Engineers Moharram –Bakhoum (ACE) ya Misri ambayo pia  ilishiriki katika kuandaa mchoro wa  daraja la Kigamboni kwa pamoja  zitaanza kazi hiyo march mwaka huu.
Kulingana na maelekezo ya mkataba kampuni hizo zitatekeleza ushauri huo kwa kipindi cha miaka miwili  na kwamba katika kipindi chote nchi mbili za Malawi na Tanzania  zitatoa pia wataalamu watakaoshirikiana nazo katika utekelezaji na kwamba hatua hiyo ni muhimu katika kurithisha utaalamu na ujuzi kwaaajili ya uendelezaji wa miradi mingine baadaye.

Hatua ya kufanya usanifu  na maandalizi ya uwekezaji (detailed design and investment preparation) inatarajiwa kugharimu kiasi cha euro 6,135,515 huku kiasi kikubwa kikichangiwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika kupitia mfuko wake wa Africa Water Facility Special Fund (itachangia euro 3,549,000), wakati  NEPAD kupitia mfuko wake wa Miundombinu itachangia euro 1,226,295  na nchi za Malawi na Tanzania zitachangia  Euro 1,360,220

Kulingana na Meneja wa Program hiyo Mhandisi Saidi Abbas Faraj  mabwawa ya uzalishaji umeme yatajengwa katika eneo la Mpaka wa wilaya ya Kyela na Ileje na mengine mawili kwa upande wa Tanzania yatajengwa katika wilaya ya Ileje wakati kwa upande wa Malawi yatajengwa katika wilaya za Kalonga na Chitipa.

Amesema hatua hiyo licha ya kutoa fulsa za kiuchumi kwa wananchi wa pande mbili za mpaka wa Malawi na Tanzania kupitia mto Songwe zikiwemo Kilimo cha umwagiliaji, utalii, ufugaji samaki na uvuvi na matumizi ya nyumbani pia yatatumika kupunguza maafa kwenye jamii hasa wilaya ya Kyelana Kalonga  ambako mafuriko yamekuwa yakijitokeza na kuhamisha wananchi kutoka nchi moja na kwenda nyingine kutokana  mto kuhama hama.

Tayari maandalizi ikiwemo ofisi za menejimenti ya mpango huo zimefunguliwa wilayani kyela ambako utekelezaji wake wa siku hadi siku utakuwa ukisimamiwa wakati ofisi za bodi zitakuwa Malawi
Mwisho